Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, Numan Kurtulmuş, Spika wa Bunge Kuu la Taifa la Uturuki, katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Mabunge ya NATO uliofanyika Istanbul, alirejelea maendeleo ya usalama duniani na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha diplomasia sambamba na ushirikiano wa kiulinzi. Alisema: NATO, mbali na kuendeleza uwezo wake wa kijeshi, inapaswa pia kuwa na mchango katika kuanzisha mifumo ya kufanikisha amani.
Akizungumzia mabadiliko ya mizani ya nguvu duniani kuelekea mfumo wa dunia wenye nguvu nyingi, alieleza kwamba; changamoto za sasa haziwezi kutatuliwa kwa mbinu za zamani, na kwamba usalama wa kudumu unaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo na diplomasia. Kurtulmuş alisisitiza kuwa: Uturuki, huku ikisimama dhidi ya uchokozi na ukiukwaji wa sheria za kimataifa, daima imeunga mkono mazungumzo na utatuzi wa migogoro kwa njia za kidiplomasia.
Spika wa Bunge la Uturuki pia alirejelea vita vya Urusi na Ukraine, akakumbusha juhudi za Ankara za kupatanisha pande mbili, na akayataja makubaliano ya ukanda wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi pamoja na kubadilishana wafungwa kuwa mifano ya mafanikio ya diplomasia.
Aidha, alikaribisha mwenendo wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani na kueleza matumaini yake kwamba mazungumzo hayo yataishia katika usitishaji wa mapigano na amani ya haki na ya kudumu, na kwamba hayatapotoshwa na vitendo vya uchochezi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kurtulmuş alilitaja suala la Palestina kuwa moja ya vitisho vikubwa zaidi kwa amani ya dunia. Alisema; mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza yamefikia kiwango ambacho, kwa mujibu wa vigezo vya sheria za kimataifa, yana sifa za mauaji ya kimbari. Alisisitiza kwamba; tatizo si kuuawa kwa makumi ya maelfu ya raia wasio na hatia au kuharibiwa kwa Ghaza pekee, bali pia mustakabali na matumaini ya ubinadamu ndiyo unaolengwa.
Spika wa Bunge la Uturuki, akisisitiza kwamba; suluhisho la mataifa mawili ndilo chaguo pekee la kufanikisha amani, alitoa wito wa kuundwa kwa dola huru na yenye mamlaka kamili ya Palestina, yenye mji mkuu wake katika Quds Mashariki. Alisisitiza akisema: "Kukomeshwa kwa uchokozi wa serikali ya Israel hakumaanishi tu kuleta utulivu kwa Wapalestina, bali pia ndiko kutakakohakikisha amani ya dunia."
Aliongeza kwa kusema: "Maadamu Wapalestina hawajapata uhuru wao, amani katika Mashariki ya Kati haitapatikana kamwe."
Maoni yako