Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hafla hii, ambayo hufanyika kila mwaka, huandaliwa kwa kuheshimu na kuadhimisha kumbukumbu ya mazazi ya Bibi Fatima Zahraa (a.s), mmoja wa wanawake bora na mwenye nafasi ya pekee katika historia ya Uislamu. Zoezi hilo hufanyika kila mwaka chini ya usimamizi wa Taasisi ya Almustafa Al-Khairiya, ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha vijana kuingia kwenye maisha ya ndoa kwa urahisi na heshima.
Sherehe hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini, wakiwemo masheikh kutoka maeneo tofauti ya nchi, huku Mgeni Rasmi akiwa ni Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Sheikh Ally Jumaa Luwuchu. Katika hotuba yake, Sheikh Luwuchu aliwapongeza wanandoa na kuhimiza jamii kuendeleza utamaduni wa kuandaa ndoa zenye misingi ya maadili na uadilifu.
Aidha, Sheikh Hemed Jalala aliwahusia vijana walioingia katika ndoa kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika safari yao ya maisha mapya, ikiwemo kuimarisha mawasiliano, kuheshimiana, kusameheana, kutanguliza hofu kwa Mwenyezi Mungu, na kujenga familia yenye upendo, subira na ushirikiano. vile vile Alisisitiza kuwa ndoa ni taasisi takatifu inayohitaji hikima, uadilifu na jitihada za pamoja ili idumu kwa amani na baraka.
Hafla hii imeendelea kuwa chachu ya kuwasaidia vijana kuanza maisha ya ndoa katika mazingira ya upendo, umoja na wepesi katika mambo yao ya kiuchumi, sambamba na kuhuisha kumbukumbu ya mafundisho ya Bibi Fatima Zahraa (a.s).







Maoni yako