Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan Taqvi, Rais wa Jumuiya ya N'adhimiya katika mji wa Lucknow, India, katika hotuba yake huku akitangaza uungaji mkono wa dhati kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mtukufu Ayatollah Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), alisisitiza kuwa; yeye ndie mbeba bendera wa kweli wa Uislamu, mtetezi wa haki, na ngome thabiti kwa Umma wa Kiislamu dhidi ya njama na mashinikizo ya maadui.
Aliendelea kwa kuashiria nafasi ya kipekee ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akisema: uongozi wa Mtukufu Ayatollah Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde) ni taswira iliyo wazi ya busara ya kidini, ikhlasi, ujasiri na kusimama imara katika njia ya haki. Kwa uthabiti na bila hofu, amebeba jukumu la kuuongoza Umma wa Kiislamu.
Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan, akiendelea na hotuba yake kwa kusoma Aya kutoka katika Sura tukufu ya An-Nasr, alisema: Qur’ani Tukufu daima hutoa bishara ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa watetezi wa haki, na huahidi kushindwa na fedheha kwa wafuasi wa batili. Historia inashuhudia kuwa sunna hii ya Mwenyezi Mungu imeendelea kutekelezwa katika zama zote. Njama na uadui dhidi ya kambi ya haki si jambo jipya, bali ni jambo lililodumu kwa karne nyingi.
Madhehebu ya Ashura – kipimo cha kuitofautisha haki na batili
Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Kihindi, akisisitiza nafasi ya Madhehebu ya Ashura katika kuuelimisha Umma wa Kiislamu, aliongeza kuwa: kumuomboleza Imam Husayn (a.s.) daima kumeekuwa kipimo cha kutambua haki na batili, na watu huru duniani wamechagua njia sahihi kwa mwanga wa madhehebu haya. Imam Khomeini (rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) pia, kwa kutegemea fikra za Husseini, aliwaamsha wananchi wa Iran na kwa kuuangusha utawala wa kifalme, aliurejesha Uislamu katika nafasi yake stahiki.
Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan aliendelea kwa kurejelea vikao vyake binafsi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akabainisha: katika kikao kilichochukua muda mjini New Delhi na Mtukufu Ayatollah Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde), nilimkuta akiwa na moyo safi, maneno ya wazi, roho ya ujasiri, na kujali kwa kina maslahi ya Uislamu. Katika mikutano iliyofuata pia—iwe ni katika makongamano ya kimataifa au hafla nyingine—ikhlasi hiyo hiyo, mapenzi na roho ya kidini yalionekana wazi ndani yake.
Alisisitiza kuwa: tunaunga mkono kikamilifu na bila masharti yoyote hatua zote zinazochukuliwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika njia ya kuinua na kuitukuza dini ya Uislamu. Wanazuoni kutoka India hadi Iran na Iraq, wote wamesimama katika safu moja; kwa sababu lengo letu la pamoja ni kuitetea haki na kupambana na batili.
Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan katika hitimisho lake alisisitiza kuwa: wale wanaompinga Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa hakika wamesimama dhidi ya haki. Historia imeonesha kwamba wapinzani wa haki daima wamekumbwa na udhalili na kushindwa, na hatima hiyo haitabadilika hata siku zijazo.
Kwa kufanya upya ahadi ya utii kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: Tumekuwepo, tupo, na Insha’Allah daima tutabaki pamoja na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Maoni yako