Jumatatu 3 Agosti 2026 - 12:45
Arubaini ni zao la ujumbe wa milele wa Bibi Zaynab (as)/ Uhai na maendeleo ya kielimu ndiyo njia pekee ya kujibu shubha

Hawza/ Ayatullah Jawadi Amuli amesisitiza kuwa: Harakati ya Arubaini ni zao la ule ujumbe wa milele uliotolewa na Bibi Zaynab Kubra (as) aliposema: “Sisi hatutanyamazishwa kamwe.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawadi Amuli, katika kikao chake na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Gholamhossein Mohseni Ejei, Mkuu wa Mamlaka ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kilichofanyika katika mji wa Damavand, akirejelea kukaribia kwa siku za Arubaini ya Imam Hussein (as), alieleza kuwa; harakati hii kubwa ni tunda la utamaduni wa “Ya Hussein” na ujumbe wa milele wa Bibi Zaynab Kubra (as). Alisema: Harakati ya Arubaini ni zao la ule ujumbe wa kudumu ambao Bibi Zaynab Kubra (as) aliutoa aliposema: “Sisi hatutanyamazishwa kamwe.”

Kisha Marjii huyu wa Taqlid aliendelea kusema: Hotuba za Bibi Zaynab (as) mjini Kufa hazikuwa maneno ya kulia na kuelezea msiba pekee, bali zilikuwa ni maneno yenye kina na msimamo dhidi ya fikra potofu ya kulazimishwa (Jabriyya). Pale Ubaydullah bin Ziyad alipomuuliza Bibi Zaynab: “Je, umeona Mwenyezi Mungu amemfanyia nini ndugu yako?” au pale aliposema: “Ali bin al-Hussein aliuawa na Mwenyezi Mungu huko Karbala!” Hapa mazungumzo hayakuwa kuhusu mimi, sisi, Banu Umayyah au wengineo, bali yalikuwa yanamhusu Mwenyezi Mungu na yalitolewa kwa mtazamo wa fikra ya Jabriyya. Ndipo Bibi Zaynab (as) akajibu: «ما رأيتُ إلا جمیلا» (Sikuona chochote isipokuwa uzuri). Yaani, matendo ya Mwenyezi Mungu ni mazuri, lakini nyinyi ndio wauaji. Ni nyinyi mliomuua kishahidi Ali bin al-Hussein, hivyo Bibi Zaynab (as) alivunja fikra ya Jabriyya ya Banu Umayyah na kubainisha ukweli wa hiari ya mwanadamu pamoja na wajibu wake.

Ayatullah Jawadi Amuli, akirejelea miaka arobaini ya juhudi za kielimu katika kufasiri Qur'ani Tukufu, alisema: Hawza hii kubwa na yenye mizizi imara, katika kipindi cha miaka arobaini na kwa juhudi za vizazi vinne vya wanafunzi na walimu wake—ambapo kila kizazi kilitumia miaka kumi ya juhudi endelevu na zisizo na mfano—imejishughulisha na tafsiri ya Qur'ani Tukufu. Ikiwa Tafsiri ya Tasnim imechukua muda mrefu kukamilika, sababu yake ni kuibuka kwa masuala mapya ya kielimu pamoja na hoja na maswali mapya yaliyojitokeza katika kipindi chote hiki.

Marjii huyu wa Taqlid aliendelea kusema: Mbele ya kila tatizo na kila suala lililojitokeza, vizazi hivi vilijitahidi na majibu ya changamoto hizo yakatolewa, kwa hiyo njia hii ya tafsiri haikufanywa na mtu mmoja pekee, haya si maneno ya kujipendekeza, bali ni ukweli ulio wazi, kazi hii ni matokeo ya juhudi za pamoja za Hawza ya Kielimu.

Alisisitiza kuwa: Hawza inapaswa daima kuwa tayari kujibu shubha, ukosoaji na maswali mapya. Itaweza kufanya hivyo pale tu itakapohifadhi upeo wake mpana na uhai wake wa kielimu. Kwa hiyo, ni lazima mijadala ya kimsingi kama vile “Asalat al-Hurriyah” (Uasilia wa Uhuru) pamoja na misingi mingine inayohusiana nayo ifundishwe na kufafanuliwa kwa njia ya kielimu ndani ya Hawza.

Ayatullah Jawadi Amuli pia, akizungumzia nafasi ya elimu ya ghaibu katika fiqhi ya Kiislamu, alisema: Elimu ya ghaibu si hoja ya kutoa hukumu za kifiqhi, ndiyo maana Maasumina (as), licha ya kuwa na elimu ya Mwenyezi Mungu, walikuwa wakitoa hukumu kwa msingi wa ushahidi na viapo. Kama walivyosema:

«إِنَّمَا أَقْضِی بَیْنَکُمْ بِالْبَیِّنَاتِ وَالْأَیْمَانِ»

"Hakika mimi nahukumu baina yenu kwa ushahidi na viapo."

Ikiwa mtu atapata haki ya mwingine kwa ushahidi wa uongo, basi kwa hakika amejipalia moto mwenyewe, hata hivyo hukumu hutolewa kwa msingi wa vielelezo vinavyoonekana na mizani ya sheria ya Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli alieleza kuwa; ushiriki mkubwa na wa kujitolea wa wananchi katika nyanja za kuilinda Mapinduzi ya Kiislamu na nchi ni miongoni mwa vielelezo vya nusura ya Mwenyezi Mungu. Akinukuu Aya Tukufu:

﴿هُوَ الَّذِی أَیَّدَکَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِینَ﴾

alisema: Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaleta Waumini uwanjani ili waisaidie dini Yake. Ushiriki huu wa makusudi wa wanaume, wanawake, vijana na makundi mbalimbali ya wananchi ni mfano halisi wa nusura ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu yuleyule aliyewapa Waislamu ushindi mkubwa mwanzoni mwa Uislamu, leo pia anao uwezo wa kuisaidia jamii ya Waumini, kama ilivyokuwa katika Vita vya Badr ambapo Waislamu hawakutarajia ushindi na maadui hawakutarajia kushindwa, lakini matakwa ya Mwenyezi Mungu yalihakikisha kutimia kwa ahadi Yake.

Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli aliwakumbuka kwa heshima mashahidi wote wa Uislamu na wa Mapinduzi ya Kiislamu, hususan Kiongozi Shahidi, na akamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awafufue pamoja na mashahidi wa Karbala. Pia alimuomba Awajaalie watumishi wa Mfumo wa Kiislamu mafanikio katika kuilinda amana hii ya Mwenyezi Mungu, ili waweze kuikabidhi bendera hii mikononi mwa Mmiliki wake wa kweli, Imam wa Zama, Al-Hujjah, Imam al-Mahdi (aj).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha