Jumatatu 27 Julai 2026 - 10:30
Swala ya Umoja yapamba jalada la kitabu “Shia; Ndugu wa Qibla Kimoja”

Hawza/ Kitabu “Shia; Ndugu wa Qibla Kimoja”, kilichoandikwa na Mus'ab Muqaddas, mtafiti kutoka jamii ya Ahlu Sunna nchini Indonesia, kimechapishwa kwa mtazamo wa kihistoria, kielimu na kisiasa kuhusu Ushia, mitazamo ya wanazuoni wa Al-Azhar na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mabadiliko ya kisasa ya ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, akinukuu Kitengo cha Habari cha Mshauri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, kitabu “Shia; Ndugu wa Qibla Kimoja” (Syiah Saudara Sekiblat) kilichoandikwa na Mus'ab Muqaddas, mtafiti na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri, kimechapishwa nchini Indonesia kwa lengo la kutoa taswira yenye nyaraka na ushahidi kuhusu madhehebu ya Shia, mitazamo ya wanazuoni wa Al-Azhar, pamoja na kuchambua nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mabadiliko ya ulimwengu wa Kiislamu. Jalada la kitabu hicho limepambwa na picha ya Swala ya Jamaa iliyoswaliwa kwa pamoja na viongozi wa Ahlu Sunna na Shia katika Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni alama ya umoja wa Kiislamu.

Swala ya Umoja; alama ya jalada la kitabu

Jalada la kitabu hicho lina picha ya kusimamishwa Swala ya Jamaa iliyohudhuriwa na Hujjatul-Islam Muhammad Boroujerdi, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, Dkt. Yahya Jahangiri, Mshauri wa Utamaduni wa ubalozi huo, pamoja na Zain al-Majdi, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Ahlu Sunna na Rais wa Chama cha Wahitimu wa Al-Azhar nchini Indonesia.

Swala hiyo ya Jamaa iliswaliwa wakati Zain al-Majdi alipofika katika Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kutoa pole na kuonesha masikitiko kufuatia shahada ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, Imam Khamenei. Picha ya tukio hilo ikawekwa kwenye jalada la kitabu kama alama ya mshikamano na umoja wa Kiislamu.

Juhudi za kuwatambulisha Shia kwa ushahidi

Mwandishi wa kitabu hiki amejaribu, kwa kutumia vyanzo vya kihistoria, vya kielimu, kisiasa na tafiti zinazohusu mabadiliko ya kisasa katika ulimwengu wa Kiislamu, kutoa taswira pana na yenye ushahidi kuhusu madhehebu ya Shia.

Yaliyomo katika kitabu yanaanza kwa kufafanua maana ya neno "Shia" katika Qur'ani Tukufu, kisha yanachunguza historia ya kuibuka kwa mikondo mbalimbali ya Kishia, maendeleo ya madhehebu ya Shia Ithnaashariyya, na nafasi yake Iran ya kisasa. Aidha, athari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maendeleo ya kikanda na kimataifa ni miongoni mwa mada kuu za kitabu hicho.

Mitazamo ya wanazuoni wa Al-Azhar kuhusu Shia

Sehemu muhimu ya kitabu imejitolea kuelezea mitazamo ya baadhi ya wanazuoni mashuhuri wa Al-Azhar kuhusu madhehebu ya Shia.

Katika sehemu hiyo, yamejadiliwa maoni ya Sheikh wa Al-Azhar, Dkt. Ahmad Al-Tayyib, Dkt. Shawqi Allam, aliyekuwa Mufti Mkuu wa Misri, Dkt. Hassan Al-Shafii, Mkuu wa Kituo cha Tafiti za Imam Ash'ari, pamoja na Dkt. Ali Jumu'ah, mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wakuu wa Al-Azhar, kuhusu Ushia na juhudi za kukurubisha madhehebu ya Kiislamu.

Uchambuzi wa Iran ya kisasa na maendeleo ya kikanda

Sehemu nyingine ya kitabu hicho imejikita katika mfumo wa fikra na siasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Inajadili mada mbalimbali kama misingi ya kiitikadi ya mfumo wa kisiasa, maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, uwezo wa kijeshi, fursa za ushirikiano kati ya Iran na Indonesia, sera ya nyuklia ya Iran, pamoja na maendeleo ya hivi karibuni katika eneo.

Mwandishi kutoka jamii ya Ahlu Sunna nchini Indonesia

Mus'ab Muqaddas ni miongoni mwa wanaharakati na viongozi vijana wa taasisi ya Muhammadiyah nchini Indonesia, na ni mhitimu wa fani ya Historia na Ustaarabu wa Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri. Hapo awali amekuwa akijishughulisha na shughuli za elimu na utafiti wa Kiislamu, na pia amefundisha katika Chuo cha Ualimu cha Muhammadiyah mjini Yogyakarta.

Kitabu hiki chenye jina “Syiah Saudara Sekiblat” kimechapishwa na shirika la uchapishaji la Media Guru.

Zain al-Majdi; mmoja wa watu wenye ushawishi nchini Indonesia

Zain al-Majdi, anayejulikana nchini Indonesia kwa lakabu ya “Tuan Guru Bajang”, ni mmoja wa viongozi mashuhuri wa kidini na kisiasa nchini humo. Aliwahi kuhudumu kwa vipindi viwili kama Gavana wa Mkoa wa West Nusa Tenggara, na katika kipindi cha uongozi wake aliufanya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa iliyofanikiwa zaidi nchini Indonesia kwa upande wa ukuaji wa uchumi na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira.

Alipata elimu yake ya chuo kikuu kuanzia shahada ya kwanza hadi uzamivu katika fani ya Tafsiri na Sayansi za Qur'ani katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri, na kwa sasa ni Rais wa Chama cha Wahitimu wa Al-Azhar nchini Indonesia.

Swala ya Umoja yapamba jalada la kitabu “Shia; Ndugu wa Qibla Kimoja”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha