Jumatatu 8 Juni 2026 - 08:49
Ufafanuzi wa Hadithi ya Akhlaq | Subira katika mitihani, utiifu na kuacha maasi kwa mujibu wa simulizi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi

Hawza/ Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, akirejelea hadithi: «فَإِنِ اسْتَطَعْتَ أَنْ تَعْمَلَ بِالصَّبْرِ مَعَ الْیَقِینِ فَافْعَل», alifafanua maana ya subira katika nyanja tatu: mitihani, utiifu na kuacha maasi, na akasisitiza nafasi ya yakini katika kurahisisha subira.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Shahidi Imam Khamenei (ra) katika mwanzo wa vipindi vya masomo yake ya Dars Kharij ya fiqhi, alikuwa akitoa ufafanuzi wa hadithi za kimaadili. “Subira” ndiyo mada ya hadithi ya kimaadili kutoka kwa Mtume mtukufu wa Uislamu, Muhammad Mustafa (s.a.w.w), ambayo video na maandishi yake yamechapishwa kama ifuatavyo:

Maandishi ya maelezo ya Kiongozi Shahidi ambayo yanaonekana katika video hii ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu.

Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), katika mwendelezo wa hadithi iliyopita:

«فَإِنِ اسْتَطَعْتَ أَنْ تَعْمَلَ بِالصَّبْرِ مَعَ الْیَقِینِ فَافْعَل»

Wakati mwingine mtu huvumilia katika tukio fulani, anafanya subira; aidha anafanya subira juu ya balaa, au anafanya subira katika utiifu, au anafanya subira dhidi ya maasi, Hizi zote ni aina za subira.

Ikiwa mnaweza kufanya subira pamoja na yakini, basi fanyeni hivyo.

Yaani, tuchukulie kwamba balaa au tukio fulani linamshukia mtu; naye analivumilia na kufanya subira huku akiwa na yakini kwamba tukio hilo limetoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba subira yake ni kwa manufaa yake na itakuwa yenye kumfaa.

Au mtu anafanya subira katika utiifu; yaani tendo fulani la kumtii Mwenyezi Mungu au tendo la kumkaribia Yeye linaweza kuwa gumu kulitekeleza, lakini mtu anafanya subira, anavumilia ugumu huo na analitekeleza.

Na anajua kwamba jambo hilo lina thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na hali ni hiyo hiyo katika suala la maasi, ambapo subira huambatana na yakini, mtu anasimama imara akiwa na yakini juu ya matokeo yake.

Ikiwa unaweza kufanya hivyo, basi ni bora zaidi; lifanye jambo hilo.

Subira ya aina hii si ngumu sana, kwa sababu mtu anapojua matokeo ya subira, basi kwa kawaida subira inakuwa rahisi kwake na inakuwa tamu.

Lakini:


«فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ»

Ikiwa huwezi kuwa na yakini pamoja na subira, basi fanya subira.

Hata kama huna yakini kuhusu matokeo yake, kuhusu manufaa na faida utakayoipata kutokana na subira hiyo, bado fanya subira.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: fanyeni subira. Ameamrisha kufanya subira.

«فَإِنَّ فِي الصَّبْرِ عَلَى مَا تَكْرَهُ خَيْرًا كَثِيرًا»

Subira juu ya jambo ambalo hulipendi, ambalo ni gumu na lisilopendeza, lina kheri nyingi kwa mwanadamu.

Lina manufaa makubwa na mengi kwa mwanadamu.

Asili ya subira yenyewe; subira juu ya maradhi, subira juu ya ufukara, subira juu ya mambo yanayotokea katika maisha, matatizo yanayotokea na balaa zinazotokea.

Na ujue pia kwamba:

«وَاعْلَمْ أَنَّ الصَّبْرَ مَعَ النَّصْرِ»

Yaani ujue kwamba subira daima huambatana na nusra.

Mahali ambapo kuna mapambano, ushindani au kukabiliana na adui, ikiwa mtavumilia — na maana ya subira hapa ni kuvumilia matatizo na kusimama imara — basi kwa hakika ushindi utaandamana nayo.

Na:

«وَأَنَّ الْفَرَجَ مَعَ الْكَرْبِ وَأَنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا، إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا»

Na ujue kwamba faraja huja pamoja na dhiki, na pamoja na ugumu kuna wepesi; hakika pamoja na ugumu kuna wepesi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha