Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti Mkuu wa Jaafari, katika hotuba yake kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya siku arobaini tangia kufariki mlezi Mustafa Yahfoufi huko Baalbek, alisema: Mwanadamu ndiye kitu kitakatifu kikubwa zaidi cha Mwenyezi Mungu, na hakuna utakatifu wowote kwa maslahi ya mwanadamu isipokuwa kuwepo kwa mamlaka yenye uadilifu. Mwislamu, Mkristo, Sunni, Shia, Druze, Alawi na wengine wote ni waja wa Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kuwa: Nchi ambayo haina uraia safi na uliokomaa ni nchi iliyoshindwa na iliyohukumiwa kusambaratika. Ubaguzi wa kidini hulenga kiini na undani wa uwepo wa waja wa Mwenyezi Mungu katika nchi hii.
Sheikh Qabalan alisema: Hakuna kheri wala maslahi katika mamlaka, serikali au siasa yoyote inayopuuza maslahi ya kitaifa au kuwa na kutojali maumivu na mateso ya taifa na wananchi wake. Ukimya ni usaliti wa amana ya Mwenyezi Mungu iliyowekwa ndani ya mwanadamu, na sisi kamwe hatutaisaliti Lebanon.
Kiongozi huyu wa kidini wa Kishia wa Lebanon aliongeza kusema: Ninawaambia wenye busara wa nchi hii: nchi iko katika hali nyeti sana, na umoja wa kitaifa ni mkate wa uhai wa Lebanon. Jambo hili linatulazimisha kuielewa hali halisi ya kikanda ya Lebanon, kwa kuwa mazingira ya eneo yako wazi kwa uwezekano wote.
Aliendelea kusema: Historia imesisitiza kwamba sisi ni watu wakubwa kuliko migawanyiko na mifarakano, hata kama dunia na eneo vinajaribu kutuvuta kuelekea huko kupitia michezo yao. Tunachohitaji leo ni mamlaka ya kitaifa yenye busara ya kindugu, itakayoichukulia Kusini kama Beirut, Bonde la Beqaa kama Kaskazini, na Jabal Amel kama Mlima Lebanon.
Sheikh Qabalan alisisitiza pia: Mashambulizi ya Kizayuni yanayoikumba Beqaa na Kusini leo ni janga katika uwanja wa mamlaka ya kitaifa, ambalo pia linalenga undani wa mji mkuu, Beirut. Hata hivyo, mamlaka iliyopo imekwama na ipo katika aina mbaya zaidi ya kupooza kwa taifa.
Aliongeza kusema: Pamoja na kwamba Lebanon inakabiliwa na hatari, licha ya kushindwa kwa kiwango kikubwa katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kitaaluma na kifedha, bado wapo wanaotaka kutekeleza miradi ya kimataifa na kikanda kwa gharama ya uhalisia na maslahi ya Lebanon, jambo ambalo linatupeleka moja kwa moja katikati ya mlipuko mbaya zaidi. Sasa ni wakati wa kutathmini hatari na kupima thamani ya kimaslahi ya kitaifa ya Lebanon katika muktadha wa mamlaka ya nchi.
Mufti wa Jaafari alisema: Sisi ni Waarabu, lakini Walebanoni kwanza kabisa ni Walebanoni. Tunachokitaka ni mamlaka ya kitaifa iliyo huru dhidi ya aina yoyote ya ulinzi wa kigeni au udhibiti unaoharibu maslahi ya Lebanon. Kutumia vibaya hali za kikanda na kimataifa kwa ajili ya kuigawa nchi na kulazimisha masharti yanayopingana na mamlaka ya kitaifa hakutapita kamwe; na mamlaka ya kisiasa aidha iwe ya Lebanon yote, au isikuwepo kabisa.
Maoni yako