Jumatano 10 Desemba 2025 - 23:11
Kioo cha Unabii: Wakati Binti wa Mtume Alipokuwa Katika Daraja la Unabii

Hawza/ Bibi Fatima Zahra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) aliishi siku sabini na tano baada ya Mtume, na katika kipindi hiki Jibril Amin alikuwa akiteremka mara kwa mara juu yake na kueleza mambo ya baadaye, yakiwemo masuala ya kizazi na mwendelezo wa risala; fadhila ya kipekee kwake, na maalumu kwa manabii wa daraja ya juu kabisa na mawalii maalumu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kukaribia kwa siku za kuzaliwa kwa Bibi Fatima Zahra (salamu za Mwenyezi Mungu zimshukie), tunawasilisha kwa wasomi waheshimiwa dondoo ya kauli za marehemu Ayatollah Misbah Yazdi kuhusu nafasi na haiba ya Bibi wa walimwengu wawili.

Imam Ja‘far Sadiq (amani iwe juu yake) anasema:


“Fatima (amani iwe juu yake) aliishi siku sabini na tano baada ya baba yake, na huzuni na majonzi mengi yalimtawala; Jibril Amin alikuwa akimjia, akimpa pole, na akimweleza mambo ya baadaye.”

Muonekano wa riwaya unaonesha kuwa katika siku hizi 75, kulikuwa na mawasiliano endelevu; yaani kuja na kwenda kwa Jibril kulikuwa kukubwa na kwa mfululizo. Sidhani kwamba tukio kama hili limewahi kumpata mtu mwingine yeyote isipokuwa wale wa tabaka la kwanza la manabii wakubwa.

Jibril Amin, katika kipindi cha siku 75, alikuwa anakwenda, akieleza masuala yatakayotokea siku za usoni, na Amirul Muuminin Ali (amani iwe juu yake) alikuwa akiyaandika. Amirul Muuminin (a.s.), kama vile alivyokuwa mwandishi wa wahyi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, alikuwa pia mwandishi wa wahyi wa Bibi Siddiqa (salamu za Mwenyezi Mungu zimshukie) ndani ya siku hizi 75.

Suala la kushuka kwa Jibril si jambo jepesi; isidhaniwe kwamba kushuka kwa Jibril kunawezekana kwa kila mtu.

Ni lazima kuwepo uwiano kamili kati ya daraja na utukufu wa Jibril—ambaye ni Ruhu Mtukufu—na roho ya yule anayeteremkiwa na Jibril.

Iwe, kama baadhi ya wana nadharia wanavyosema, kwamba kushuka kwa Jibril kunatokana na roho adhimu ya nabii au wali mwenyewe, na kwamba ni roho hii tukufu ya nabii au wali inayomteremsha Jibril; au kama baadhi ya wanazuoni wa dhahiri wanavyosema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anayempa Roho tukufu jukumu la kushuka—kwa hali yoyote ile, uwiano kamili kati ya pande mbili ni lazima na ni muhimu. Bila ya kuwepo uwiano wa kiroho na Jibril aliye Roho Mkuu, kushuka hakuwezekani.

Uwiano kama huu umekuwepo tu kati ya Jibril na roho tukufu za manabii wa daraja ya kwanza, kama vile Ibrahim, Musa, Isa, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (amani iwe juu yao).

Uhusiano wa aina hii haujawahi kuwapo kwa kila mtu. Hata kuhusu Maimamu pia, sijaona imepokewa kwamba Jibril aliteremka juu yao kwa namna hii.

Daraja hii ni maalumu kwa Bibi Fatima Zahra (amani iwe juu yake), ambapo Jibril katika kipindi cha siku hizi 75, aliteremka mara kwa mara juu yake na kueleza masuala ya baadaye yatakayowakumba kizazi chake, na Amirul Muuminin alikuwa akiyahifadhi kwa kuyaandika.

Inawezekana kwamba miongoni mwa masuala aliyoyaeleza ni mambo yatakayotokea katika zama za kizazi chake kilicho cha juu zaidi, yaani Hadhrat Sahib (amani iwe juu yake).

Kwa vyovyote vile, mimi ninachukulia heshima na fadhila hii ya Bibi Fatima Zahra (amani iwe juu yake) kuwa juu kuliko fadhila zote walizomtajia—ingawa nazo ni fadhila kubwa—kwa sababu ni fadhila ambayo, isipokuwa kwa manabii (amani iwe juu yao), na tena si kwa manabii wote, bali kwa tabaka la juu kabisa la manabii na baadhi ya mawalii walio katika daraja lao, haijamfikia mtu mwingine yeyote. Na maelezo yanayoonesha uhusiano endelevu na mawasiliano ya siku 75 mfululizo hayajawahi kutokea kwa yeyote mpaka sasa. Hii ni miongoni mwa fadhila maalumu za Bibi Siddiqa (amani iwe juu yake).

Chanzo: Kitabu Jami‘ Az Zilal Kauthar, ukurasa wa 36 na 37.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha