Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Taasisi ya Bilal Muslim nchini Kenya imeandaa na kuendeleza majlisi za maombolezo ya Imam Hussein (as) tarehe 22 Juni 2026, katika mwendelezo wa shughuli za mwezi wa Muharram zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Majlisi hizo zimekuwa zikiwakutanisha waumini kutoka sehemu tofauti za Kenya, ambapo wanapata fursa ya kujifunza kwa undani historia ya tukio la Karbala, sababu za mapambano ya Imam Hussein (as), pamoja na mafunzo makubwa yanayotokana na kujitolea kwake kwa ajili ya kuilinda dini ya Kiislamu na kusimamisha haki dhidi ya dhulma.
Miongoni mwa wahadhiri waliopata nafasi ya kuzungumza katika majlisi hiyo ni Sheikh Juma Shughuli, ambaye aliwasilisha mada maalumu olioangazia kwa kina matukio ya Karbala na mazingira yaliyopelekea kuuawa kishahidi Imam Hussein (as) pamoja na masahaba na watu wa familia yake.
Katika hotuba yake, Sheikh Juma Shughuli alieleza kwa ufafanuzi dhulma na ukandamizaji uliofanywa na utawala wa Bani Umayyah dhidi ya Ahlul-Bayt (as), huku akisisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka katika msimamo wa Imam Hussein (as) wa kusimama imara mbele ya batili na kutetea haki bila kujali gharama.
Aidha, mhadhara huo uliibua hisia kubwa miongoni mwa washiriki, ambao walionekana kuguswa na simulizi za mateso na dhulma zilizowakumba familia ya Mtume (saww) katika ardhi ya Karbala, waumini walihimizwa kuendeleza maadili ya kujitolea, subira na kusimama upande wa haki kama alivyofanya Imam Hussein (as).
Majlisi za maombolezo zinaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini Kenya, huku zikitoa fursa kwa waumini kuimarisha uelewa wao wa historia ya Karbala na kuhuisha ujumbe wa milele wa Imam Hussein (as), ambao unaendelea kuwa taa ya mwongozo kwa Waislamu na wapenda haki duniani kote.


Maoni yako