Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mamia ya waumini walihudhuria majlisi hiyo ya kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (as), ambapo walipata fursa ya kusikiliza darsa na mawaidha yaliyolenga kuhuisha ujumbe wa Karbala na kuimarisha uhusiano wao na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as).
Akitoa darsa katika Majlisi hiyo ya maadhimisho ya Tukio la Karbala, Sheikh Hemed Jalala alizungumzia kwa kina suala la Imam Mahdi (as) na nafasi yake muhimu katika mafundisho ya Kiislamu, alieleza kwamba; Uislamu umeendelea kusimama imara na kuhifadhiwa kwa vizazi mbalimbali kupitia mafundisho sahihi ya Mtume Muhammad (saww) pamoja na Ahlul-Bayt (as), ambao wamekuwa nguzo ya uongofu na mwangaza kwa Umma wa Kiislamu.
Sheikh Jalala alisisitiza kuwa; waumini wanapaswa kuimarisha maarifa yao kuhusu Maimamu wa Ahlul-Bayt (as), hususan Imam Mahdi (as), na kuendelea kushikamana na mafunzo yao ili kujenga jamii yenye msingi wa uchamungu, haki na uadilifu.
Aidha, aliwahimiza waumini kujifunza, kutafakari na kuishi kwa mujibu wa mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), akibainisha kuwa tukio la Karbala si tukio la kihistoria pekee, bali ni shule ya milele inayofundisha thamani ya kusimamia haki, kupambana na dhulma na kujitolea kwa ajili ya kuilinda dini na maadili ya Kiislamu.
Majlisi hiyo ilihitimishwa kwa dua na maombolezo ya kumbukumbu ya Imam Hussein (as), huku waumini wakionesha hisia zao za huzuni na mshikamano na ujumbe wa Karbala ambao umeendelea kuhamasisha mamilioni ya watu duniani kote katika harakati za kutetea haki na kupinga batili.
Majlisi za Muharram zinaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, zikitoa fursa kwa waumini kujifunza kwa kina historia ya Karbala na kuendeleza urithi wa kiroho na kimapinduzi ulioachwa na Imam Hussein (as) kwa Umma wa Kiislamu.




Maoni yako