Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafiy katika mkutano wa viongozi wa upangaji na usimamizi wa ofisi kuu na za mikoani za Hawza, uliofanyika katika ofisi ya usimamizi wa Hawza mjini Qum Iran, akirejelea khutba ya 222 ya Nahjul-Balagha inayojulikana kwa jina la Khutbat al-Dhikr, alisema:
“Mikakati yote, juhudi na mipango yetu inapaswa kuelekezwa katika kukuza na kuinua hali ya kiroho, kimaanawi na kimaadili ya nafsi zetu, pamoja na ya wanafunzi na wasomi wa Hawza; kwani lengo la mwisho ni ustawi wa kiroho katika jamii na ulimwengu mzima, jambo ambalo ndilo linalofafanua falsafa ya uwepo wa Hawza.”
Kauli ya Amirul-Mu’minin (a.s.) ndiyo mwanzo wa mazungumzo
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu aliendelea kusema: “Ili tujue njia sahihi ya shughuli za kielimu na malezi ndani ya Hawza, tunapaswa kuanza mazungumzo yetu kwa maneno ambayo yatakuwa mwongozo wetu katika njia hii yenye nuru na baraka — nayo ni khutba ya 222 katika Nahjul-Balagha inayojulikana kama Khutbat al-Dhikr — na kuhusu ubora na undani wa khutba hii, maneno mengi yamenukuliwa kutoka kwa wakubwa wa dini.”
Akaongeza kusema: “Khutba hii tukufu ilitolewa wakati wa kusomwa aya ya 37 ya Suratu An-Nur:
«رِجَالٌ لَا تُلْهِیهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَیْعٌ عَنْ ذِکْرِ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِیتَاءِ الزَّکَاةِ یَخَافُونَ یَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِیهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ»Na kwa hakika khutba hiyo ni maelezo na dhihirisho la aya hiyo ambayo inawataja wanaume ambao hawaghafiki na kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa sababu ya ya biashara.”
Tafsiri na maelezo ya Imam Ali (a.s.) kuhusu dhikri
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu nchini, akiisoma sehemu ya mwanzo ya khutba hiyo:
«إِنَّ اللَّهَ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى جَعَلَ الذِّكْرَ جِلاءً لِلْقُلُوبِ تَسْمَعُ بِهِ بَعْدَ الْوَقْرَةِ وَتُبْصِرُ بِهِ بَعْدَ الْعَشْوَةِ وَتَنْقَادُ بِهِ بَعْدَ الْمُعَانَدَةِ...»Alifafanua akisema: “Hii ni picha anayoitoa Imam Ali (a.s.) kuhusu hakika ya dhikri. Dhikri ni dhana asili na ya ndani; ni hali ya moyoni na kisaikolojia inayokabiliana na kughafilika na kusahau. Hali hii ya moyoni ikitanda ndani ya mtu, huathiri ulimi, viungo na sehemu zote za uwepo wa binadamu — katika ngazi ya mtu binafsi au kijamii.”
“Kile alichokianzisha Imam Khomeini (r.a.) na Hawza ya Qum ni nukta ya mabadiliko makubwa katika historia ya Uislamu, kwani katika kipindi chochote cha nyuma, dini na uongozi wa kielimu na kimawazo wa Hawza haujawahi kuwa katika kilele cha usimamizi na uongozi wa jamii kwa namna hii. Tukio hili ni mabadiliko makubwa ya kimkakati na mageuzi ya kistaarabu ya kimsingi yaliyotokea Qum, na leo sisi tuko katikati ya mzunguko huo.”
Athari za kiroho na kisaikolojia za dhikri kwa mtazamo wa Amirul-Mu’minin (a.s.)
Ayatullah A‘rafiy aliendelea kusema: “Katika khutba hii, zimeelezwa sifa nne za dhikri ya moyoni:
1. Mwenyezi Mungu ameifanya dhikri kuwa msafishaji wa nyoyo, kiasi kwamba husafisha na kuondoa kutu moyoni;
2. Huufanya moyo wa mwanadamu kuwa msikivu baada ya kutoelewa;
3. Huyafanya macho kuona baada ya upofu;
4. Na huifanya nafsi iliyokuwa na ukaidi kuwa laini na yenye kunyenyekea haki.”
Akasema wazi kuwa: “Hizi ni athari za kisaikolojia za dhikri. Wakati moyo wa mwanadamu unapouelewa ulimwengu wa ghaibu, hutokea tofauti kubwa ndani yake. Mwanadamu ana aina mbili za maisha: moja ni maisha ya bila dhikri, ambayo hata yakiwa ni ya juu katika manufaa ya kidunia, yanaambatana na moyo wenye kutu, masikio yasiyosikia, na macho yasiyoona; na aina ya pili ni maisha yenye dhikri, ambayo ndani yake hisia na nguvu za mtu huwekwa katika mwongozo wa nuru ya Mwenyezi Mungu.”
Aina mbili za dhikri katika maisha ya mwanadamu
Ayatullah A‘rafiy akaendelea kusema: “Tuna aina mbili za dhikri:
Ya kwanza ni dhikri ya kidunia inayohusiana na mali na mambo ya kimaada, na matokeo yake ni maisha yaliyofungwa ndani ya dunia. Na ya pili ni dhikri ya Kimungu, inayosababisha roho kupaa katika ngazi za juu zaidi. Katika hali ya kwanza, nguvu zote hujikita katika masuala ya kimaada, lakini katika dhikri ya Kimungu, moyo hupata uongozi mpya na mwanadamu huingia katika maisha matukufu (hayat tayyiba).”
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza akaendelea kusema: “Dhikri ikikaa ndani ya moyo, chemchemi za ndani ya mwanadamu huanza kutiririka, Pambizo hufunguka, masikio husikia na moyo hupata utulivu. Hii ndiyo tofauti kati ya maisha ya kimaumbile na maisha ya Kimungu;
katika maisha ya kwanza, mwanadamu hubaki katika kiwango cha manufaa ya dunia, lakini katika maisha ya pili, hupaa kutoka katika dunia ya kimaumbile hadi katika daraja la dhikri, ambalo kituo chake cha uongozi ni moyo.”
Mtume (s.a.w.) ni kielelezo kamili kwa watu wa dhikri
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akirejea sunna ya Mtume (s.a.w.w), alisema: “Imenukuliwa katika riwaya kuwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) hata katika mikutano ya kimaanawi na ya kiroho, baada ya kutoka katika kikao, alikuwa akitubia na kufanya istighfari mara ishirini hadi ishirini na tano. Hii inaonyesha kuwa hata Mtume alikuwa katika daraja la juu kabisa la dhikri, alikuwa bado anajiona mwenye haja ya kufanya istighfari.” Hivyo basi, msingi wa njia ya kimaanawi ni kuuelekeza moyo daima kwa Mwenyezi Mungu.
Kufahamu silsila ya dhikri katika historia
Ayatullah A‘rafiy, akifafanua sehemu ya pili ya khutba ya 222, aligusia mtazamo wa kijamii wa Imam Ali (a.s.) na kusema: “Bwana Mtukufu (a.s.) anasema:
«مَا بَرِحَ لِلَّهِ عَزَّتْ آلَاؤُهُ فِی الْبُرْهَةِ بَعْدَ الْبُرْهَةِ وَ فِی أَزْمَانِ الْفَتَرَاتِ عِبَادٌ نَاجَاهُمْ فِی فِکْرِهِمْ وَ کَلَّمَهُمْ فِی ذَاتِ عُقُولِهِمْ...»
Yaani, silsila ya dhikri na uongofu haijawahi kukatika duniani katika kipindi chochote. Hata katika zama za utulivu na ghaibu ya Mitume wakuu, Mwenyezi Mungu huwa na waja wake ambao huzungumza nao katika akili na fikra zao, na huwafanya kuwa wabebaji wa bendera ya dhikri Yake.”
Mkurugenzi wa Hawza akaongeza kusema: “Wabebaji hawa wa bendera ni wahuishaji wa dhikri ya Mwenyezi Mungu ambao katika kila zama wanakamilisha hoja ya Mwenyezi Mungu juu ya watu. Yeyote atakayepiga hatua katika njia hii na kujiunga na msafara huu, ana nafasi tukufu sana; na Hawza za kielimu zinapaswa zijihesabu kuwa miongoni mwa msafara huu wa wahuishaji wa dhikri.”
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alibainisha: “Kila ninaposoma khutba hii, mambo mawili hunivutia sana; kwanza, kwa sababu inatoka katika ulimi wa Amirul-Mu’minin (a.s.) ambaye ni mwaminifu wa maelezo na kiongozi wa maarifa; na pili, kwa kuwa nilisikia khutba hii kwa mara ya kwanza kutoka kwa marehemu Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari, aliyesoma kwa sauti yenye mvuto mkubwa.”
Akaongeza kusema: “Katika khutba ya 222 ya Nahjul-Balagha kuna mihimili mitatu mikuu:
1. Kwanza, dhikri ina mantiki na thamani gani;
2. Pili, wabebaji wa bendera ya dhikri wana sifa gani;
3. Tatu, nafasi yao ya kijamii ni ipi.”
Imam (a.s.) anasema:
«یُذَکِّرُونَ بِأَیَّامِ اللَّهِ وَ یُخَوِّفُونَ مَقَامَهُ بِمَنْزِلَةِ الْأَدِلَّةِ فِی الْفَلَوَاتِ»؛
Yaani, wale ambao wao wenyewe ni watu wa dhikri, huwawakumbusha wengine kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na kama waongozaji katika jangwa, huwafikisha wanadamu kwenye chemchemi ya uhai.
Mkurugenzi wa Hawza alisisitiza: “Mabadiliko ya kasi duniani pamoja na changamoto za kifikra na kitamaduni yanahitaji Hawza ziwe na basira, undani na utayari wa kushiriki katika uwanja huu. Hawza inapaswa kukusanya ngazi hizi tatu ndani yake: dhikri ya moyo, kuwa dhakiri, kisha kuwa mudhakkir – yaani kuwa waongozaji wa jamii. Wasimamizi na wapangaji wa Hawza nao lazima watambue kuwa nafasi yao ipo katika njia hii, na wasije wakaghafilika na vigezo vya Kimungu na vya malezi.” Hawza ni mwendelezo wa kihistoria wa wahuishaji wa dhikri ya Mwenyezi Mungu. Mapinduzi ya Kiislamu ni mageuzi yasiyo na mfano katika njia ya fikra ya kidini
Ayatullah Alireza A‘rafiy aliendelea na mazungumzo yake kwa kufafanua mtazamo wa kihistoria wa Hawza na nafasi yake ya sasa katika ustaarabu wa Kiislamu, akasema:
“Tunapotazama historia ya zaidi ya miaka elfu moja ya Hawza, tunashuhudia kupanda na kushuka kwingi, lakini kwa jumla mteremko wa harakati za kijamii na kisiasa za Hawza umekuwa wa maendeleo na kuinuka.”
Nafasi ya maulamaa katika mabadiliko ya kijamii na kisiasa
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akirejea mchango wa harakati za kielimu na kishia katika historia, aliongeza kusema: “Baada ya zama za uwepo wa Maimamu Ma‘sumin (a.s.), harakati mbalimbali za Aalawiyyah na za kielimu kama vile Waidrisiyyun, Aalawiyyun wa Tabaristān, Wafatimiyyun katika kaskazini mwa Afrika, Al-Buwaihiyun katika Iran na Iraq, pamoja na Wasarbadaariyyun na baadaye Safawiyyah, zote ziliendelea katika njia ya nguvu za Kimungu na zikiwa zimeungana na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.). Katika harakati hizi zote, maulamaa na wanazuoni wakubwa ima walikuwa mstari wa mbele, au walikuwa wachezaji wa nyuma wenye nafasi ya kiungo na mikakati.”
Akaendelea kusema: “Katika haya, kuna vipindi viwili vya kihistoria vilivyo mashuhuri zaidi: kimoja ni zama za Wamongolia, na kingine ni kipindi cha Safawiyyah. Vipindi hivi viwili vilikuwa na nafasi muhimu sana katika kuunda ustaarabu wa kielimu na kidini wa Kishia. Katika zama hizi, wanazuoni wakubwa kama Allamah Hilli, Khwajah Nasiruddin Tusi, na Muhaqqiq Karaki walikuwa na mchango wa kipekee, iwe katika nyanja za maendeleo ya kielimu au katika mageuzi ya kijamii na kisiasa.”
Maoni yako