Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, zifuatazo ni dondoo za baadhi ya aya za Qura'n ambazo kwa kila siku fuatilieni baadhi ya vipengele vya “Aya ambazo hujenga Maisha”; mkusanyiko wa aya za Qur’ani Tukufu pamoja na tafsiri fupi na zilizo na matumizi ya kivitendo, ambazo ni mwongozo wa maisha na mafanikio.
Hujjat al-Islam wal-Muslimin Jawad Muhaddithi:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu;
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 139 ya Suratul Āli ‘Imrān:
«وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن کُنتُم مُّؤْمِنِینَ»
Wala msilege, wala msihuzunike; nanyi ni bora ikiwa nyinyi ni Waumini.
Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa lengo la kuchora taswira ya jamii iliyo bora na ambayo ni kielelezo, ametoa maelekezo mbalimbali. Miongoni mwa maelekezo hayo ni kujiepusha na udhaifu, kulegea na kuporomoka katika njia ya imani na maadili ya kidini. Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba katika njia ya dini, itikadi na maadili tunayoyaamini, hatupaswi kudhalilika, kulegea wala kukosa hamasa.
Vilevile, hatupaswi kuzama katika huzuni na masikitiko; kwa kuwa huzuni ni masikitiko yanayotokana na kutofikia lengo au kupoteza kile tulichokuwa nacho. Lakini Mwenyezi Mungu anasema: “Msiwe na huzuni wala msilege”; kwa sababu “nyinyi ni bora, iwapo mna imani.”
Maagizo haya ya kusimama imara na kudumu katika njia ya haki yamesisitizwa pia katika aya nyingine za Qur’ani. Miongoni mwazo ni aya maarufu:
«إِنَّ الَّذِینَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا...»
Hakika wale wanaosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakasimama imara.....
Kwa hivyo, yeyote anayeshikamana na imani na misingi yake, na akaonesha ustahimilivu na uthabiti katika njia ya imani na itikadi, atakuwa bora na kuinuliwa daraja.
Kauli mbiu kongwe iliyokuwapo katika historia ni hii: «الإِسْلَامُ یَعْلُو وَلَا یُعْلَی عَلَیْهِ» yaani: Uislamu upo juu, wala hakuna kitu kinachokuwa juu yake. Kwa msingi huo, Umma wa Kiislamu pia utakuwa bora, lakini kwa sharti la kuwa na imani ya kweli.
Mwenyezi Mungu anasema:
«وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن کُنتُم مُّؤْمِنِینَ»
Yaani: Nyinyi Waislamu ni bora, iwapo kwa hakika mmeamini na mkashikamana na maadili ya Mwenyezi Mungu.
Ubora wa Umma wa Kiislamu unategemea imani thabiti, ustahimilivu katika njia ya haki, na kushikamana na maadili ya Mwenyezi Mungu. Hakuna nguvu yoyote itakayoweza kuwashinda Waislamu wanaodumu katika misingi na imani zao; kama Mwenyezi Mungu alivyoahidi, Ataufanya Uislamu uonekane na kutawala juu ya dini zote. Sharti la kutimia kwa ahadi hii ni kwamba Waislamu waache kulegea na udhaifu, wasiruhusu huzuni na kukata tamaa vitawale nyoyo zao, bali kwa imani na uthabiti wapitie njia ya ukamilifu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie tuwe miongoni mwa waja Wake wanaoshikamana kwa dhati na dini na mwenendo wa Mwenyezi Mungu.
Maoni yako