Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Matembezi hayo yamefanyika leo, tarehe 28 Swafar 1448 AH, yakiongozwa na Hawza ya Imam Swa'diq (as) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Shia Ithnaasharia Tanzania (TIC), na kushirikisha mamia ya waumini kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Matembezi hayo yalianzia katika eneo la Ilala Boma, kisha waombolezaji wakatembea kupitia Barabara ya Msimbazi, kuelekea eneo la Njiapanda ya Mbuyuni, kabla ya kuhitimisha safari yao katika Msikiti wa Ghadir, uliopo katika makao makuu ya Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC).
Matembezi hayo yaliongozwa na Sheikh Mkuu wa Mashia Tanzania, Maulana Hemed Jalala Mwakindenge, ambaye aliongoza waumini katika maandamano hayo ya maombolezo yaliyojaa huzuni, heshima na mapenzi makubwa kwa Mtume Muhammad (saww). Aidha, matembezi hayo pia yalishirikisha wageni mbalimbali, akiwemo Kiongozi Mkuu wa Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, masheikh pamoja na viongozi wengine wa dini na jumuiya katika ngazi mbalimbali.
Ushiriki huo uliifanya shughuli hiyo kuwa jukwaa muhimu la kuonesha umoja wa waumini katika kuhuisha kumbukumbu ya Mtume Muhammad (saww) na kusisitiza umuhimu wa kushikamana na mafundisho yake.
“Huyu Ndiye Mtume Muhammad (saww)”
Kauli mbiu kuu ya matembezi hayo ilikuwa ni hii isemayo “Huyu Ndiye Mtume Muhammad (saww)”, ujumbe uliolenga kumtambulisha Mtume wa Uislamu kwenye jamii kwa kuangazia maisha yake, tabia zake njema, sifa zake tukufu pamoja na changamoto na mitihani mikubwa aliyokabiliana nayo katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu.
Kauli mbiu hiyo pia ilibeba ujumbe wa kuwakumbusha waumini kwamba kumuenzi Mtume Muhammad (saww) si kwa maneno pekee, bali pia ni kwa kufuata mwenendo wake, kushikamana na mafundisho yake na kuyaishi katika maisha ya kila siku.
Kwa upande mwengine katika kuyapa matembezi hayo mguso wa kipekee wa maombolezo, nyimbo za huzuni na maombolezo ya kumkumbuka Mtume Muhammad (saww) ziliimbwa huku zikiongozwa na Sheikh Idi Wambua, akishirikiana na waombolezaji wenzake.
Nyimbo hizo zilizoambatana na safari ya waombolezaji, ziliongeza hali ya huzuni na kuamsha hisia za mapenzi na mahaba kwa Mtume Muhammad (saww), huku washiriki wakionesha kwa nyuso na nyoyo zao, uchungu wa kuadhimisha siku ya kuondoka Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu.
Matembezi hayo yamekuwa sehemu ya shughuli za kuhuisha kumbukumbu ya Mtume Muhammad (saww), na pia fursa ya kuwakumbusha waumini umuhimu wa kuendelea kuutangaza ujumbe wake wa imani, maadili mema, umoja, huruma na haki katika jamii.









Maoni yako