Alhamisi 23 Julai 2026 - 13:15
Mfalme wa Bahrain Aanzisha Operesheni ya Kuwafuta Mashia

Hawza/ Kitendo cha Ayatullah Sheikh Isa Qassim kuvunja ukimya wake na kutangaza kuwa hatima ya madhehebu ya Shia nchini Bahrain inakabiliwa na tishio la kuwepo kwake, kina maana kwamba sehemu hii ya jamii ya taifa la Bahrain imewekwa katika vita visivyo na mwisho, visivyo na huruma na vya kimfumo vinavyolenga kuiangamiza.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Mir'at al-Bahrain, kitendo cha Ayatullah Sheikh Isa Qassim kuvunja ukimya wake na kutangaza kuwa; hatima ya madhehebu ya Shia nchini Bahrain inakabiliwa na tishio la kuwepo kwake, kinaashiria kwamba sehemu hii ya jamii ya taifa la Bahrain imewekwa katika vita visivyo na mwisho, visivyo na huruma na vya kimfumo vinavyolenga kuiangamiza.

Suala hilo limefikia hatua hatari sana; si tena suala la "kuondolewa" kwa kawaida, bali ni "usafishaji wa kimadhehebu" kwa maana yake kamili. Kiwango hiki cha mashinikizo kinachowekwa na sera rasmi dhidi ya jamii hiyo kimefikia hatua ambayo haiwezekani tena kukaa kimya mbele yake, kwa sababu jambo hilo limevuka mipaka ya kuwekewa vizuizi na kuzingirwa, na sasa imefikia kulengwa utambulisho wa kidini na kijamii wa madhehebu hayo.

Operesheni ya ukandamizaji ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya wanazuoni wenye hadhi walioko magerezani, na ambayo imefichuliwa na Jumuiya ya Al-Wefaq Al-Watani Al-Islamiyyah, haiwezi kukubalika kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Hatua hizi si makosa ya mtu binafsi wala uzembe wa kiutawala, bali ni uhalifu wa kimadhehebu uliopangwa kwa utaratibu na unaoongozwa kutoka katika ngazi za juu kabisa za mamlaka; jambo ambalo Bahrain haijawahi kulishuhudia hapo awali.

Jambo lisilo na shaka ni kwamba Mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa, anawajibika moja kwa moja kwa usalama wa wanazuoni wote waliokamatwa. Kushindwa kusitisha uhalifu huu au kuendelea na sera za adhabu za pamoja na udhalilishaji kutazidisha tu migawanyiko ya ndani na kuongeza hasira za wananchi. Serikali haziendeshwi kwa kuwakandamiza au kuwavunjia heshima wapinzani wake, bali kwa misingi ya uadilifu, utawala wa sheria na kuheshimu utu wa binadamu.

Hatua hatari zaidi ambayo utawala unaweza kufanya ni kudhani kwamba mkono wa chuma unaweza kutatua mgogoro wenye sura za kidini na kitaifa. Kadiri wigo wa ukiukwaji wa haki unavyopanuka, na hisia miongoni mwa wananchi kwamba utambulisho na haki zao zinalengwa zinavyozidi kuimarika, ndivyo gharama za mgogoro huu kwa jamii nzima zitakavyokuwa kubwa zaidi.

Kwa sasa, suala hili linahitaji jumuiya ya kimataifa iliingilie kwa haraka pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu; kuingilia ambako hautakubali madai ya Mfalme wa Bahrain kuhusu "kuishi pamoja kwa amani" au "ustahamilivu wa uongo" kama ukweli usio na shaka. Udanganyifu huu hauwezi tena kuwashawishi maafisa wa kigeni wala waangalizi wa haki za binadamu katika Mashariki na Magharibi mwa dunia.

Huu ni mgogoro wa haki za binadamu na wa kibinadamu unaohitaji kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi, uangalizi makini wa kimataifa na uwajibikaji wa kweli. Isitoshe, haifai kutegemea simulizi rasmi au kampeni za vyombo vya habari zilizoundwa kwa ajili ya kuficha ukweli.

Jumuiya ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu zina wajibu wa kutekeleza viwango vya kimataifa, kuchunguza matukio yaliyopo uwanjani na kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa haki za binadamu, hususan katika kulinda wafungwa na kuhifadhi heshima yao.

Aidha, haikubaliki tena Bahrain kuonekana kupitia picha rasmi pekee inayotangazwa katika mikutano ya kimataifa, wakati wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mafaili ya ukiukwaji wa haki za binadamu unazidi kuongezeka. Heshima haijengwi kwa hotuba za propaganda, bali hupatikana kwa uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria. Ikiwa utawala una imani na simulizi lake, basi njia ya kawaida ni kufungua milango kwa mifumo huru ya kutafuta ukweli. Kila ucheleweshaji katika jambo hili utamaanisha kuthibitisha uhalifu wa utawala huo na kulifanya suala hili liwekwe kwenye ajenda ya mashirika ya kimataifa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha