Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kongamano la kila mwaka la “Kumbukumbu ya Mashahidi wa Uislamu” lilifanyika katika jimbo la Sindh, Pakistan. Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan, alilihutubia kongamano hilo kwa njia ya simu na kusema:
Manabii na Mitume wote (amani iwe juu yao) walitumwa kwa ajili ya kusimamisha uadilifu na haki, na hilo pia ni miongoni mwa malengo ya jumuiya yetu. Daima tumekuwa tukidai kuanzishwa kwa mfumo na haki za uadilifu kwenye nchi hii. Tunataka kuona haki, usawa na ustahiki vikitekelezwa, na kwa ajili ya kuyafikia hayo ni lazima kuboresha taasisi, kuongeza juhudi na kupaza sauti kwa nguvu zaidi. Katika mazingira haya, ili kufikia malengo, ni muhimu kuziimarisha taasisi zetu, kuzidisha mawasiliano, mshikamano na uratibu miongoni mwetu, na kuepuka kuchochea migogoro.
Aliendelea kusema kuwa, katika zama hizi kuna mapungufu makubwa ya mifumo ya haki, na ni juu yetu kupambana kwa ajili ya kuanzishwa kwa mfumo wa haki wa kimataifa. Qur’ani Tukufu inatuongoza kwenye mapambano haya, na hili pia ndilo jukumu la manabii na warithi wao. Ni wazi kwamba kwa ajili ya kufikia lengo hili, kuinua sauti na kusimama kidete ni jambo la lazima.
Msomi huyo mashuhuri wa Pakistan aliongeza kuwa, hata katika ngazi ya kimataifa, ni wajibu wetu kuchukua nafasi na kushiriki katika kukabiliana na changamoto na hali zilizopo. Tunasimamia na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mambo ya kimataifa. Lengo na juhudi za ubeberu ni kuiimarisha Israel kwa kutumia nguvu na uonevu, na kuiangamiza Palestina; hata hivyo hali hii haikubaliki kabisa.
Aliendelea kusema kuwa; hatua na jitihada zetu zinaendelea kulingana na mahitaji ya wakati. Ni lazima tuwe na umakini zaidi, tuimarishe uratibu na mshikamano wetu, kwa sababu mshikamano na umoja ni nguvu kubwa sana, na pale tutakapochukua hatua na kufanya juhudi, bila shaka tutapata matokeo chanya.
Mwisho wa hotuba yake, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan alimwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aujaalie mkusanyiko huu uwe na athari chanya na matunda mema, azibariki juhudi hizo, na azidishe mshikamano na uratibu miongoni mwao.
Maoni yako