Alhamisi 23 Oktoba 2025 - 13:20
Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Lebanon: Kauli za Imam Khamenei Zinaleta Utulivu na Fakhari

Hawza/ Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Lebanon imesema kwamba maneno ya Mtukufu Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei kuhusiana na matamshi ya Rais wa Marekani aliyedai kwamba alishambulia sekta ya nyuklia ya Iran — ambayo ni dhana potovu — ni kauli zinazotoa utulivu na fahari, kwani zinathibitisha uthabiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya changamoto zote.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tajama cha  Shirika la Habari la Hawza, bodi ya uongozi ya Jumuiya hiyo, baada ya kikao chake cha kawaida, ilitoa tamko lake ikisema: “Kama ilivyotokea Lebanon ambapo makubaliano ya kusitisha vita na azimio namba 1701 yalivunjwa, ndivyo maadui Wazayuni wanavyovunja makubaliano ya kusitisha vita huko Ghaza, wakishambulia maeneo ya kiraia na raia wasio na hatia, na kupuuza makubaliano hayo. Hivyo pia wanazuia kuingia idadi ya misafara ya misaada ya kibinadamu inayosubiria kwenye mipaka ya Ghaza.”

Tamko hilo liliongeza kuwa: “Adui Mzayuni amekiuka makubaliano ya kusitisha vita zaidi ya mara 80 huko Ghaza, jambo lililosababisha kuuwawa mashahidi 97 na kujeruhiwa watu 230. Hii ina maana kwamba vita bado vinaendelea, na Marekani haijatekeleza ahadi yake iliyotolewa na Rais wake, Donald Trump, ya kusitisha vita; bali imekuwa ikilinda uvamizi wa utawala wa Kizayuni, kama inavyofanya pia kuhusu uvamizi wa utawala huo nchini Lebanon.”

Jumuiya hiyo iliendelea kusema: “Kutokana na uvamizi huu, wanamuqawama jasiri wa Ghaza walijibu kwa operesheni za kishujaa dhidi ya adui Mzayuni, jambo lililosababisha kuuawa kwa afisa mmoja na askari mmoja wa kikosi cha ‘Nahal’, katika tukio ambalo jeshi la Kizayuni lenyewe lililitaja kuwa ‘hatari’.”

Wanazuoni hao walibainisha kuwa: “Uvamizi wa Wazayuni dhidi ya raia wasio na hatia haukuishia Ghaza pekee, bali umeenea hadi Ukingo wa Magharibi, ambapo askari wa utawala wa Kizayuni walivamia mji wa Nablus na kuwafyatulia risasi raia wasio na silaha, na kujeruhi watu kumi na mmoja.”

Tamko hilo liliendelea kueleza: “Mabasi ya walowezi Wazayuni yalivamia eneo la mashariki mwa mji wa Nablus na kuelekea kwenye kaburi la Nabii Yusuf (a.s.), katika jitihada za kulazimisha hali ya kivitendo inayopetuka makubaliano yaliyofikiwa kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni, huku mamlaka hiyo ikikaa kimya na kutofanya chochote mbele ya uvamizi wa Wazayuni.”

Jumuiya hiyo iliongeza: “Mamlaka ya Ndani ya Palestina bado imezama ndani ya makubaliano ya usalama na utawala wa Kizayuni, ikishirikiana katika kuwatambua wapiganaji wa muqawama na kuwakamata ili kuwakabidhi kwa wavamizi wa Kizayuni, na hivyo kuzima harakati za upinzani kote Ukingo wa Magharibi.”

Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Lebanon pia ililaani mashambulio ya mara kwa mara yaliyofanywa na adui Mzayuni dhidi ya maeneo ya Al-Mahmudiyya na Al-Jarmaq katika wilaya ya Al-Nabatiyya, pamoja na uvunjaji wa anga ya Lebanon kupitia ndege zisizo na rubani (drones), zilizoruka kwa urefu wa wastani juu ya Beirut na Dahiya Kusini, bila hatua yoyote kuchukuliwa na serikali ya Lebanon kuwasilisha malalamiko katika Baraza la Usalama, baada ya mazungumzo na kamati ya ufuatiliaji wa usitishaji vita huko Naqoura kutozaa matunda.

Mwisho, Jumuiya hiyo ilisisitiza kuwa: “Kauli zilizotolewa na Mtukufu Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei kuhusiana na matamshi ya Rais wa Marekani aliyedai alishambulia sekta ya nyuklia ya Iran, kwamba hayo ni mawazo ya kufikirika na waendelee na ndoto hizo, ni maneno yanayotoa utulivu na fahari kubwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara mbele ya changamoto zote na inaendelea kupambana na ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani hadi ushindi wa mwisho na kutokomea kabisa kwa utawala wa Kizayuni.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha