Jumatano 10 Desemba 2025 - 19:00
Msimamo wa Kichochezi wa Wanaodai Kuhifadhi Uhuru wa Mamlaka, kwa Hakika ni wa Khiyana na Unaendana na Adui wa Kizayuni

Hawza/ Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon katika taarifa yake ulisema: Adui bado anaendelea na hujuma zake kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano na Azimio namba 1701, na kwa mfululizo wa mashambulizi ya anga na kwa droni, analenga vijiji vya eneo la Jabal Amel.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, katika taarifa yake baada ya kikao chake cha mara kwa mara, ulieleza kuwa: wakati wawakilishi wa kimataifa wanakuja Lebanon mmoja baada ya mwingine kwa lengo la kumaliza hali ya vita iliyosababishwa na uvamizi wa upande mmoja wa adui wa Kizayuni, adui huyu bado anaendelea na hujuma zake kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano na Azimio namba 1701, na kwa mfululizo wa mashambulizi ya anga na ya droni, analenga vijiji vya eneo la Jabal Amel.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa: badala ya Walebanon wote kusimama katika safu moja dhidi ya hujuma hii, baadhi ya wanaodai kulinda “uhuru wa mamlaka” nchini Lebanon, hutoa kauli zinazoendana na misimamo ya adui wa Kizayuni; yule yule adui aliyotekeleza uhalifu wa kikatili kabisa dhidi ya watu wa Lebanon. Ni kana kwamba sehemu kubwa ya taifa ambalo sasa liko chini ya moto wa mashambulizi si sehemu ya Lebanon, na uwepo wake hauhesabiwi kuwa sharti la kutimia kwa uhuru wa mamlaka ya nchi.

Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu, huku ukikaribisha msaada wowote wa kimataifa kwa ajili ya kusimamisha hujuma za Kizayuni, ulisisitiza kuwa: msaada huo haupaswi kufungamanishwa na sharti lolote; kwa kuwa Lebanon imezingatia na kutekeleza kikamilifu vipengele vyote vya Azimio namba 1701, bali hata imechukua hatua zaidi ya azimio hilo kwa yale ambayo adui wa Kizayuni alidai kupitia Marekani. Kwa hiyo, msaada wowote unapaswa kwanza kabisa kumtaka adui wa Kizayuni atekeleze wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano, yakiwemo: kujiondoa kikamilifu katika ardhi za Lebanon alizozikalia kabla ya hujuma, na pia maeneo aliyoyakalia baada ya vita vya hivi karibuni; kuwaachilia huru wafungwa wote wa Kilabanoni; na kusitisha mashambulizi ya anga, baharini na nchi kavu dhidi ya uhuru wa mamlaka ya Lebanon.

Mkusanyiko wa wanazuoni uliendelea kusema: baada ya utekelezaji wa wajibu huu, ndipo itakapowezekana kujadili masuala mengine yoyote — hata suala la silaha za muqawama linaweza kujadiliwa ndani ya mazungumzo ya kitaifa na ya ndani, katika muktadha wa kuandaa mkakati wa ulinzi wa taifa, ambapo silaha za muqawama zitakuwa sehemu yake.

Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeelezwa: jana tulishuhudia katika maeneo mbalimbali ya Lebanon maandamano yaliyoambatana na kauli mbiu za kichochezi kwa kumuunga mkono Ahmad al-Sharaa (al-Julani); lau si kuingilia kati kwa wakati na kwa njia inayostahili kwa Jeshi la Lebanon, kauli mbiu hizi zingeweza kuifikisha nchi kwenye ukingo wa janga kubwa.

Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu ulisisitiza: tunawataka wakimbizi wa Kisyria waheshimu nchi yao inayowahifadhi, kwa kuwa wao ni wageni nchini Lebanon. Ni wajibu wao kujiepusha na tabia au kauli mbiu zozote za kichochezi, ili hali isielekee kwenye fitna ya ndani — fitna ambayo hakuna yeyote anayeitamani, na ambayo haitamnufaisha yeyote isipokuwa adui wa Kizayuni. Ni lazima Lebanon itumie nguvu na uwezo wake kupambana na adui mkoloni, si katika migogoro ya ndani.

Katika muendelezo wa taarifa hiyo imeelezwa: Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu unalaani vikali mashambulizi makubwa ya adui wa Kizayuni yaliyoanza tangia usiku wa manane uliopita; mashambulizi ya anga ambayo yalilenga mara kadhaa maeneo ya Jabal Safi katika nyanda za juu za Iqlim al-Tuffah. Vilevile unalaani kupenya kwa majeshi ya adui katika viunga vya eneo la al-Rahib kuelekea Telat Shawat, karibu na kijiji cha Aita al-Shaab, pamoja na kupenya kwa majeshi mengine ya Kizayuni hadi katikati ya kijiji cha al-Adaysah na kulipua nyumba moja karibu na uwanja wa manispaa.

Mkusanyiko huu pia ulisema: tunalaani msimamo wa kichochezi wa wanaodai kuhifadhi uhuru wa mamlaka, ambao badala ya kulaani hujuma za mara kwa mara za Kizayuni dhidi ya kusini mwa Lebanon, Bonde la Biqaa na Dhahiya ya Kusini, wameelekeza mashambulizi yao dhidi ya muqawama na silaha zake. Msimamo huu, kwa hakika, ni wa khiyana na unaendana na matakwa ya adui wa Kizayuni, na ni lazima uzuiwe.

Mwisho, Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu, ukiwapa pongezi Saraya al-Quds kwa upinzani wao wa kishujaa katika Ukingo wa Magharibi, ulisema: tunapongeza mapambano yao ya kishujaa dhidi ya uvamizi wa jeshi la Kizayuni, hususan operesheni iliyofanikiwa ya kikosi cha kivita katika eneo la al-Silah al-Harithiyya, ambapo kwa kulipua bomu katika njia ya msafara wa kijeshi wa adui kulipelekea kusababisha hasara ya moja kwa moja kwa mojawapo ya magari ya kijeshi. Tunatoa wito wa kuongezwa na kushadidiwa kwa mapambano hadi pale jeshi la Kizayuni litakapoondoka kikamilifu kutoka Ukingo wa Magharibi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha