Shirika la Habari la Hawza - Moja kati ya masuala muhimu na ya msingi kabisa katika kipindi cha ghaiba ni suala la "wilaya" na uongozi wa masuala ya Waislamu.
Ni wazi kuwa tangu mwanzoni mwa kuja kwa Uislamu, suala la "wilaya" na uongozi wa umma lilikuwepo, na Mtume Mtukufu (saw) pamoja na maimamu ma’sumīn (as), si tu kuwa walikuwa wakielezea dini na sheria ya Uislamu pamoja na mafundisho yake, bali pia walikuwa ndio maimamu, viongozi na wenye mamlaka juu ya umma, yaani Waislamu wote walikuwa na wajibu wa kuwatii wao katika mambo yote ya mtu binafsi na kijamii, na hakuna Muislamu yeyote Mshia ana shaka kuhusu ukweli huu.
Swali hapa linajitokeza ni hili: Baada ya ghaiba ya Imam wa kumi na mbili (as), uongozi na uimamu wa umma uko mikononi mwa nani? Je, mtu mmoja au watu fulani wana mamlaka juu ya umma? Ikiwa kuna mamlaka, mipaka yake ni ipi?
Katika kujibu swali hili la msingi, tangia zamani suala la "wilayatul-faqīh" lilikuwa likijadiliwa.
Ufafanuzi wa dhana ya Wilayatul-Faqīh
Neno “wilaya” limetokana na mzizi wa neno “walī”, na asili ya maana yake ni kuwepo kwa kitu kando ya kitu kingine, pamoja na kuwepo uhusiano kati yao, hivyo, limekuja pia kwa maana ya urafiki, msaada na ufuasi.
Moja kati ya maana muhimu na inayotumika sana ni "uongozi na kusimamia masuala ya wengine", Kwa maana hii, “walī” ni mtu ambaye anasimamia na kuwajibika kwa mambo ya wengine, na anawasimamia wao, maana hii ndiyo inayokusudiwa katika dhana ya "wilayatul-faqīh".
Neno “faqīh” limetokana na mzizi wa neno “fiqh”, linalomaanisha "ufahamu na elimu", na kwa kiasi kikubwa linahusishwa na elimu ya dini, “Faqīh” ni mtu ambaye ana uelewa kamili wa maarifa na hukumu za Kiislamu na ni mtaalamu katika hayo; yaani kwa kuzingatia elimu pana aliyopata katika nyanja mbalimbali za elimu, anaweza kutoa hukumu ya Mwenyezi Mungu katika masuala ya mtu binafsi na kijamii kutoka katika Qur’ani na riwaya za Kiislamu.
Historia ya nadharia ya Wilayatul-Faqīh
Baadhi ya watu hudhani kuwa "wilayatul-faqīh" ni jambo jipya lisilo na historia katika fiqhi na elimu ya fiqh ya Kiislamu, na kwamba limetokana na fikra za kisiasa za Imam Khomeini (r.a), Hali ya kuwa dhana hii ni potofu kabisa, inayotokana na kutokuwa na taarifa kuhusu "fiqhi" na pia athari za ma’sumīn (as).
"Wilayatul-faqīh" ina mizizi katika maneno ya ma’sumīn (as), Wao,kutokana na dharura za kidini na kijamii, walieleza mamlaka na uongozi kwa mafaqihi, na baada yao, daima "wilayatul-faqīh" imekuwa ikijadiliwa katika mitazamo ya mafaqihi wakuu wa Kiislamu, Hapa tunataja mifano kadhaa:
"Sheikh Mufid (mw. 413 Hijria)", mmoja wa mafaqihi wakubwa wa Kishia, anasema:
“Wakati ambapo sultani mwadilifu -ambaye ni Imam ma’sum (as)- hayupo kwa ajili ya uongozi, basi ni juu ya mafaqihi wa haki, waadilifu, wenye maoni bora, akili na fadhila, kuchukua jukumu la uongozi na kusimamia yale ambayo kwa kawaida yako chini ya mamlaka ya sultani mwadilifu.”
(Al-Muqni‘ah, uk. 675)
"Sheikh Tusi (mw. 460 Hijria)", anayefahamika kama "Sheikh al-Ta’ifah", anasema:
"Kutoa hukumu baina ya watu, kusimamisha hudud, na kuhukumu baina ya waliotofautiana haifai ila kwa mtu aliyeruhusiwa kutoka kwa sultani wa haki (Imam ma’sum (as)), mambo haya, wakati ambapo maimamu hawana uwezo wa kuyatekeleza wao wenyewe, bila shaka yanakabidhiwa kwa mafaqihi wa Kishia.”
(al-Nihayah wa Nukatuhā, j. 2, uk. 17)
"Al-Muhaqqiq al-Thānī" maarufu kama "Muhaqqiq Karaki" ( 940 Hijria) anasema:
“Mafaqihi wa Kishia wameafikiana kuwa faqīh mwadilifu wa Kishia aliyekamilika kwa masharti ya kutoa fatwa, katika zama za ghaiba, ni naibu wa Maimamu waongofu (as) katika mambo yote yanayowezekana kuwakilishwa.”
(Rasā’il, j. 1, uk. 142)
"Mullā Ahmad Narāqī", maarufu kama "Fādhil Narāqī" (1244 Hijria), anasema:
“Kila ambacho Mtume (saw) na Imam (as), ambao ni watawala na walinzi wa Uislamu, walikuwa na mamlaka nacho, basi faqīh naye anayo mamlaka hiyo hiyo, isipokuwa tu panapokuwepo ushahidi wa kuiondoa.”
(ʿAwā’id al-Ayyām, uk. 187–188)
Ayatollah Gulpaygani (r.a.), mmoja wa mafaqihi wakubwa wa zama hizi, anasema:
“Mipaka ya mamlaka ya mafaqihi ni mipaka ya jumla… mipaka ya wilaya ya faqīh mwenye sifa katika mambo yanayohusiana na uongozi na usimamizi wa jamii ni kama ilivyo mipaka ya mamlaka ya Maimamu (as), isipokuwa tu pale dalili inapotenga jambo fulani.”
(al-Hidāyah ilā man lahu al-Wilāyah, uk. 79)
Haya ni baadhi tu ya maneno ya mafaqihi wa Kishia katika karne mbalimbali, kuna mamia ya mifano mingine yenye uwazi ambayo inaonesha kuwa suala la "wilayatul-faqīh" daima limekuwa likijadiliwa katika fikra na matamshi ya wanazuoni wa Kishia na limekubaliwa na wengi wao.
Faqīh mkubwa wa zama hizi na kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, "Imam Khomeini (r.a.)", kwa kuwa na maarifa ya hali ya wakati na hekima isiyo na mfano, alieleza waziwazi nadharia hii ya Kiislamu na kidini, na akaasisi mfumo wa Kiislamu kwa msingi huo, yaani, alitekeleza suala la "wilayatul-faqīh" katika uwanja wa kijamii wa Waislamu na kulitangaza kuwa ndiyo mfumo kamili kabisa wa utawala wa kidini katika zama za ghaiba.
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Negin-e Āfarinish”, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Rejea
1. Mufradāt Raghib, neno “Walī”
2. Lisān al-ʿArab, j. 13, neno “Fiqh”
3. Al-Muqni‘ah, uk. 675
4. Al-Nihāyah wa Nukatuhā, j. 2, uk. 17
5. Rasā’il – Al-Muhaqqiq al-Karaki, j. 1, uk. 142
6. ʿAwā’id al-Ayyām, uk. 187–188
7. Al-Hidāyah ilā man lahu al-Wilāyah, uk. 79
Maoni yako