Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Islami Analysis, kamanda wa kikosi cha "Tzabar", kilicho chini ya Brigedi ya "Givati", aliwataka wanajeshi waliokuwa katika kambi ya kijeshi ya "Sde Teiman" kuondoa mabango, bendera na kumbukumbu nyingine zinazohusiana na operesheni za kijeshi kutoka eneo la kumbukumbu lililopo ndani ya kambi hiyo. Hata hivyo, uamuzi huo ulikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanajeshi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makumi ya wanajeshi waliondoka kambini huku wakipaza sauti wakisema: "Makamanda wote waende Jahannamu," na wakakataa kutekeleza amri ya makamanda wao.
Jeshi la utawala wa Kizayuni pia, katika taarifa yake, lilithibitisha kuwa idadi ya wanajeshi wa kikosi kimoja cha mapigano waliondoka katika kambi yao bila kupata ruhusa kutoka kwa makamanda wao, baada ya kutolewa kwa amri ya kuondoa kumbukumbu hizo.
Jeshi la Israel pia liliweka muda wa mwisho wa saa 10:00 jioni kwa saa za eneo husika (16:00) kwa wanajeshi hao kurejea kambini.
Mtandao wa televisheni wa serikali ya Israel "Kan" pia uliripoti kuwa katika siku za hivi karibuni wanajeshi waliorejea kutoka kwenye mapigano nchini Lebanon walikuwa wameagizwa kuondoa eneo lililotengwa kwa ajili ya kumbukumbu za wanajeshi waliouawa pamoja na bendera zilizokuwa zimewekwa kambini. Kufuatia uamuzi huo, baadhi ya wanajeshi waliweka silaha zao chini kama hatua ya kupinga, na vyombo vya habari vya Israel vikaitaja hatua hiyo kuwa ni "uasi."
Kambi ya kijeshi ya "Sde Teiman", iliyoko katika Jangwa la Negev, ndiyo makao ya kikosi cha "Tzabar" cha Brigedi ya "Givati", kikosi ambacho kimeshiriki katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na Lebanon.
Kambi hiyo pia imepata sifa mbaya kutokana na ripoti nyingi kuhusu unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za wafungwa wa Kipalestina waliohamishwa kutoka Ukanda wa Ghaza. Kwa sababu hiyo, mara nyingi hutajwa kwa jina la "Guantanamo ya Israel."
Maoni yako