Ijumaa 18 Septemba 2026 - 22:56
Kudumisha matumaini na kuimarisha moyo wa kimadhehebu, ustahimilivu na subira katika nyoyo za wananchi wote/ Kuhifadhi utajo wa mashahidi wanazuoni wa dini ni jukumu la kila mmoja

Hawza/ Ayatullah al-dhma Makarim Shirazi, huku akisisitiza umuhimu wa kueneza utamaduni wa kujitolea na jihadi, amesema kuwa kuhifadhi hai kumbukumbu na kueleza mwenendo wa mashahidi wanazuoni wa dini na wanafunzi wa hawza ni miongoni mwa majukumu ya Hawzah na kizazi kipya cha wanazuoni.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Nasser Makarim Shirazi, mmoja wa Mara'jii wakuu wa Taqlidi, ametuma ujumbe katika mkusanyiko wa wanafunzi wa hawza wa Mkoa wa Fars Iran, uliofanyika katika Madrasa ya Imam Musa al-Kadhim (as), maandishi ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu, na rehma zimshukie Bwana wetu Muhammad na Ahlul-Bayt wake watukufu, pamoja na laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie maadui wao wote.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

«فَضَّلَ اللّهُ الْمُجَاهِدِینَ عَلَی الْقَاعِدِینَ أَجْرًا عَظِیمًا / دَرَجَاتٍ مِنْهُ وَمَغْفِرَةً وَرَحْمَةً وَکَانَ اللّهُ غَفُورًا رَحِیمًا»

“Mwenyezi Mungu amewafadhilisha wanaopigana jihadi kuliko wanaokaa bila kushiriki, kwa ujira mkubwa; daraja zitokazo kwake, msamaha na rehema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”

Ni jambo la lazima kwangu, mwanzoni, kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati waandaaji na washiriki wote, hususan wanafunzi waheshimiwa wa Mkoa wa Fars, ambao wamekusanyika katika mkutano huu wenye baraka na uliobarikiwa kwa jina la mashahidi, hususan wanazuoni waliouawa kishahidi.

Vilevile, ni jambo la lazima kwangu kutoa shukrani zangu za dhati kwa uungaji mkono na ushiriki wenye hamasa wa wananchi wetu wapendwa, hususan wananchi wenye heshima wa Mkoa wa Fars, kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na kuwashukuru kwa dhati wote ambao, kupitia juhudi na bidii zao za dhati, katika siku hizi ngumu na zenye changamoto, wamechukua hatua kwa ajili ya heshima, usalama na ustawi wa nchi.

Kipindi tulichopitia kilikuwa kipindi kilichochanganyika na huzuni na matumaini; huzuni kutokana na kushambuliwa nchi ya Kiislamu ya Iran, kuuawa koshahidi baadhi ya wapendwa na wana bora wa nchi hii, hususan kiongozi aliyeuawa kkshahidi (Allah ainue daraja yake), pamoja na hasara za maisha na mali zilizowapata wananchi wenye heshima; na wakati huohuo, matumaini ya kupata ushindi dhidi ya adui mwovu, kujenga upya yale yaliyoharibiwa, na kujenga mustakabali ulio mzuri, ulioendelea zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko hapo awali.

Katika mazingira kama haya, jambo lenye umuhimu mkubwa ni kuhifadhi matumaini haya na kuimarisha moyo wa kimadhehebu, ustahimilivu na subira katika nyoyo za wananchi wote. Bila shaka, mojawapo ya njia za kuimarisha moyo huu ni kuhifadhi kumbukumbu na majina ya wapiganaji ambao walitoa uhai na mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa kauli ya Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu Mtukufu amenunua kutoka kwao nafsi na mali zao kwa malipo ya Pepo, na amewaahidi daraja za juu, msamaha na rehema zake.

Katika jambo hili, mashahidi wanazuoni wa dini na wanafunzi ni miongoni mwa hazina zenye thamani kubwa za Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu; ni watu wakubwa ambao, sambamba na jukumu lao la kielimu, kidini na kimalezi, walikuwa na uwepo wa kipekee katika uwanja wa jihadi na kulinda maadili ya Mwenyezi Mungu. Kwa kutoa maisha yao, walithibitisha ukweli wa imani yao na uaminifu wao kwa Uislamu, wananchi na nchi yao ya Kiislamu. Kwa hiyo, kuhifadhi kumbukumbu na majina ya wapendwa hawa, pamoja na kueleza mwenendo wao, mapambano yao na malengo yao, ni jukumu lililo juu yetu sote, hususan Hawzah na kizazi kipya cha wanazuoni wa dini.

Kuwatambulisha watu hawa kama mifano ya imani na kujitolea itakuwa msingi wa kuhamisha utamaduni wa kujitolea na jihadi kwa vizazi vijavyo, na kutasaidia kuendeleza urithi huu wenye thamani katika jamii ya Kiislamu.

Mwisho, kwa mara nyingine tena, nawapongeza na kuwashukuru kwa dhati wahusika wote na waandaaji wa mkusanyiko huu wenye thamani. Pia nawapelekea salamu zangu za dhati na za upendo, wananchi wacha-Mungu na wapendwa wa Mkoa wa Fars. Na ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azidi kuupa Uislamu na Waislamu heshima na utukufu, awapandishe daraja mashahidi wapendwa, hususan mashahidi wanazuoni wa dini na wanafunzi wa Mkoa wa Fars, na awajaalie nyote, enyi wapendwa, mafanikio na tawfiki.

Na amani iwe juu yenu, pamoja na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.

Qum — Nasser Makarim Shirazi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha