Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli, katika hotuba yake ameeleza nukta muhimu kuhusu ukubwa wa msiba wa kufariki dunia kwa Mtume Mtukufu (saww), ambazo zinawasilishwa kwenu wasomaji kama ifuatavyo:
Amirul Muuminina (as) anasema kuhusu msiba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww): Kila msiba mbele ya msiba wako ni “jallal”. Neno “jallal” maana yake ni kitu kidogo na kisicho na uzito; kwa sababu msiba wako ni mkubwa na wenye utukufu. Anasema:
«وَ إِنَّ الْمُصَابَ بِکَ لَجَلِیلٌ، وَ إِنَّهُ قَبْلَکَ وَ بَعْدَکَ لَجَلَلٌ» ¹
Msiba wako na kufariki kwako ni mkubwa, mzito na wenye kutisha; lakini misiba iliyotokea kabla ya msiba wako au itakayotokea baada ya msiba wako ni “jallal”, yaani ni midogo na isiyo na uzito. Huo ndio msiba mkubwa, nao ni mkubwa; na kila kitu kingine isipokuwa huo ni “jallal”, yaani kidogo na kisicho na uzito.
Katika sehemu nyingine, alizungumzia tukio chungu la kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), na akamuelekea Mtume (saww) kwa kusema:
«لَقَد خَصَّصْتَ حَتَّی صِرْتَ مُسَلِّیاً عَمَّنْ سِوَاکَ وَ عَمَّمْتَ حَتَّی صَارَ النَّاسُ فِیکَ سَوَاءً.» ²
Akasema: Msiba wako una sifa ya pekee inayoufanya uwe faraja mbele ya misiba mingine. Hakuna msiba unaolingana na msiba wako, na ikiwa misiba mingine isiyokuwa msiba wako itatokea, sisi tunaweza kuistahimili kwa kuutazama msiba wako; kwa sababu misiba hiyo mingine ni midogo.
Rejea:
¹. Hikma ya 292.
². Hotuba ya 235, Nahjul-Balagha.
Maoni yako