Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sayyid Yasin Mousawi — Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mwalimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf — katika khutba za Swala ya Ijumaa ya jana, alieleza kuwa; wiki iliyopita, kulishuhudiwa mabadiliko muhimu katika uwanja wa ndani na wa kimataifa, ambapo Iraq ilikuwa katika kiini cha mabadiliko hayo. Alibainisha kuwa kumbukumbu ya ushindi na Siku ya Hashdu Shaabi ni alama muhimu ya kihistoria na ya hatima katika safari ya taifa na dola ya Iraq.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, akirejelea kipindi hatari mno ambacho Iraq ilikipitia, alisema: njama kubwa ya kuigawa na kuiangusha Iraq ilipangwa kupitia ugaidi wa kitakfiri; bila kujali waliokuwa watekelezaji wake ni akina nani, kilichotekelezwa ilikuwa ni mradi ulio wazi, mahsusi na wenye malengo yaliyopangwa. Kwa mujibu wake, fatwa ya jihadi ya kifaya iliyotolewa na Marja‘iya Kuu ya Kidini, Mtukufu Ayatollah Udhma Sayyid Ali Sistani, sambamba na roho ya juu ya utaifa ya wananchi wa Iraq, ndivyo vilivyounda nguzo kuu ya kuisambaratisha njama hio.
Ayatollah Mousawi aliongeza: Wairaqi waliitikia wito wa Marja‘iya, wakaelekea katika medani za mapambano, wakajaza safu za mapambano, na kwa kutoa sadaka kubwa za mashahidi na majeruhi, waliweza—katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja—kuikomboa ardhi yao; hali ambayo ilipingana kabisa na makadirio ya Wamarekani waliodai kuwa vita hivyo vingechukua takriban miaka kumi.
Alisisitiza kuwa: Serikali ya Iraq wakati huo iliomba msaada kutoka Marekani, lakini jibu lililotolewa lilikuwa kwamba Marekani haina uwezo wa kutoa msaada wa haraka na inahitaji kufanya tafiti zitakazochukua kwa miezi sita; jambo ambalo kivitendo lilikuwa sawa na kuiacha Iraq iangamie. Hata hivyo, taifa la Iraq kwa kuwategemea Hashdu Shaabi, muqawama, wanazuoni na Marja‘iya yake, lilithibitisha upotofu wa mahesabu hayo na kuwaonesha Wamarekani uwezo wake wa kuunda ushindi wa kihistoria.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad katika sehemu nyingine ya khutba zake alisisitiza kuwa nguvu za kitaifa zilizoikomboa Iraq na kuweka misingi ya uthabiti wake bado zinaendelea kutekeleza majukumu yao, huku kivuli cha himaya ya Marekani kikitanda wazi nchini.
Alisema: Iraq bado inakabiliwa na aina mbalimbali za uvamizi. Katika muktadha huo, alirejelea uamuzi uliotangazwa hivi karibuni katika gazeti rasmi la “Al-Waqa’i‘ al-‘Iraqiyya”, ambapo Hizbullah na Ansarullah waliwekwa katika orodha ya makundi ya kigaidi na miamala yote yao ya kifedha ikapigwa marufuku; uamuzi ambao baadaye serikali iliuelezea kuwa ni “kosa la kiutawala”.
Ayatollah Mousawi alifichua kuwa: kamati husika katika Benki Kuu ya Iraq inaundwa na wajumbe wa Kiiraq na wa Kimarekani, na kuingizwa majina ya makundi hayo kulikuwa ni matokeo ya kufuata maagizo ya Marekani, ilhali kwa hakika hakuna akaunti rasmi wala miamala ya kifedha ya taasisi hizo ndani ya Iraq. Kwa mujibu wake, jambo hili linaonesha wazi kuwa maamuzi ya kifedha na kiuchumi ya Iraq bado yako chini ya matakwa ya Marekani.
Aidha, alirejelea kauli za wajumbe wa Marekani, hususan katika kipindi cha urais wa Donald Trump, na akaonya kuhusu mashinikizo makubwa yanayoelekezwa katika mchakato wa kuunda serikali ya Iraq; mashinikizo ambayo masharti yake ni kuondolewa kwa mtu yeyote aliye karibu na makundi ya muqawama, la sivyo Baghdad itakabiliwa na kusitishwa mahusiano ya kimataifa. Alisisitiza kuwa; wananchi wa Iraq wanapaswa kuwa na uelewa kamili kuhusu asili na malengo ya sera hizi.
Ayatollah Mousawi alifafanua kuwa; mkakati mpya wa Marekani katika kipindi cha Trump unatofautiana kimsingi na sera za nyuma; kwani kauli mbiu ya “kusambaza demokrasia” imeondolewa, na badala yake mkazo umelekezwa kwenye kulinda maslahi ya Marekani pekee ambapo hilo litafanikisha kupitia sera za kinyama, vitisho vya wazi vya uvamizi au uingiliaji wa kijeshi, hali ambayo athari zake zinaonekana wazi katika eneo lote na ndani ya Iraq.
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliwataka viongozi wa kisiasa wa Iraq kuendesha mazungumzo yao na Marekani kwa misingi ya uhalisia, akisisitiza kuwa uhuru haupatikani kwa siku moja, bali ni matokeo ya jihadi ndefu inayoanzia katika uhamasishaji wa kitamaduni na elimu ya wananchi kuhusu umuhimu wa mamlaka ya kitaifa.
Vilevile, alisisitiza ulazima wa wananchi na Bunge lijalo kuibana serikali ijayo ili iandae mkakati wa kitaifa ulio wazi; mkakati ambao kabla ya kuingia katika maelezo ya uundaji wa serikali, uainishe misingi isiyoyumba ya mamlaka na ujenzi wa dola huru ya Iraq. Katika muktadha huo, alikosoa vikali siasa za kuabudu watu, ambapo mtu, chama au kiongozi hutangulizwa mbele ya maslahi ya taifa na raia.
Ayatollah Mousawi alisisitiza kuwa uzalendo si kauli mbiu tupu, bali ni mwenendo wa vitendo unaojengwa juu ya kujitolea, kujitoa mhanga na uaminifu wa dhati. Alionya kuhusu juhudi za kimakusudi za kuua roho ya uzalendo miongoni mwa Wairaqi, hadi kufikia hatua ambayo kwa baadhi yao, kuwa mzalendo kumegeuzwa kuwa kosa au fedheha.
Aliwataka wenye mamlaka kuiweka hadhi ya raia wa Iraq katika kilele cha vipaumbele, na akakumbusha kuwa ni wananchi hawa waliowafikisha katika nyadhifa za uongozi; hivyo, wajibu wa kimaadili na kitaifa unawalazimisha kuwahudumia wananchi, kupunguza mateso yao, si kuongeza tamaa, ufisadi na dhulma.
Katika hitimisho, Ayatollah Mousawi aliwakumbusha viongizi jinsi mashahidi walivyo jitoa mhanga, hususan Shahidi wa Umma, Imamu Sayyid Muhammad Baqir as-Sadr, na Shahidi wa Mihrabu, Sayyid Muhammad Baqir al-Hakim, akisema kuwa watu hawa wakubwa walijitoa wao na familia zao kwa ajili ya uhuru na heshima ya Iraq, na lau si sadaka zao, leo Wairaqi wasingekuwa wakizungumza kuhusu uhuru.
Ayatollah Mousawi alihitimisha khutba zake kwa kauli hii: “Mashahidi wetu ni viongozi wetu, na viongozi wetu ni mashahidi wetu; sisi ni wabeba fikra ya Muhammadī–‘Alawī na Shi‘a ya Ali (a.s). Hatutetemeki mbele ya dunia, na tunajitahidi ili lengo la Mwenyezi Mungu liwe tukufu na lenye ushindi.”
Maoni yako