Jumapili 20 Septemba 2026 - 00:59
Serikali ya Bahrain inapuuzia Sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu

Hawza/ Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain, katika taarifa yake amelaani maamuzi ya utawala wa Khalifa ambayo yanaweka vikwazo kwa baadhi ya sifa na taratibu za madhehebu ya Shia.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sheikh Issa Qa'sim, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain, ametoa taarifa yakulaani maamuzi ya utawala wa Khalifa ambayo yanaweka vikwazo kwa baadhi ya sifa na taratibu za madhehebu ya Shia, Matini ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:

Je, kuna Aya yoyote ya Qur’ani, au Hadithi Qudsi, au Hadithi yoyote sahihi, au hata Hadithi dhaifu miongoni mwa Hadithi za Mtume Mkuu (saww) au Ahlul-Bayt Maasumu (as), na je, kuna madhehebu yoyote miongoni mwa madhehebu ya Kiislamu, au mwanazuoni yeyote miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, anayeshikilia kwamba Uislamu umeweka kikomo maalumu ambapo hukumu za Sheria ya Kiislamu, iwe katika zama za mwanzo za Uislamu au siku zijazo, zitamalizika kabisa chini ya utawala wowote utakaoanzishwa, kwa aina yoyote ya serikali au utawala, au kupitia mtawala na serikali ya aina yoyote?

Hili ni swali linaloelekezwa kwenye madhehebu yote ya Kiislamu, wanazuoni wote wa Kiislamu, Waislamu wote wanaoamini katika Uislamu, na linaelekezwa pia kwa Serikali ya Bahrain; serikali ambayo leo inaweka mipaka kwa wigo mpana wa hukumu thabiti katika Sheria Tukufu ya Uislamu kwa ujumla, na hasa yale yanayohusiana na hukumu kwa mujibu wa madhehebu yaliyopokelewa kutoka kwa Ahlul-Ismah wa Nyumba ya Utume.

Ndiyo, serikali inafanya hivyo, na inafuta Sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika suala la utekelezaji, hukumu na maamuzi, na inafanya uwezekano wa kutekeleza [matukufu na ibada za kidini] utegemee vibali vya kibinadamu vya serikali kwa yale ambayo yenyewe inaona yanafaa. Aidha, inaweka sharti kwamba suala la kuruhusu au kuzuia liwe chini ya matakwa ya serikali yenyewe, hata kama matakwa hayo yanapingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa kufanya hivyo, inabatilisha sheria ya Mwenyezi Mungu, na inamwadhibu Muislamu ambaye haoni kuwa inajuzu kwenda kinyume na Sheria ya Mola Mtukufu!

Na swali jingine: Ni nini kinachozuia madhehebu yote ya Kiislamu, wanazuoni wote wa Kiislamu na kila muumini wa Uislamu kutangaza kwamba jambo hili ni haramu kwa mujibu wa dharura na misingi iliyo wazi ya Uislamu, mbele ya uovu huu mkubwa? Ni uovu ambao ikiwa utaendelea katika njia iliyowekewa, utauangamiza Uislamu kwa ukamilifu na kwa namna isiyoweza kurekebishika?

Hapa, visingizio vyote vimekwisha, na sababu zinazotolewa kwa ajili ya taarifa hii ni dhaifu sana, sana.

Mwenyezi Mungu atuongoze sote kwa uongofu Wake kuelekea njia iliyonyooka.

Issa Ahmad Qasim

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha