Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Bashiri alikuwa miongoni mwa wazungumzaji waliotoa nasaha katika majlisi hizo za maombolezo, katika muhadhara wake, alieleza kwa uchungu na masikitiko makubwa kuhusu msiba mzito uliompata Imam Hussein (as), Ahlu Bayt wake na wafuasi wake waaminifu katika jangwa la Karbala, tukio ambalo limeendelea kuacha athari za huzuni katika nyoyo za Waislamu na wapenda haki duniani kote kwa karne nyingi.
Aidha, Sheikh Bashiri aliwakumbusha waumini umuhimu wa kuhuisha ujumbe wa Ashura na kujifunza masomo ya kusimama upande wa haki, uadilifu na kujitolea kwa ajili ya kutetea dini ya Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Imam Hussein (as).
Kwa upande mwingine, Sheikh Ramadhani Amini naye alikuwa miongoni mwa wahadhiri waliopata fursa ya kuzungumza na waumini waliohudhuria majlisi hizo, katika nasaha zake, aliwakumbusha washiriki matukio mbalimbali ya kusikitisha yaliyotokea katika tukio la Karbala, akibainisha namna familia ya Mtume (saww) ilivyopitia mateso makubwa, dhuluma na majaribu mazito baada ya kuuawa kishahidi Imam Hussein (as).
Majlisi hizo zimeendelea kuhudhuriwa na waumini wengi ambao wamekusanyika kwa lengo la kuomboleza msiba wa Karbala, kuonyesha mapenzi yao kwa Imam Hussein (as) na kuhuisha malengo matukufu aliyoyasimamia hadi dakika zake za mwisho katika uwanja wa Karbala.




Maoni yako