Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maadhimisho hayo yaliyofanyika jana Jumamosi yalilenga kuwakumbusha Waislamu umuhimu wa kutafakari maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (saww), na kuyafanya kuwa dira katika kujenga maisha bora ya kiroho na kijamii. Hafla hiyo ilihudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali, ambao walijumuika kwa ajili ya kusherehekea tukio hilo tukufu na kujifunza ujumbe wa Mtume (saww).
Miongoni mwa viongozi na masheikh waliohudhuria alikuwa ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Abbas Ramadhani Abbas, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo. Katika hotuba yake, Sheikh Abbas alitoa wito kwa Umma wa Kiislamu kuacha mazoea yasiyojenga na kuchukua hatua za kufanya mabadiliko chanya katika mifumo ya maisha, fikra na mwenendo wa kijamii, huku akisisitiza kuwa mafundisho ya Mtume (saww) yanapaswa kuonekana katika vitendo na si katika maneno pekee.
Aidha, Sheikh Abbas alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, undugu na mshikamano miongoni mwa Waislamu, huku akitolea mfano funzo kubwa la kihistoria la kuunganisha udugu, ambapo Mtume Muhammad (saww) aliwaunganisha Muhajirina na Answar na kuwafanya kuwa ndugu. Alieleza kuwa tukio hilo ni mfano muhimu unaoonesha namna Uislamu unavyosisitiza kuondoa tofauti na kuijenga jamii inayosimama juu ya misingi ya upendo, kusaidiana na mshikamano.
Kwa upande wake, Bilal Muslim Mission of Tanzania imetoa shukrani za dhati kwa Mgeni Rasmi, viongozi wa dini, wageni mbalimbali pamoja na waumini wote walioshiriki katika maadhimisho hayo. Taasisi hiyo imesisitiza kuwa ujumbe wa maadhimisho hayo haupaswi kuishia katika ukumbi wa hafla, bali unapaswa kubebwa na kutekelezwa katika maisha ya kila siku, ili kuijenga jamii yenye upendo, umoja na mshikamano na kuweka msingi imara wa mustakabali bora wa Umma wa Kiislamu.


Maoni yako