Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatullah Haj Sheikh Ja‘far Subhani Tabrizi, mmoja wa Maraji‘ wakubwa, katika Mkutano wa Kitaifa uliokuwa na anuani isemayo “Kuinua bendera ya Tafsiri ya Qur’ani Tukufu” uliofanyika Alhamisi tarehe 11 December mjini Qum Iran, alibainisha nafasi ya Qur’ani kama muujiza wa daima aliokuja nao Mtume wa Uislamu (s.a.w.w).
Mtukufu huyo aligusia tofauti ya mazingira ya kitamaduni na fikra katika zama za Mitume waliotangulia, na akakumbushia: “Katika zama za Musa (a.s.) kulienea uchawi na mazingaombwe; katika zama za Isa (a.s.) tiba na matibabu yalikuwa maarufu; na katika zama za Utume wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) sanaa ya hotuba na balagha ilistawi, kwa hiyo, miujiza yao ilikuwa ikilingana na mahitaji ya kifikra katika zama zao.”
Akaendelea kusema: “Kwa kuwa sheria ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) ni ya kudumu milele, basi ni muujiza tu wa milele unaoweza kutekeleza jukumu lake kwa uhalisia; nao ni Qur’ani Tukufu, ambayo imewataka wanadamu na majini kuleta mfano wake, na hadi leo hakuna aliyefaulu.”
Qur’ani: Kigezo cha kupimia vitabu vyengine vya mbinguni
Marji' huyu wa taqlid, akiashira tamko “Muhayminan ‘alayh” «مُهَیْمِنًا عَلَیْهِ» katika aya ya 48 ya Surah al-Ma’idah, alibainisha: “Qur’ani Tukufu, mbali na kuuthibitisha utume wa Mitume waliotangulia, pia ina uangalizi, udhibiti na mamlaka juu ya vitabu vyao.”
Ayatullah Subhani akaendelea kusema: “Ikiwa nakala yoyote ya Torati au Injili ya leo inadai uhalisia, basi ni lazima yaliyomo yalinganishwe na Qur’ani, kwani hitilafu zilizopo katika maandishi yaliyopotoshwa zinaonekana bayana zinapolinganishwa na Qur’ani.”
Ulazima wa ubunifu katika uandishi wa tafsiri
Mtukufu huyo aliendelea kuwataka waandishi wa tafsiri wajiepushe na kurudia rudia na wajikite kwenye ubunifu, na akasema: “Kueleza kwa mdomo tafsiri ni rahisi, lakini kuandika ni jukumu kubwa. Mfasiri lazima afungue kifundo, alete hoja au nukta mpya, ili kazi yake iwe na hadhi ya kielimu na kudumu.”
Umuhimu wa kuzingatia kwa umakin na uchunguzi wa maneno ya Qur’ani
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake aliielekeza kwenye umuhimu wa kuchunguza kwa makini maneno ya Qur’ani, na akasema: “Baadhi ya maneno kama ‘Ilaahi’ hufasiriwa mara nyingine kwa maana ya ‘muabudiwa’;{معبود} ilihali katika aya nyingi maana sahihi ni ‘Mungu’. Tafsiri zisizo sahihi kama hizi zinaweza kupelekea hitilafu katika uelewa wa aya, kwa hiyo utafiti katika msamiati wa Qur’ani ni wa dharura ya kudumu.”
Maoni yako