Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, wanazuoni wa Kishia wa Pakistan walitoa msimamo huo katika mkutano na waandishi wa habari, huku wakilaani kwa nguvu kauli za kudhalilisha na vitisho zilizo tolewa na Donald Trump, Rais wa Marekani, dhidi ya Ayatullah al-‘Udhmaa Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Wahadhiri katika mkutano huo walitahadharisha kwamba, endapo kitafanyika kitendo chochote cha kumdhuru Ayatullah al-‘Udhmaa Sayyid Ali Husayni Khamenei, kitendo hichokitakuwa na athari kali na pana katika eneo lote, na Marekani itabeba dhamana kamili ya madhara hayo.
Wanazuoni hao waliendelea kwa kukataa waziwazi uamuzi wa serikali ya Pakistan wa kujiunga na kile kinachoitwa “Kamati ya Amani ya Ghaza” ya Donald Trump, huku wakieleza kuwa uamuzi huo ni haramu, kinyume na Katiba, unapingana na maslahi ya taifa na uko kinyume kabisa na matakwa ya umma.
Katika mkutano huo ilielezwa kuwa kile kinachoitwa “Kamati ya Amani ya Ghaza” si mradi wa kuleta amani duninia, bali ni mpango uliopangwa kwa makusudi kulinda maslahi ya Marekani na Israel, kwa lengo la kuzidhoofisha taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na kudhibiti siasa za dunia kwa kutumia nguvu.
Wahadhiri waliongeza kuwa, chini ya kivuli cha “Kamati ya Amani ya Ghaza”, kwa hakika usalama wa Israel unalindwa huku haki halali za wananchi wa Palestina zikikanyagwa.
Wanazuoni hao walisisitiza pia kuwa, Israel hata baada ya kupita miaka miwili tangu tukio la “Tufani ya Al-Aqsa”, imeshindwa kuishinda Hamas, na sasa njama zinaendelea ili kuyanyang'anya silaha makundi ya muqawama kupitia majeshi ya nchi za Kiislamu. Hatua hii ni jaribio la kuifuta kabisa dhana ya kuwepo dola huru ya Palestina.
Hujjatul-Islam Sayyid Nazir Abbas Taqvi, mjumbe mwandamizi wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan, alisema katika hotuba yake kwamba, wanasimama pamoja na Hamas na wananchi wa Palestina, na kwamba damu ya zaidi ya mashahidi 60,000 wa Kipalestina haiwezi kwa vyovyote vile kufanyiwa biashara. Aliongeza kuwa; kutumia majeshi ya Kiislamu dhidi ya Hamas au kundi lolote la upinzani ni njama ya wazi ya kuleta mgawanyiko ndani ya Umma wa Kiislamu.
Washiriki wa mkutano huo waliwataja wahusika wa kile kinachoitwa “Kamati ya Amani ya Ghaza” kuwa wamechafuliwa na damu ya Waislamu, wakisema kuwa kuzungumzia amani chini ya uongozi wa watu wa aina hiyo ni hadaa tupu. Aidha, walieleza kuwa ombi la Trump la kulipwa mamilioni ya dola kama ada ya uanachama katika kamati hiyo ni mfano wa wazi wa uporaji na sura mbaya zaidi ya siasa za kibeberu za kisasa.
Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan waliwasilisha matakwa yafuatayo kwa serikali ya Pakistan:
1. Kutangazwa mara moja kusitishwa kwa uhusiano wowote na kile kinachoitwa “Kamati ya Amani ya Trump”.
2. Kulindwa na kudumishwa kwa sera ya nje ya Pakistan iliyo huru na inayojitegemea.
3. Rasilimali, majeshi na mitaji ya Pakistan isitumiwe katika miradi inayoiunga mkono Israel.
4. Msaada wa kimaadili, kisiasa na kidiplomasia kwa wananchi wa Palestina uwe sera rasmi ya serikali.
5. Balozi wa Marekani aitwe rasmi kwa ajili ya kuelezea upinzani mkali dhidi ya vitisho vilivyotolewa kwa Ayatullah al-‘Udhmaa Sayyid Ali Husayni Khamenei.
Mwisho wa mkutano na waandishi wa habari, wanazuoni wa Kishia wa Pakistan waliwaomba wananchi, uongozi wa kisiasa na taasisi za serikali kuutanguliza msimamo wa msingi wa mwanzilishi wa Pakistan, hisia za umma na maslahi ya pamoja ya Umma wa Kiislamu juu ya shinikizo lolote la kimataifa.
Maoni yako