Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Tareh 11 Oktoba 2025 Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, alihudhuria hafla fupi ya utangulizi wa maadhimisho wa Maulid iliyoandaliwa na Jumuiya ya Vijana na Wanafunzi wa Dhehebu la Shia Ith’naashariyyah Tanzania (TIMSYA), mkoani Arusha.
Hafla hiyo imefanyika kwa lengo la kuashiria mwanzo wa shughuli za maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), ambapo vijana wa TIMSYA wameonyesha hamasa kubwa katika maandalizi ya tukio hilo muhimu kwa Waislamu duniani kote.
Katika hotuba yake, Sheikh Jalala amewapongeza vijana wa TIMSYA kwa jitihada zao za kuandaa hafla hiyo, akisisitiza umuhimu wa umoja, elimu ya dini, na kushikamana na mafundisho sahihi ya Uislamu kama urithi wa Mtume (saww). Aidha, amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kueneza amani, upendo na maadili mema katika jamii.
Viongozi mbalimbali wa kidini kutoka ndani na nje ya Arusha walihudhuria hafla hiyo, wakiwemo masheikh, walimu wa dini, na wawakilishi wa taasisi za Kiislamu. Ushirikiano huo umeonesha dhamira ya pamoja ya kukuza mshikamano na kuendeleza maadhimisho ya kidini kwa njia yenye manufaa kwa jamii.
Maadhimisho kamili ya Maulid yanatarajiwa kufanyika siku za usoni, ambapo shughuli mbalimbali za kielimu, kiroho na kijamii zimepangwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini, yakihusisha mihadhara, nasaha za viongozi wa dini na dua za pamoja.
Maoni yako