Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, hotuba za Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao na waandaaji wa Kongamano la Kuadhimisha Mashahidi 5,580 wa Mkoa wa Alborz Iran, zilirushwa leo usiku katika ukumbi ulio fanyika kongamano hilo mjini Karaj Iran.
Katika kikao hiki, Ayatollah Khamenei alielezea moja ya kazi muhimu katika hali ya sasa kuwa ni kuhamisha motisha na thamani za kipindi cha Ulinzi Mtakatifu kwenda kwa kizazi cha vijana, na akasema: Vijana wetu wa leo ni vijana wazuri, na licha ya kuwepo kwa nyenzo za kisasa sana za kuhamisha maudhui na dhana mbalimbali katika fikra zao, wamefanikiwa kulinda utambulisho wao wa kidini; na ni lazima kutumia mazingira haya kueleza na kuhamisha kwa njia ya kisanaa thamani hizo kwa vijana.
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alieleza shauku ya kukutana na Mwenyezi Mungu na hisia ya wajibu wa kidini miongoni mwa wapiganaji wa Ulinzi Mtakatifu kuwa ni miongoni mwa thamani na motisha nyingi za kipindi hicho, na kwa kusisitiza kwamba hairuhusiwi motisha hizi zisahaulike, aliongeza: Mienendo ambayo mtu huiona kutoka katika baadhi ya taasisi za kitamaduni na baadhi ya vyombo vya uwajibikaji haioneshi jitihada na dhamira ya kuhamisha thamani za Ulinzi Mtakatifu.
Ayatollah Khamenei, kwa kusisitiza kwamba kuhamisha thamani na motisha za kipindi cha Ulinzi Mtakatifu kwenda katika kizazi kipya kunahitaji kazi ya kisanaa na ufuatiliaji usiokoma, alibainisha: Pamoja na ugumu wote, dhiki za maisha na matatizo yaliyopo, kuna mambo mengi chanya na maandalizi mengi katika nchi kwa ajili ya kusonga mbele kuelekea Uislamu na Mapinduzi, ambayo ni lazima yaimarishwe.
Aidha, kwa kuwatukuza wananchi wa Mkoa wa Alborz hususan familia za mashahidi wa mkoa huu na kuwashukuru waandaaji wa kongamano la kuadhimisha mashahidi wa Alborz, alielezea mahudhurio ya watu kutoka maeneo mbalimbali ya Iran kwenye mji wa Karaj kuwa ni faida, na akasema: Ikiwa kuadhimisha mashahidi na kuhamisha ujumbe na thamani za mashahidi hao kutafanywa ipasavyo, kutokana na faida hii kuna uwezekano wa kuyahamisha pia katika maeneo mengine ya nchi.
Soma hapa chini matini kamili ya hotuba ya Mtukufu Ayatollah:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote; na rehma na amani zimshukie kiongozi wetu na Nabii wetu Abul-Qasim al-Mustafa Muhammad, na Aali zake watoharifu, watukufu na wateule.
Karibuni sana ndugu wapendwa, dada wapendwa! Nami nawashukuru sana kwa juhudi mlizozifanya kuanzisha mfumo huu wenye manufaa na kwa maana fulani ya kimaisha, yaani mfumo wa kufufua kumbukumbu na majina ya mashahidi, katika mji wa Karaj na katika Mkoa wa Alborz.
Mkoa wa Alborz una sifa maalumu kama ilivyotajwa na waheshimiwa; ni mkusanyiko wa watu wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya nchi, ambao katika miongo kadhaa iliyopita wamehamia katika mji huu. Kwa hiyo, kila kazi njema inayofanyika katika mji huu kuna uwezekano ikasambaa katika nchi nzima na ikaathiri pia maeneo mengine. Hivyo basi, kazi yenu ni kazi njema sana, na hatua mliyochukua ni ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na yenye manufaa. Mimi nawashukuru waandaaji wa kazi hii.
Hoja ya kwanza hapa ni kwamba; katika maelezo yenu kuhusu mipango ya kongamano hili, mlitaja mambo mazuri — waheshimiwa wote wawili (1) mlieleza mambo muhimu, mkataja athari zinazotarajiwa kutokana na kazi hii — lakini haya ni matarajio yenu; na ni lazima yatimie. Hili linahitaji kufikiriwa; yaani, kitabu kile ni lazima kipate wasomaji, filamu ile ni lazima ipate watazamaji; na hili linahitaji juhudi ya pili.
Yaani, ikiwa kazi haitafanywa kwa njia ya kisanaa, au haitafuatiliwa, au pande zote za kazi hazitazingatiwa, basi juhudi hii iliyofanywa vizuri na kwa wakati unaofaa haitafikia malengo yake. Ni lazima mfanye kazi kwa namna ambayo juhudi hii ifikie malengo yake; na hii yenyewe inahitaji juhudi ya pili. Nataka niseme kwamba kufikiria kazi njema na kupanga mpango mzuri ni nusu ya kazi; nusu ya pili — ambayo ni muhimu zaidi — ni ufuatiliaji, kuendeleza na kutekeleza kazi hiyo; na hili ndilo mnalo takiwa kulifanya.
Hoja nyingine hapa ni suala la maadhimisho haya; kwa nini tunafanya maadhimisho haya? Tunapowachunguza mashahidi wa vita vya kulazimishwa, mashahidi wa vita hivi vya hivi karibuni, kwa ujumla mashahidi wengi wa vita hivi, tunaona kwamba walikuwa na motisha fulani zilizowasukuma kuingia katika uwanja wa hatari na wakati mwingine kupoteza maisha yao; na kulikuwa na wengine wengi pia waliokuwa na motisha hizo hizo, lakini kwa fadhila za Mwenyezi Mungu walirejea wakiwa salama. Motisha hizo ni zipi? Kwa nini kijana anaacha maisha ya starehe, kuwa karibu na wazazi wake, masomo, kazi, ndoto, ajira na kila kitu, na anaingia katika magumu ya vita na taabu zake — na wale waliokuwa katika uwanja huu wanajua magumu yake — na anajitosa mwenyewe katika hatari?
Ikiwa tutapunguza harakati hii kubwa na tendo hili tukufu na kulifanya kuwa hisia tu, tutakuwa tumedhulumu; kusema kwamba hotuba zilihutubiwa, hisia za vijana hawa zilichochewa, wakasimama na wakaenda vitani; hii kwa hakika ni dhulma kwa tukio hili na kwa watu hawa; sivyo ilivyokuwa. Kuna mambo mengine; yahesabuni, yatambueni.
Moja [ya motisha hizi] ni “shauku ya kukutana na Mwenyezi Mungu.” Miongoni mwa vijana hawa tunawajua, ni watu ambao kwa maana halisi ya neno walikuwa na shauku ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu; yaani, walifanya yale aliyoyaashiria Imam kuhusu wakubwa wa maarifa na wasafiri kiroho, aliposema: "mmeabudu kwa maisha yenu yote, huenda ika kubalika", lakini nendeni mkasome pia wasia wa kijana huyu; kijana huyu wakati mwingine amepita njia ya miaka sabini au themanini katika miezi au hata siku chache na akafikia huko. Suala hili la shauku, shauku ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, ni lazima liundwe kwa vijana. Suala la “hisia ya wajibu wa kidini” — kwamba hili ni jukumu, ameambiwa alitekeleze, na ni lazima alitekeleze; kama swala; ni lazima lifanyike. Suala la “hisia ya kukabiliana na adui”; hii ni hisia muhimu sana. Kijana anapofikia kiwango cha ufahamu wa ujana wake — pale anapotoka katika hatua ya utoto na ujana mdogo — anahisi kuwa ana jukumu fulani kwa nchi yake ambalo ni lazima alitekeleze; na anahisi kuwa kuna watu wanaongojea kuipora nyumba yake, nchi yake, na urithi wake wa kitamaduni na kistaarabu; na anataka kusimama dhidi yao. Hii ni hisia ya kibinadamu; na mambo mengine kama haya. Huenda mtu akaweza kuorodhesha motisha kumi muhimu mfululizo kwa harakati hii ya vijana hawa, ambayo sasa nyinyi mnaifanya na mnaitekeleza. Haya yote ni lazima tuyahamishie kizazi kijacho; huu ndio ujumbe wangu.
Nasema kwamba ni lazima msiruhusu motisha hizi zizimike; motisha hizi ni lazima zihamishiwe kizazi kijacho. Mienendo ambayo mtu huiona kutoka katika baadhi ya taasisi za kitamaduni na baadhi ya taasisi za uwajibikaji na wale wanaopaswa kuwaza mambo haya, hawaoneshi hilo; yaani, kwa kweli hatuoni katika matukio mengi kwamba dhana hizi tukufu na thamani hizi zinahamishiwa kwa vijana.
Vijana wetu ni vijana wazuri. Vifaa vilivyopo leo havikuwepo katika kipindi cha vita vya kulazimishwa na mwanzoni mwa Mapinduzi; vyombo hivi vya kisasa sana vya kuhamisha ujumbe, dhana na maudhui katika fikra za watu na kuwaathiri, havikuwepo wakati huo; leo kijana wetu anavikabili na kuvipinga. Yule anayeswali swala ya usiku, anayetekeleza ibada za ziada, anayehudhuria msikitini, anayehudhuria majlisi na maombolezo, kwa hakika anahifadhi na kuimarisha utambulisho wake wa kidini mbele ya mawimbi haya makubwa; hili ni jambo lenye thamani kubwa sana; tunapaswa kulithamini.
Vijana wetu wa leo kwa mtazamo wangu ni vijana wazuri sana na wako tayari; mpango wetu unapaswa kuwa ni kuweza kufafanua thamani hizi zilizozaa shahada, ukuu huu na kujitolea huku katika taifa la Iran, na kuzipeleka kwenye kizazi kijacho ili waweze, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kuiendeleza nchi na jamii.
Kwa bahati njema, pamoja na magumu yote, dhiki za maisha na matatizo yaliyopo, tuna mambo mengi chanya katika nchi, na mtu anaona maandalizi mengi katika nchi kwa ajili ya kusonga mbele kuelekea Mapinduzi na kuelekea Uislamu; hili linaonekana wazi. Tunatarajia, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, mambo haya yaimarishwe, na kazi yenu iweze katika njia hii kufanya kazi kubwa sana; na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu mtaweza kufanya kazi hii katika eneo lenu. Kama nilivyosema, msijitosheleze na mkoa wenu tu; yaani, fanyeni kwa namna ambayo wale wanaohusiana na wilaya nyingine, miji mingine na maeneo mengine ya nchi, wabebe zawadi hii kutoka hapa, waipeleke kwao, waandae fikra, mwelekeo na maandalizi, na thamani hizi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, zisambae hadi maeneo mengine ya nchi.
Mwenyezi Mungu awape nyinyi mafanikio, awasaidie na awawezeshe ili, kwa idhini Yake, mfikie lengo mlilolikusudia kwa kufanya kazi hii; na Mwenyezi Mungu awakubalie nyinyi na ndugu wote. Nasi tunawasalimia wananchi wapendwa wa Karaj, hususan familia za mashahidi wapendwa.
Amani iwe juu yenu, na rehema na baraka za Mwenyezi Mungu.
(1) Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kongamano na Katibu Mkuu wa Kongamano.
Maoni yako