Ijumaa 30 Januari 2026 - 23:00
Kuwatendea wema wazazi hakuishii katika kipindi cha uhai wao pekee

Hawza/ Hadhrat Ayatollah Subhani amesisitiza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya za Qur’ani Tukufu, anapowszungumzia wazazi, anawaelekeza watoto kwamba hawana haki hata ya kuwatamkia neno dogo kabisa linaishusha heshima ya baba na mama zao.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatollah Ja‘far Subhani, katika kikao cha darsa yake ya maadili kilichofanyika jioni ya Jumatano kwenye Taasisi ya Imam Ja‘far Sadiq (a.s) Pardisan, Qum, Iran alipofafanua umuhimu na nafasi ya kuwatendea wema wazazi wawili alisema: Kumheshimu baba na mama ni jambo la kimaumbile (kifitra), na dalili ya kuwa ni jambo la ulimwengu mzima na la wote ni kuenea kwake katika maeneo yote duniani.

Marji' huyu wa taqlid aliongeza kuwa: Popote duniani unaposafiri, utaona watoto wanaonesha aina fulani ya mapenzi ya kimaumbile kwa wazazi wao, na jambo hili linashuhudia kuwa mapenzi hayo ni ya kifitra; maana yake ni kwamba katika asili na umbile la kila binadamu, kuna hulka ya kuonesha upendo kwa baba na mama na kuwathamini.

Mtukufu huyo, huku akirejea kwenye asili ya mapenzi haya, alibainisha kwamba: Kipengele cha kifitra cha jambo hili, kwanza kabisa kinarejea kwenye uumbwaji wa mwanadamu, na sababu yake ni kulelewa kwa watoto kwa miaka mingi katika mikono ya wazazi wao. Watoto huishi kwa muda mrefu—miaka 10 au 20—pamoja na baba na mama zao, na hali hii husababisha mapenzi ya wazazi kuingia ndani ya nafsi ya binadamu kwa namna ya kifitra na yenye mizizi imara.

Hadhrat Ayatollah Subhani aliendelea kwa kurejea aya za Qur’ani Tukufu na kusisitiza uhakika na ulazima wa hukumu ya kuwafanyia wema wazazi, akasema Katika aya tukufu:

“وَ قَضىٰ رَبُّكَ أَلّا تَعْبُدُوا إِلّا إِيّاهُ وَ بِالْوالِدَيْنِ إِحْسانًا”,

neno “qadha” limetumika, tamko hilo katika Qur’ani Tukufu popote linapotumika humaanisha hukumu iliyo thabiti na isiyobadilika. Katika aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka misingi miwili mikuu: kwanza, kumuabudu na kumtumikia Mungu kwa ikhlasi, na pili, kuwafanyia wema wazazi.

Akieleza nafasi ya juu ya wazazi katika Uislamu, alisema: Mtu anaewafanyia wema baba na mama yake, yupo katika daraja ya pili baada ya kumuabudu Mwenyezi Mungu. Umuhimu wa jambo hili ni mkubwa kiasi kwamba hata katika aya zinazofuata, wale wanaotaka kuwaudhi wazazi wao wameonywa vikali.

Ayatollah Subhani aliendelea kwa kuashiria hali ngumu ya uzee wa wazazi na kubainisha: Wakati baba na mama wanapofikia umri wa uzee na kupoteza nguvu zao, wanahitaji uangalizi na heshima zaidi. Kama Qur’ani Tukufu inavyosema:


“إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا”.

Katika hatua hii nyeti, mwanadamu anawajibika kuwatendea wema wazazi wake kwa heshima kamili katika hali zote, na ajiepushe kabisa na kuonesha kutoridhika au hata neno “uffi” ambalo ndilo aina ndogo kabisa ya kukosa heshima.

Katika kuendelea kufafanua masuala ya maadili na malezi, huku akirejea aya za Suratul-Israa, alielezea vipengele mbalimbali vya kuwafanyia wema wazazi na kusema: Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya za Qur’ani Tukufu, anapozungumzia uzee na udhaifu wa wazazi, anawaambia watoto kwamba hawana haki hata ya kutamka neno dogo kabisa la kukosa heshima dhidi ya wazazi wao.

Marji' huyu wa taqlid alisema: Neno “uffi” katika aya tukufu ndilo alama ndogo kabisa ya kukosa heshima. Msithubutu kuinua sauti zenu mbele ya wazazi au kuwaita kwa njia isiyo ya heshima; bali semeni nao kwa adabu kamili na kwa sauti ya chini kabisa iliyojaa mapenzi.

Katika kuendelea, akieleza ujumuishi wa hukumu za Uislamu, alisisitiza: Hukumu ya kuwafanyia wema wazazi haiwahusu wazazi Waislamu pekee, bali inawahusu wanadamu wote, wawe ni waumini wa Mungu Mmoja au wasio waumini.

Mtukufu huyo aliendelea kusema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.ww) aliulizwa: Je, baada ya kufariki wazazi pia mtu anaweza kuwafanyia wema? Mtume akajibu: “Ndiyo; kwa kuwaombea dua na istighfari, kutimiza ahadi zao, kulipa madeni yao, na kuwaheshimu marafiki zao.”

Kwa upande mwengine Marji' huyu wa taqlid, huku akielezea tofauti kati ya mtindo wa maisha ya Kiislamu na mitazamo ya Magharibi, alibainisha kuwa: Katika nchi za Magharibi, mara nyingi watoto wanapokua huwapeleka wazazi wao katika nyumba za wazee, lakini katika utamaduni wa Kiislamu, Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani Tukufu anasema: “وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا” na anatuamrisha ikiwa wazazi wako hai, tuwatendee wema, na ikiwa hawapo hai, tuwaombee msamaha na kheri.

Ayatollah Subhani alisisitiza: Tunapaswa kuuthamini Uislamu na kuwaheshimu wazazi, na tusiyatenganishe maisha yetu na dini. Zamani, nyumba zilikuwa kubwa; mtoto wa kiume alipokua, aliishi katika moja ya vyumba kwenye nyumba ile ili kuwa karibu zaidi na baba na mama na wasihisi upweke. Lakini leo, kwa bahati mbaya, kwa kuwa kioa mmoja anaishi kwake uhusiano huu wa kihisia umedhoofika.

Mwisho wa mazungumzo yake, huku akitoa wito wa kutekeleza hadithi za Ahlul-Bayt (a.s) kuhusu haki za wazazi, aliongeza kuwa: Imam Zaynul-Abidin (a.s) katika dua zake anamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kulinda haki za baba na mama zetu:


“وَاخْصُصِ اللَّهُمَّ وَالِدَيَّ بِالْكَرَامَةِ لَدَيْكَ وَالصَّلَاةِ مِنْكَ يَا أَرْحَمَ الرَّاحِمِينَ”.

Tunapaswa kujitahidi kutekeleza kwa uadilifu haki zote zilizo juu ya mabega yetu. Maadili ya Uislamu na heshima ya kibinadamu vipo juu kiasi cha kwamba hata kwa wazazi makafiri, imeamrishwa kuwafanyia wema na kuwaonesha upendo.

Uislamu umetoa tiba ya matatizo ya kijamii

Ayatollah Subhani, huku akilinganisha zama za ujahilia kabla ya Uislamu na mafundisho ya Qur’ani, alibainisha: Katika kipindi cha ujahilia, kulikuwepo na desturi kali na za ajabu kuwaelekea wazazi, lakini Uislamu kupitia maagizo haya ya Mwenyezi Mungu ulitoa tiba yenye kuponya matatizo ya kijamii na kifamilia.

Mtukufu huyo, huku akirejea mfano mzuri uliotolewa na Qur’ani Tukufu, alisema: Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya “وَ اخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ” amemfananisha muumini na ndege anayeteremsha mabawa yake kwa unyenyekevu na rehema. Aliendelea kusema: Mtazameni ndege; ikiwa kuku ana vifaranga wanne au watano, hutandaza mabawa ylzake ili kuwafunika vifaranga wote na kuwalinda. Qur’ani inasema: Mwanadamu pia anapaswa kufungua mlango wa rehema kwa wazazi wake na kuwafunika chini ya mabawa za huruma yake.

Kutenda wema kwa wazazi hakuishii katika kipindi cha uhai wao tu

Ayatollah Subhani, akibainisha kuwa hakuna maneno yenye ujumuishi na uzuri kama haya katika fasihi ya wanadamu, aliongeza kuwa: Maelezo haya ya kina na yenye maana pana ni mfano kamili wa namna wanadamu wanavyopaswa kuishi na kuamiliana.

Mtukufu huyo aliendelea kwa kugusia jambo jingine muhimu na kusema: Kuwafanyia wema na ihsani wazazi hakuishii katika kipindi cha uhai wao pekee, wala hakutoshelezi. Manabii wakubwa wa Mwenyezi Mungu, akiwemo Nabii Nuh na Nabii Ibrahim (a.s), hata baada ya kufariki kwa wazazi wao waliendelea kuwaombea dua. Dua ya Nabii Nuh (a.s) kwa wazazi wake ilikuwa: “رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَنْ دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ”, na dua ya Nabii Ibrahim kwa wazazi wake ilikuwa: “رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ”. Hata walipokuwa watu wazima, hawakukatisha uhusiano wa kihisia na wazazi wao, bali waliendelea kuwaombea dua.

Aliendelea kwa kurejea dua ya Nabii Isa (a.s) iliyotajwa katika Qur’ani Tukufu, akasema: Nabii Isa (a.s) anasema: “وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا”. Vilevile Mwenyezi Mungu katika aya ya 14 ya Suratul-Maryam, anazitaja sifa mbalimbali za Nabii Yahya (a.s): “وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُنْ جَبَّارًا عَصِيًّا”. Maombi haya yanatolewa hali ya kuwa Manabii, hata baada ya kupita miaka mingi, hawakuwa wamewasahau mama zao. Hii inaonesha kuwa wajibu wa mtoto kwa wazazi wake unaendelea hata baada ya kifo chao kupitia dua na kuwaombea msamaha.

Mfumo wa maisha ya Kiislamu ni dhamana ya kuimarisha familia

Ayatollah Subhani, huku akirejea nafasi ya msingi ya wazazi katika dini tukufu ya Uislamu, alielezea nukta muhimu na simulizi za kielimu zinazo tokana na mwenendo wa Ma‘sumin (a.s), na akarejea riwaya kutoka kwa Imam Ja‘far Sadiq (a.s), akasema: Kijana mmoja alimwambia Imam Ja‘far Sadiq (a.s): Mimi nimekuwa Mshia, lakini mama yangu ni Mnaswara, nifanye nini kumhusu mama yangu? Imam akamuuliza: Je, mama yako anakula nyama ya nguruwe na kunywa pombe? Kijana akasema: Hapana. Imam akasema: Kadiri uwezavyo, mpende mama yako na mheshimu; wakati wa kula, kula pamoja naye katika chombo kimoja.
Kijana huyo aliporudi Madina, mama yake alimwambia: Mwanangu, umebadilika; sababu ya mabadiliko haya ni nini na nani amekuathiri? Kijana akasema: Imam Ja‘far Sadiq (a.s) ndiye aliyenifanya nibadilike na nikutendee wema. Wakati huo huo, mama huyo ambaye alikuwa Mnaswara kwa takribani miaka 90, alisilimu.

Aliongeza kuwa: Msimulizi anasema: Mtu mmoja alikuwa amembeba mama yake mabegani na kumzungusha katika tawafu, ndipo akamwona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w). Akauliza: Je, nimelipa haki ya mama yangu? Mtume Mtukufu (s.a.w) akasema: “Hata haki ya kilio kimoja tu ya wakati wa kujifungua bado hujalipa.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha