Jumamosi 25 Julai 2026 - 21:43
Hakuna hatua yoyote ya adui ya kuondoka; Serikali ya Lebanon inatumia maonesho ya kisiasa kutengeneza ushindi wa kufikirika

Hawza/ Hassan Fadlallah amesisitiza kuwa; adui wa Kizayuni hajaondoka hata kutoka kipande kimoja cha ardhi inayokaliwa kwa mabavu kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hassan Fadlallah, mjumbe wa Kambi ya "Uaminifu kwa Muqawama" katika Bunge la Lebanon, wakati wa hafla ya kumbukumbu iliyoandaliwa na Hizbullah kwa ajili ya Shahidi Sheikh Muhammad Baqir Ali Karaki katika Jengo la Imam Mujtaba (as) eneo la Saint Therese, alisisitiza kuwa; hakuna hata hatua moja ya kuondoka iliyochukuliwa na adui wa Kizayuni kutoka hata kipande kimoja cha ardhi inayokaliwa kwa mabavu kusini mwa Lebanon.

Alifafanua kwamba; kilichotokea ni kuimarishwa tu kwa uwepo wa Jeshi la Lebanon katika vijiji na miji iliyokombolewa ambayo adui alishindwa kuikalia kwa mabavu kutokana na damu ya mashahidi na kujitolea wapiganaji wa Muqawama. Alisema jeshi lina haki ya kuwepo miongoni mwa wananchi wake na kuimarisha uwepo wake, na hakuna anayepaswa kulizuia. Hata hivyo, pale jeshi lilipotaka kusonga mbele kidogo nje ya mipaka ya maeneo yaliyokombolewa katika eneo la Zawtar al-Gharbiyah, adui alilifyatulia risasi, na kwa ujasiri mkubwa, huku kukiwa na ukimya wa Serikali ya Lebanon, akatangaza kuwa Jeshi la Lebanon limesonga mbele kwa mita 100; ilhali ukweli ni kwamba Jeshi la Lebanon lilikuwa likisonga ndani ya ardhi yake, wakati jeshi la adui ndilo jeshi linalokalia ardhi hiyo kwa mabavu.

Makubaliano yaliyofikiwa hayajamsababisha adui kuondoka katika eneo lolote analolikalia

Aliongeza kuwa; katika yaliyotokea Zawtar al-Gharbiyah, adui wa Kizayuni hakuondoka. Serikali haina haja ya maonesho hayo ili kuonesha kana kwamba kuna mafanikio yaliyopatikana, ilhali huo ni ushindi wa kufikirika, alisema; wanaunga mkono kuondoka adui kutoka eneo lote analolikalia kwa mabavu, na jambo hilo halisababishi wasiwasi wowote kwao. Lakini akahoji kwa nini serikali inataka kutumia mbinu hiyo ya kuchekesha, ambayo ni sawa na kucheza juu ya damu za mashahidi na kudharau kujitolea kwao. Kwa mujibu wake, hatua hizo si chochote isipokuwa maonesho ya vyombo vya habari kwa ajili ya kujijengea mtaji wa kisiasa, bila kubadili chochote katika hali halisi.

Fadhlallah aliendelea kusema kuwa, ili watu wasidanganywe, ni lazima isemwe wazi kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mfumo uliopo hayajamsababisha adui kuondoka katika eneo lolote analolikalia kwa mabavu, ili watu wasidhani kuwa kuna mafanikio yoyote yaliyopatikana kwa nchi. Alisema kama kungekuwa na mafanikio yoyote, wako tayari kuyathibitisha. Hata hivyo, kwa maoni yake, serikali hii inafanya kazi kwa msingi wa kuhalalisha uwepo wa utawala wa Kizayuni na kuendelea kwa ukaliaji wake, huku ikionesha kuondoka kwa Israel kuwa kunategemea suala la kunyang'anywa silaha Muqawama.

Muqawama wetu ni dharura na hitaji la kitaifa

Alibainisha kuwa; wale wanaotoa ahadi kwa Marekani na kuwasilisha mipango ya namna ya kunyang'anywa silaha Muqawama, kwa hakika wanaiuzia Serikali ya Marekani ndoto zisizo na uhalisia. Alisema watatumia maisha yao ya kisiasa wakiwa madarakani huku wakihesabu siku na miezi bila kufanikisha hata lengo moja la kudhoofisha mojawapo ya nguzo za nguvu zao. Adui alijaribu kwa nguvu za chuma na moto kuunyang'anya Muqawama silaha zake lakini alishindwa; hivyo akauliza, je, watu wachache walioko serikalini wanaweza kufanya jambo ambalo adui alishindwa kulifanya? Akahoji watu hao wanaishi katika dunia gani au sayari gani hadi wanakataa hali halisi. Alisisitiza kuwa; ahadi hizo hazina thamani yoyote kwao, na kwamba Muqawama ni dharura na hitaji la kitaifa, na wataendelea kuushikilia hadi ardhi yao ikombolewe, nchi yao ilindwe na damu za mashahidi wao zihifadhiwe.

Tunakabiliana na utawala wa mabavu unaokiuka usitishaji wa mapigano

Mjumbe huyo wa Kambi ya Muqawama alisema kuwa; msingi wa msimamo wao ni kuondoka adui katika ardhi yao, kurejea wakimbizi, ujenzi upya na kuachiwa huru wafungwa. Alisema iwapo serikali itafanikiwa hata kupata fanikio moja katika mambo hayo, wao watayatambua kuwa ni mafanikio. Lakini hadi sasa, kwa mujibu wake, serikali haijapata mafanikio yoyote ya kweli. Aliongeza kuwa hali ya sasa ni kwamba wanakabiliana na utawala wa mabavu unaokiuka makubaliano ya usitishaji wa mapigano; wanashuhudia uthabiti wa kishujaa wa wapiganaji walioko mstari wa mbele, pamoja na juhudi za adui za kukwepa wajibu wake chini ya makubaliano ya usitishaji wa mapigano ya kikanda na kutumia vibaya mapendeleo ambayo serikali imeipa kupitia makubaliano yake.

Serikali ya Lebanon inaisukuma nchi kuelekea mivutano na migongano ya ndani

Fadhlallah anaamini kuwa; Serikali ya Lebanon, kupitia hatua zake za ndani, inaielekeza nchi kuelekea kwenye mivutano na migongano ya ndani, na inaleta shinikizo katika pande mbalimbali ili kuzalisha makabiliano ya ndani. Alisema; Hizbullah inajitahidi kuepuka migongano ya ndani na inasisitiza kulinda nchi pamoja na amani ya kijamii. Amesema wamekuwa wakiionya serikali mara kwa mara isiwasukume wananchi wake kuelekea katika makabiliano, kwa sababu hakuna serikali yoyote nchini Lebanon ambayo imewahi kushinda kwa kuwatumbukiza wananchi wake katika migogoro ya ndani.

Aidha, alieleza kuwa; serikali imechukua hatua mbalimbali za kimahakama, kiusalama na kutoa kauli maalumu. Kwa upande wao, alisema wataendelea kuwa na subira kadiri watakavyoweza ili kulinda Muqawama na kujitolea kwa vijana wao, pamoja na kuzingatia maslahi ya taifa. Hivyo, kuepuka kwao migongano ya ndani hakutokani na udhaifu, kurudi nyuma wala ukosefu wa uungwaji mkono wa wananchi, bali kunatokana na kujali mustakabali wa nchi yao. Aliongeza kuwa; baadhi ya viongozi waliopo katika majumba yao ya utawala wanadhani jamii ya Muqawama imedhoofika na kwamba Iran nayo inazidi kudhoofika, lakini kwa maoni yake wanaishi katika ndoto na wamejenga misimamo yao juu ya mawazo yasiyo na msingi.

Tuna imani na msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mjumbe huyo wa Kambi ya Muqawama alihitimisha kwa kusema kuwa tegemeo kuu bado ni mwamvuli wa kikanda unaoendelea kujengeka katika eneo hili, hata pamoja na mashambulizi ya Marekani. Alisema, mwishowe, hata kama mashambulizi hayo yataendelea kwa muda mrefu, Marekani italazimika kurejea kwenye makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kifungu cha kwanza cha makubaliano hayo kitaihusu Lebanon.

Alisisitiza kuwa; wana imani na msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wanafahamu kuwa hakuna makubaliano yoyote ya kikanda au ya mwisho yatakayofikiwa bila ya adui wa Kizayuni kuondoka kikamilifu katika ardhi yao. Alisema huo ni msimamo thabiti na usiobadilika. Wakati huo huo, aliongeza kuwa kwanza wanamtegemea Mwenyezi Mungu, kisha wanategemea irada na uthabiti wa wananchi wao pamoja na uwepo endelevu wa Muqawama katika medani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha