Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, zoezi hilo limeandaliwa na Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) kwa ushirikiano na Hawza ya Imam Swadiq (as), ikiwa ni sehemu ya shughuli zinazofanyika kila mwaka katika mwezi wa Muharram kwa lengo la kuhuisha ujumbe wa Karbala na kuonesha mshikamano na huduma kwa jamii.
Imeelezwa kuwa mpango huo wa uchangiaji damu umekuwa ukitekelezwa kila mwaka kama ishara ya kukumbuka matukio ya kusikitisha ya Karbala, ambapo damu za watu wema na watukufu, wakiongozwa na Imam Hussein (as), zilimwagika kwa dhuluma katika njia ya kutetea haki, uadilifu na mafundisho ya kweli ya Uislamu.
Zoezi hilo limewashirikisha waumini wengi ambao walijitokeza kwa hiari kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa na watu wenye mahitaji mbalimbali ya huduma hiyo muhimu, hatua ambayo imepongezwa kama mchango mkubwa wa kibinadamu na kijamii.
Washiriki wa zoezi hilo wameeleza kuwa uchangiaji damu katika mwezi wa Muharram ni njia mojawapo ya kugeuza mafunzo ya Ashura kuwa vitendo halisi vinavyowanufaisha watu, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza shughuli kama hizo zinazookoa maisha ya binadamu.
Zoezi hilo limefanyika katika mazingira ya mshikamano, kujitolea na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as), likiwa sehemu ya maadhimisho ya Muharram yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kwa lengo la kuhuisha ujumbe wa Imam Hussein (as) kupitia kuihudumia jamii na matendo ya kheri.






Maoni yako