Alhamisi 6 Agosti 2026 - 11:23
Bila ya Kusini Lebanon na watu wake, serikali itakuwa dhaifu, isiyo imara na isiyo na uhalali

Hawza/ Mufti Mkuu wa Jaafaria nchini Lebanon amesisitiza kuwa; serikali ambayo haishiriki Kusini mwa Lebanon na wananchi wake itabaki kuwa serikali dhaifu, isiyo imara, isiyo na uzito wa kisiasa wala uwakilishi wa kweli, na haitakuwa na uhalali wowote wa kitaifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti Mkuu wa Jaafari nchini Lebanon, amesema katika taarifa yake ya Jumatano kuwa; serikali isiyokuwa na ushiriki Kusini mwa Lebanon na watu wake itabaki kuwa serikali dhaifu, isiyo imara, isiyo na uzito wa kisiasa wala uwakilishi wa kweli, na haitakuwa na uhalali wowote wa kitaifa.

Amesisitiza kuwa; Lebanon imejengwa juu ya misingi thabiti ya kitaifa ambayo haikubali masharti ya pembeni, na akaonya kwamba, kuidhoofisha nafasi ya kitaifa ya Jeshi la Lebanon ni sawa na kuchinja taifa zima na kupiga pigo katika kiini na msingi mkuu wa muundo wa Lebanon.

Kipaumbele cha maslahi ya taifa kuliko mashinikizo ya kigeni

Sheikh Qabalan alisema: Kwa kuwa suala hili linatuhusu sisi kama Walebanon, na kwa kuwa mantiki ya mataifa yenye nguvu imejengwa juu ya kuimeza nchi, utajiri na mamlaka ya mataifa katika eneo ambalo liko katika hatua hatari zaidi za mabadiliko ya kikanda na kimataifa, naiambia serikali ya sasa kwamba hata kama tutakuwa na tofauti kiasi gani, hakuna mji mkuu wowote duniani unaoyajali zaidi maslahi ya Lebanon kuliko wananchi wa Lebanon wenyewe. Ukweli huu unatulazimisha kusisitiza umoja wetu wa kitaifa kwa mujibu wa mfumo wa makubaliano ya Lebanon. Historia ya nchi hii inaonyesha wazi kwamba yeyote anayechukua njia ya peke yake anajipeleka kwenye maangamizi, Serikali ya kisiasa ambayo itategemea nguvu za nje na kutoa kafara maslahi ya wananchi pamoja na mamlaka ya taifa haitakuwa na uwezo wa kutawala, huu ni ukweli wa kihistoria uliothibitika ndani ya Lebanon na mizania yake ya msingi, wazo la kuikabidhi Lebanon kwa mataifa ya nje ni sawa na kichocheo cha bomu la nyuklia linalochoma kila kitu.

Nafasi ya Spika wa Bunge (Nabih Berri)

Aliongeza kuwa jambo ambalo limethibitika kihistoria na kwa sasa ni kwamba serikali, kama mfumo wa makubaliano ya kitaifa, haiwezi kufanya kazi bila ushirikiano, mshikamano na uratibu wa karibu kati ya taasisi za kitaifa, kuwepo kwa Nabih Berri ni fursa ya kihistoria ambayo athari zake zinazidi mipaka ya Lebanon na eneo zima. Rais Aoun na Waziri Mkuu Salam wanapaswa kushirikiana naye kwa ajili ya kufanikisha makubaliano kamili ya kitaifa, bila ya Berri hakutakuwa na Lebanon, hakutakuwa na utulivu wala suluhisho la kitaifa, watu kama Nabih Berri ni nadra sana katika eneo hili, na ni fursa ya kitaifa ambayo ikipotea haitafidiwa, atakayeharibu mtaji huu wa kitaifa, kwa hakika atakuwa ameiweka Lebanon yote kwenye moto.

Tahadhari kuhusu sera za Washington na Tel Aviv

Sheikh Qabalan alisisitiza kuwa; sasa ni wakati wa kuiokoa Lebanon, na hakuna wokovu bila ushirikiano na mshikamano unaozingatia vipaumbele vikuu na namna ya kushughulikia tofauti kuu, hali ya sasa na hatari zilizopo haziruhusu majaribio ya kisiasa, kukabidhi mamlaka kwa wageni wala mikutano ya siri ya kisiasa. Washington na Tel Aviv zinaichukulia Lebanon kama bomba lililojaa sumu na hazioni ndani yake isipokuwa maslahi yao ya kiusalama na kisiasa, hata Balozi Michel Issa alifutilia mbali matokeo ya duru ya mazungumzo ya Roma kabla hayajakamilika kwa namna iliyokuwa ni dharau kwa serikali ya sasa.

Aliongeza kuwa; njia ya kutatua matatizo ya ndani inapitia katika "uokozi wa kisiasa", na bila ya chaguo hilo serikali haitakuwa tena nguvu ya kitaifa wala chombo cha uwakilishi. Lebanon imejengwa juu ya misingi ya kitaifa isiyokubali masharti ya pembeni, itikadi ya kitaifa ndiyo msingi wa misingi hiyo, na Jeshi la Lebanon lina jukumu na dhamana ya kulinda taifa. Hivyo, kuondoa nafasi yake ya kitaifa ni sawa na kuichinja nchi nzima na kupiga pigo katika kiini cha muundo wake.

Umuhimu wa kuutegemea "Muqawama na Jeshi"

Mufti Mkuu wa Jaafaria aliendelea kusema kuwa; ulazima wa kitaifa unahitaji kuimarishwa uwezo wa mshikamano wa kitaifa na nyenzo zote za nguvu ya taifa, kwa kuwa hatari zinazoikabili Lebanon ni za kudumu, kubwa na za kimsingi, na zimeendelea kwa miongo kadhaa. Hali hii inauweka Muqawama, Jeshi na fikra za mamlaka ya kitaifa katikati ya mradi wa kimkakati unaopaswa kuandaa upya misingi ya "Mkakati wa Usalama na Ulinzi wa Kitaifa usioegemea madhehebu" kwa kuendana na ukubwa wa vitisho vya kikanda na kimataifa.

Alisema kuwa; hili ndilo hitaji muhimu zaidi la kitaifa, na kuliacha mikononi mwa Washington pamoja na maonesho ya sasa ya mazungumzo ni sawa na kudunga sumu kali katika mishipa ya Lebanon. Kutokana na ugumu mkubwa wa mfumo wa kisiasa wa Lebanon, serikali inapaswa kufuata sera ya "Umoja wa Kitaifa" inayotumikia maslahi ya Lebanon, hususan Kusini mwa Lebanon ambayo tangu mwaka 1948 hadi leo imebeba gharama ya kulinda mamlaka ya taifa kwa niaba ya nchi nzima. Bila ya mtazamo huo, serikali ya sasa haitaweza kutekeleza ahadi zake ambazo zinapingana na maslahi ya taifa.

Kusini Lebanon; Nguzo ya Mamlaka ya Taifa

Mwishoni, Sheikh Ahmad Qabalan aliisemesha serikali ya sasa: Naiambia serikali ya sasa kwamba bila ya Kusini mwa Lebanon na watu wake, serikali itabaki kuwa dhaifu, isiyo imara, isiyo na uzito wa kisiasa wala uwakilishi wa kweli, na haitakuwa na uhalali wowote wa kitaifa. Sababu yake ni kwamba leo serikali iko mezani kwa mazungumzo huku Israel ikiendelea na mabomu na uharibifu, hali ambayo ni udhalilishaji wa makusudi wa mfumo wa kisiasa na uwezo wa Lebanon wa kujadiliana. Suluhisho pekee liko katika meza ya umoja wa kitaifa, kuweka mbele vipaumbele vya mamlaka ya taifa na kutafuta mfumo wa kuhuisha mkataba wa serikali na taasisi zake. Vinginevyo, hakutakuwa na mamlaka, hakutakuwa na uwakilishi wa kitaifa wala uwezo wa kuiokoa Lebanon.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha