Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika hafla hiyo, wazazi, walezi, walimu pamoja na wageni waalikwa walipata fursa ya kushuhudia maendeleo ya elimu na malezi ya watoto wao, shule hiyo inaendelea kutoa elimu kwa kuzingatia misingi ya taaluma sambamba na maadili ya Kiislamu, lengo likiwa ni kuwajenga wanafunzi wenye nidhamu, maarifa na hofu juu ya Mwenyezi Mungu.
Wanafunzi waliomaliza muhula wao walitunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali kulingana na ufaulu wao wa masomo, nidhamu na ushiriki wao katika shughuli za shule. Hatua hiyo ililenga kuwahamasisha wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao na kuendelea kufanya vizuri zaidi katika vipindi vijavyo.
Aidha, walimu na viongozi wa shule walitumia fursa hiyo kutoa nasaha kwa wanafunzi, wakisisitiza umuhimu wa elimu, utii kwa wazazi na walimu, pamoja na kuzingatia maadili mema katika maisha yao ya kila siku. Wazazi pia walihimizwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na shule katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao.
Kwa ujumla, mahafali ya pili ya Lady Zahraa Islamic Pre and Primary School imekuwa na mafanikio makubwa na pia imeonesha jitihada zinazofanywa na uongozi wa shule katika kukuza elimu bora inayochanganya elimu ya kisasa, malezi na misingi ya dini kwa watoto.





Maoni yako