Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohsen Qiraati, katika mkutano wa wanafunzi na maulamaa, uliofanyika katika jengo la Yawaran wa Hadhrat Mahdi (a.j.) mjini Qum Iran, alisema: Wakati mwingine tafiti nyingi hufanywa lakini hazina zao la kivitendo kwenye jamii. Nilitembelea taasisi moja iliyokuwa na tasnifu 800 za uzamivu (PhD) kuhusu Qur’ani Tukufu, lakini mada hizo nyingi haziwezi hata kujadiliwa kwenye runinga wala hazina manufaa kwa watu wa kawaida. Hizi ni mada zisizo na matumizi ya moja kwa moja. Lau watafiti wangetumia muda wao kufanya tafiti zinazokidhi mahitaji ya jamii, manufaa yangekuwa makubwa zaidi.
Mwenyekiti wa Baraza la Kusimamisha Swala (Setad-e Iqamat-e Namaz), katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisisitiza juu ya tabligh ya ana kwa ana na akasema: Tabligh ya ana kwa ana ni muhimu sana. Lazima kwenda sambamba na watu na kuwasilisha maarifa ya dini kwa lugha nyepesi na rahisi. Wanzuoni wanaofanya tabligh ya ana kwa ana kwa ufanisi hupata mafanikio makubwa.
Akigusia umuhimu wa tafsiri ya Qur’ani kuwa inayoeleweka, alisema: Tafsiri yoyote inayoandikwa lazima iwe kwa namna ambayo watu wa kawaida waielewe, na wasomi pia wapendezwe nayo. Qur’ani Tukufu inasema katika aya ya 32 ya Surat al-Qamar:
“وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ”Kwa hakika Sisi tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kwa mawaidha; basi yupo anayepokea mawaidha?
Ushauri kwa Wanafunzi wa dini
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qiraati mwishoni mwa hotuba yake akiwahutubu wanafunzi wa dini alisema: Msimsubiri mtu. Ninyi wenyewe lazima mchukue hatua za mwanzo. Mkiwa na maandalizi, fursa zitajidhihirisha zenyewe. Mimi nimetoa nukta 2,600 za kisheria (kihoja) kutoka katika Qur’ani, ambazo leo zinafundishwa chuoni kama kitabu cha masomo.
Maoni yako