Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Rasul Bagheri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Qademoun, katika kikao cha kwanza cha kimataifa cha “Ujumbe wa Uamsho wa Umma wa Muhammad”, kilichofanyika Jumatano, tarehe 25 Shahrivar 1405 (Sep 16 2026), kwa kuandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Qademoun, akisisitiza umuhimu wa kuvuka hatua za kiishara na mikutano ya kawaida ili kufanikisha umoja wa Kiislamu, alisema: “Leo Umma wa Kiislamu unapaswa kushikana mikono na kusimama pamoja dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani, na kutoka katika ‘Ujumbe wa Uamsho wa Wananchi wa Iran’ kuelekea ‘Ujumbe wa Uamsho wa Umma wa Kiislamu’.”
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Qademoun, akirejea kufanyika kwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w), alisema: “Katika Wiki ya Umoja wa Kiislamu, kulizungumzwa suala la umoja baina ya Shia na Sunni, lakini tunapaswa kujiuliza: Je, umoja wa Kiislamu unapaswa kubaki tu katika kufanyika mikutano, au tunapaswa kutafuta njia za kivitendo za kuufanikisha kwa hakika?”
Akirejea matukio na mapigano ya hivi karibuni katika eneo hilo, aliongeza: “Umma wa Kiislamu katika mazingira ya sasa unapaswa kushikana mikono na kusimama pamoja dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani.”
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Qademoun, akirejea moja ya kauli za hivi karibuni za Kiongozi wa Mapinduzi kuhusu nafasi ya wananchi katika matukio ya nchi, alisema: “Kwa mujibu wa mtazamo huu, iwapo tukio lolote litatokea nchini, Mwenyezi Mungu atawainua wananchi na wananchi watakamilisha jambo hilo. Leo tumeona kwamba wananchi wa Iran walijitokeza katika medani na wakaonesha kwa vitendo dhana hii ya kwaamsha wananchi.”
Bagheri aliendelea kusema: “Hata hivyo, uamsho huu haupaswi kuishia kwa wananchi wa Iran pekee; swali ni kwamba, je, wakati haujafika kwa Umma wa Kiislamu nao kusimama ili kukabiliana na dhuluma na uchokozi, pamoja na kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa?”
Akirejea matukio katika nchi mbalimbali za eneo hilo, alisema: “Nchini Iraq tunaona uwepo wa wananchi pamoja na vikosi vya Al-Hashd Al-Shaabi, na ushirikiano baina ya Shia na Sunni; nchini Lebanon pia Hezbollah na wananchi wa nchi hiyo wapo katika medani. Nchini Pakistan, baada ya kuuawa viongozi na watu mashuhuri wa muqawama, tulishuhudia wananchi wakijitokeza; na nchini Bahrain, Kuwait na Yemen pia kuna dalili za uamsho huu na uwepo wa wananchi.”
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Qademoun, akirejea matukio ya Yemen, alisema: “Leo nchini Yemen tunaona jinsi wananchi wa nchi hii walivyosimama na kukabiliana na utawala wa Kizayuni, mchakato huu unaonesha kwamba tunaweza kutoka katika Ujumbe wa Uamsho wa Wananchi wa Iran na kuelekea katika Ujumbe wa Uamsho wa Umma wa Kiislamu.”
Alisema kuwa “Ujumbe wa Kuuamsha wa Umma wa Kiislamu” unahusiana na kufanikisha umoja baina ya Waislamu, na kuongeza: “Tunatafuta Ujumbe wa Kuuamsha Umma wa Kiislamu, umoja wa Umma wa Kiislamu na kuundwa kwa Umma wa Kiislamu, na harakati hii inapaswa kuendelea katika njia ya kukabiliana na dhuluma, kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa na kuliunga mkono suala na malengo ya Palestina.”
Bagheri, mwishoni, alieleza matumaini yake kwamba umoja na uamsho wa Umma wa Kiislamu utafikia haraka iwezekanavyo hatua ya utekelezaji wa kivitendo, na kusema: “Tunatumaini kwamba jambo hili litatokea hivi karibuni.”
Maoni yako