Jumapili 20 Septemba 2026 - 14:21
Imam Askari (as) Aliwalea Mashia kwa Ajili ya Kuandaa Mazingira ya Kudhi­hiri Imam Mahdi (aj)

Hawza/ Mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi katika Mkoa wa Khorasan Razavi (Mash-had, Iran), huku akisisitiza kwamba harakati ya wananchi katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu inaandaa mazingira ya kudhihiri Imam wa Zama (aj), amesema kuwa: Imam Askari (as) aliwalea Mashia kwa ajili ya kipindi cha ghaiba na kuandaa mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (aj), na kwamba leo hii, muqawama na kusimama imara wananchi wa Iarn, dhidi ya adui ni uwanja mkubwa zaidi wa jihadi na sababu ya kumkatisha tamaa adui katika jaribio lake la kuvuruga hali ya ndani ya Iran.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Mashhad, Ayatullah Sayyid Ahmad Alam al-Huda, Mwakilishi wa Walii wa Faqihi katika Mkoa wa Khorasan Razavi, amesema hayo katika usiku wa 203 kwenye mkusanyiko wa wananchi wanamapinduzi na wenye uelewa wa eneo la Abdul-Muttalib mjini Mashhad Iran. Huku akiwashukuru wananchi kwa muqawama na ustahimilivu wao mkubwa baada ya kufanyika mikusanyiko hiyo kwa muda wa usiku 203, alisema: “Mikusanyiko hii ni uwanja imara na wenye nguvu wa wananchi dhidi ya adui, na ninatumai Mwenyezi Mungu Mtukufu azidishe uwezo wenu, nguvu zenu za kustahimili na kusimama imara, ili mikusanyiko na muqawama huu uendelee hadi kufikia hatua ya mwisho ya kuangamizwa adui.”

Akirejea kuwadia kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Hasan Askari (as), baba wa Imam wa Zama (aj), aliongeza: “Usiku wa leo ni usiku wa kuzaliwa kwa baraka Imam Askari (as), baba wa Imam wa Zama (aj), na sisi tuna mafungamano mbalimbali na mtoto huyu anayezaliwa usiku wa leo.

Uhusiano wa kwanza unatokana na upande wa Imam wa Nane (as), ambapo usiku wa leo tunda la moyo wa Imam Ridha (as), yaani Imam Askari (as), amezaliwa.

Uhusiano wa pili ni kwamba yeye ni baba wa Imam wa Zama (aj), ambaye ni Imam wetu, tegemeo letu, kimbilio letu na mwenye mamlaka juu ya maisha yetu ya leo katika nyanja zote za maisha.”

Ayatullah Alam al-Huda aliendelea kusema: “Usiku wa leo tunamheshimu baba wa Imam wetu aliye hai, aliyepo na mwenye mamlaka juu yetu, ambaye ni utangulizi wa kuzaliwa na kudhihiri uwepo mtakatifu wa Bwana wetu Imam wa Zama (aj), na ninawapongeza ndugu na dada wote kwa sikukuu hii yenye baraka.”

Jukumu la Imam Askari (as) katika Kuandaa Umma kwa Ajili ya Kipindi cha Ghaiba

Akieleza kwamba miongoni mwa Maimamu Watukufu (as), mhimili na sehemu kubwa ya jukumu la uongozi wa Imam Askari (as) ilikuwa ni kuuandaa Umma na Mashia kwa ajili ya ghaiba ya muda mrefu ya Imam wa Zama (aj), alisisitiza: “Lengo lilikuwa kwamba kwa kipindi cha karne na miaka mingi, watu waweze kuhifadhi maisha yao ya kidini na jamii yao ya kidini katika kipindi cha ghaiba ya Imam wao.”

Mwakilishi wa Walii wa Faqihi Khorasan Razavi alisema: “Kwa bahati nzuri, Mapinduzi yetu matukufu ya Kiislamu yalijitokeza duniani kwa lengo la kuweka na kuandaa mazingira ya kudhihiri Imam huyo. Kwa miaka 47, wananchi wetu wamesimama pamoja na Mapinduzi haya, na leo kiwango cha ulinzi na ustahimilivu wa wananchi dhidi ya Mapinduzi haya, ambayo yanaandaa mazingira ya kudhihiri Imam wa Zama (aj), kimekuwa kikubwa zaidi kuliko siku za mwanzo.”

Akirejea mazingira ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alibainisha: “Siku ambayo Mapinduzi haya yalishinda, watu hawakufikiri kwamba mapinduzi ya kijeshi yalikuwa yamefanyika, mfumo wa utawala wa kifalme wa kidhalimu ulikuwa umeangushwa, na kwamba mfumo wa kidini ungechukua nafasi ya mfumo huo wa kifalme wa kidhalimu; kwamba Shah alikuwa amefukuzwa nchini na kwamba wanazuoni wa dini, mara'jii na fatwa vingetawala nchini Iram, baadhi ya watu walitafsiri tukio hili kama mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika nchi hii pekee.”

Ayatullah Alam al-Huda aliongeza: “Wakati huo hakuna mtu aliyeelewa kwa kina ukubwa, asili, upanuzi na kuenea kwa Mapinduzi haya, isipokuwa Imam wetu shujaa, ambaye alikuwa mwanzilishi wa Mapinduzi, pamoja na wapendwa waliokuwa karibu na Imam, wao walijua uwanja ambao Mapinduzi yangeweza kupanuka na kuenea ulikuwa hadi wapi.”

Alisema: “Leo tunaona kwamba uwanja wa kuenea kwa Mapinduzi matukufu ya Kiislamu si nchi hii pekee, bali umehusisha nchi nyingi na kuunda jamii ya kimapinduzi.”

Kuenea Harakati ya Muqawama katika Jamii za Kiislamu

Mwakilishi wa Walii wa Faqihi Khorasan Razavi, huku akifafanua suala hilo, alisema: “Tuna ushahidi na mfano wa jambo hili. Muda mfupi uliopita, kwa jina la Mkataba wa Makka, nchi tatu za Saudi Arabia, Pakistan na Uturuki ziliingia katika mkataba wa kiulinzi na kijeshi; kwa namna ambayo ikiwa moja kati ya nchi hizi tatu itashambuliwa, nchi nyingine mbili, kwa mujibu wa mkataba huo, zitaenda kuisaidia na kuiunga mkono katika nyanja zote za kijeshi na kiulinzi.”

Aliendelea: “Saudi Arabia imekabiliwa na mashambulizi kutoka kwa Wayemeni mashujaa na mara kwa mara imeiomba Pakistan na Uturuki, kwa mujibu wa mkataba huo wa kiulinzi na kijeshi, kuingilia kati ili kuisaidia nchi hiyo katika kukabiliana na Yemen, lakini hawathubutu, kwa mujibu wa mkataba huo, kushiriki katika vita kati ya Saudi Arabia na Yemen.”

Ayatullah Alam al-Huda aliongeza: “Kwa nini hawathubutu na wanaogopa nini? Je, wanaiogopa Iran kwamba huenda wakakabiliwa na mashambulizi na uvamizi kutoka Iran? Si suala hilo; kwa sababu vita vyetu na Marekani kwa sasa ni suala letu la kwanza, na kwa nguvu zetu zote tunapaswa kupambana na chanzo hiki cha ufisadi duniani na tutaendelea na mapambano haya.”

Alisema: “Wao wanaogopa ndani ya nchi zao wenyewe. Leo, ndani ya Pakistan na Uturuki, muqawama umeingia na kuenea. Wananchi wa Pakistan, wengi wao, wanaunga mkono muqawama, na ikiwa serikali ya Pakistan itachukua hatua kinyume na muqawama katika kukabiliana na Yemen, ndani ya Pakistan kutatokea machafuko na wananchi hawa wanaounga mkono muqawama wataivuruga hali ya ndani ya nchi, hali hiyo hiyo ipo Uturuki, na leo katika nchi hiyo pia muqawama una wafuasi wengi.”

Mwakilishi wa Walii wa Faqihi Khorasan Razavi alisisitiza: “muqawama si jambo linalojitokeza tu katika uwanja wa vita; uwanja wa vita ndio dhihirisho lake, lakini msingi wa muqawama ni fikra, mawazo na imani. Kwa bahati nzuri, imani, fikra na mawazo ya muqawama yameingia ndani ya mataifa yote ya Kiislamu, na Mapinduzi yetu matukufu ya Kiislamu yameweza kusambaza msingi wa muqawama miongoni mwa mataifa yote ya Kiislamu.”

Alisema: “Leo, nchi yoyote, hata kama serikali yake ni ya Kimarekani au ya Magharibi na haina utegemezi wa Kiislamu na kidini, ikitaka kuchukua hatua yoyote kwa manufaa ya Marekani, harakati ya muqawama huibuka kutoka ndani ya nchi hiyo.”

Ayatullah Alam al-Huda aliendelea: “Leo, wakati vikosi vya Marekani vinapoingia Jordan na kutaka kukusanya na kuongeza vikosi vyao huko, ni wananchi wa Jordan wanaoripoti kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu anwani za maeneo ambayo vikosi vya Marekani vimejikusanya, na vikosi hivyo vinapigwa na kuangamizwa kwa makombora. Pia siku ambayo makombora yanarushwa kwa ajili ya kuwaangamiza wanajeshi wa Marekani, wananchi wa Jordan hupiga takbira na kusema ‘Allahu Akbar’.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha