Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, kabla ya adhuhuri ya leo, katika kongamano la kumbukumbu ya Mirza Na’ini, alisema: Kufufua kumbukumbu ya wanazuoni wapiganaji ni kufufua uhai wa kielimu, kimaadili na kistaarabu wa Hawza.
Akaongeza: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ametukusanya tena katika mkutano huu wenye nuru, ili tumheshimu mwanazuoni mkubwa na shakhsia tukufu, moja ya mishumaa inayong’aa ya hawza, marehemu Mirza Muhammad Husayn Na’ini (ra).
Vilevile, aliwakaribisha wageni na wahudhuriaji wa ndani na nje ya nchi katika kongamano hilo, akisema: Natoa shukrani za dhati kwa wageni wote waheshimiwa kutoka Iran na nchi mbalimbali waliohudhuria mkusanyiko huu wa kielimu na kima’arifa. Natoa pia shukurani kwa wanazuoni wakubwa, wahadhiri wakuu, wawakilishi wa nyumba za Maraji‘ wakubwa wa Taqlid, Nyumba Tukufu ya Imam Khomeini (ra), Nyumba Tukufu ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi (Mola amuhifadhi), pamoja na Mwenyekiti na wajumbe wa Jumuia ya Walimu wa Hawza ya Qum, na Katibu na wajumbe wa Baraza Kuu la Vyuo vya Kidini waliohudhuria katika hafla hii.
Mjumbe wa Baraza Kuu hawza aliongeza: Nawashukuru pia wakurugenzi wa vyuo vya kidini kote Iran na ulimwenguni — kutoka Mashhad, Isfahan, Najaf Ashraf na miji mingine ya Kiislamu — kwa kushiriki katika mkutano huu wenye nuru. Tunaheshimu pia uwepo wa wawakilishi wa Atabat ‘Aliyyat na nyumba tukufu ya Ayatullah al-Udhma Sayyid Sistani. Uwepo wenu wote ni wenye thamani kubwa na wa heshima kwetu.
Aidha, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah A‘rafi aliwashukuru waandaaji wa kongamano hilo, akisema: Natoa shukrani kwa Katibu wa Baraza la Sera, kwa watafiti na waandaaji wa kongamano hili, kwa waandishi na washirika wa utekelezaji waliotoa juhudi kubwa katika kuandaa hafla hii ya kimataifa na kielimu. Vivyo hivyo, nawashukuru wanahabari na vyombo vya habari vya kitaifa vilivyojitahidi katika kutangaza na kueneza habari za tukio hili.
Mirza Na’ini — Kituo cha Mizania Kati ya Jadi na Ubunifu katika Fikra ya Kiislamu
Mjumbe wa Baraza Kuu la hawza alifafanua sifa za shule ya fikra ya Mirza Na’ini, akisema: Mwenendo wa kielimu wa Mirza Na’ini una sifa kadhaa mashuhuri. Kwanza, alikuwa na uhusiano wa kina na urithi wa kielimu wa ijtihadi wa kale; alidumu juu ya njia madhubuti ya ijtihadi ya kihistoria ya hawza, bila kuondoka hata kidogo kutoka katika misingi asili ya ijtihadi. Pili, pamoja na kushikamana na jadi, alikuwa mwenye ubunifu, uvumbuzi na ijtihadi hai — kiasi kwamba anachukuliwa kuwa moja ya nukta za mageuzi katika historia ya elimu ya usul na elimu za Kiislamu.
Alibainisha zaidi: Marehemu Mirza Na’ini alikuwa kielelezo cha namna ya kushughulikia masuala mapya. Aliweza, huku akiwa mwaminifu kwa asili ya kielimu ya Hawza, kufungua upeo mpya katika uelewa wa dini, fiqhi ya kijamii, na uhusiano kati ya dini na siasa. Kwa akili yake ya kiijtihadi, hasa kupitia kitabu chake mashuhuri “Tanbīh al-Ummah wa Tanzīh al-Millah”, alitoa mchango muhimu sana katika kubainisha fikra ya Kiislamu yenye mwelekeo wa uadilifu, uhuru, na uwajibikaji wa kijamii.
Ulazima wa Kuendeleza Njia na Mbinu ya Kielimu ya Mirza Na’ini
Ayatullah A‘rafi alisisitiza umuhimu wa kuendeleza njia ya kielimu na kifikra ya Mirza Na’ini, akisema: Vyuo vya kidini vinapaswa kusoma upya urithi wa wakubwa hawa kwa lugha ya kisasa, na kwa kufuata mbinu ya ijtihadi, viunganishe asili na mageuzi ya zama hizi. Mustakabali wa Hawza na umma wa Kiislamu uko mikononi mwa usomaji na ujenzi upya wa kiakili kama huu — usomaji unaoangaza njia ya ustawi wa jamii kwa mwanga wa akili ya kidini na ijtihadi hai.
Mkurugenzi wa Vyuo vya Kidini nchini Iran aliongeza: Marehemu Mirza Na’ini, akiwa mwaminifu kwa jadi na mwenye ufahamu wa mabadiliko mapya, alikuwa mfano bora wa mizania na mtazamo wa kina katika fikra ya Kiislamu. Katika kushughulikia masuala mapya, hakuwahi kuachana na misingi ya asili ya ijtihadi, na wakati huohuo hakupuuzia masuala ya kisasa. Hii ndiyo nukta angavu katika mwenendo wa kielimu wa Mirza Na’ini — ile inayoitwa kwa usahihi “kuunganisha asili na uhalisia wa kisasa” (الجمع بین الأصالة والمعاصرة).
Ayatullah A‘rafi alisema kwa kusisitiza kwamba Mirza Na’ini, sambamba na uaminifu wake kwa sunna za kielimu za Hawza, aliendeleza ubunifu na ujenzi wa nadharia katika ngazi za juu, akiongeza: Katika nyanja zote za kielimu — kuanzia fiqhi na usul, hadi masuala ya kalamu na falsafa — alikuwa na uelewa wa kina wa sunnah ya kielimu ya kale, huku akiwa na mtazamo wa mbali wa kimaendeleo.
Marehemu Mirza Na’ini hakuvuka mipaka yoyote katika misingi ya kiakida na kimantiki ya Shia, bali kwa kutumia hazina hiyo halisi na yenye kina, alikuwa mbunifu, mvumbuzi na mwenye kutoa nadharia mpya.
Sifa hii kuu ndiyo iliyomfanya atambulike katika historia ya Hawza kama kitovu cha kipimo kati ya kuhifadhi sunnah na kujibu mahitaji ya zama.
Mirza Na’ini — Mzani kati ya Wenye Kushikamana na sunnah na Wenye Kuvutiwa na mapya
Ayatullah A‘rafi aliongeza: Katika ulimwengu wa Kiislamu, wapo wanaoendelea kubakia katika jadi bila kuangalia masuala mapya, na wapo wanaoingia katika masuala mapya lakini wakipuuza mbinu asilia za ijtihadi; ilhali Mirza Na’ini alisimama katikati ya uwiano huu. Alikuwa mwaminifu kwenye urithi wa kielimu wa Hawza, na wakati huohuo alikuwa mwenye kujibu changamoto mpya za kifikra na kijamii.
Umakini Mkubwa wa Mirza Na’ini katika Masuala ya Kifiqhi na Fatwa
Mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum, akigusia kazi zilizochapishwa za faqihi huyu mkubwa, alisema: Katika mkusanyo wa juzuu 40, ulioandaliwa kwa juhudi za wakubwa wa Hawza na utakaozinduliwa leo, tunaona kuwa marehemu Na’ini katika sehemu ya maswali ya kifiqhi na fatwa, alikuwa mujtahid wa kisasa, makini, na mwenye kujibu ipasavyo masuala mapya ya zama zake; huku akitembea juu ya njia sahihi na imara ya kielimu na ijtihadi.
Nafasi ya Mirza Na’ini katika Mageuzi ya Elimu ya Usul
Mkurugenzi wa vyuo vya kidini alibainisha: Elimu ya Usul ilipiga hatua kubwa ya maendeleo mikononi mwa Na’ini. Pamoja na ubunifu wa wahakiki wakubwa kama Wahid Bahbahani, Shaykh al-A‘zam Ansari, na Akhund Khurasani, Usul katika zama za Na’ini ulipevuka na kuwa mfumo wa kielimu ulio kamili na wenye kina. Usul ya marehemu Na’ini ina utaratibu mzuri, utafiti makini, tafsiri mpya na ufafanuzi wa kisasa. Ndani ya mfumo wake wa kielimu, mbali na kanuni za istinbath (kuchimbua hukumu), upo pia uchambuzi wa kimantiki, kifalsafa, na hata kiisimu, vinavyowezesha ufahamu mpya wa Qur’ani na Sunna.
Akaongeza: Katika elimu ya Usul ya marehemu Na’ini, hakuna jambo la juu juu. Hakupita juu ya jambo lolote kwa urahisi. Kila mjadala wake una kina na unachunguza hadi mizizi ya dhana. Hata hivyo, katika uchambuzi wake alikuwa anazingatia utamaduni wa lugha ya watu na muktadha wa maandiko. Mirza Na’ini aliweza kuunganisha kati ya kina cha kielimu na mtazamo wa kimantiki wa kawaida, jambo ambalo ni moja ya sifa kuu za mbinu yake.
Mageuzi ya Msingi katika Mfumo wa Ijtihadi
Ayatullah A‘rafi alisisitiza kuwa mfumo wa Usul wa Na’ini ulileta mapinduzi ya msingi katika mfumo wa ijtihadi, akasema: Mfumo huu wa kielimu ulienea kwa kasi huko Najaf na kisha katika vyuo vingine vya kidini, na ukawa sababu ya kustawi elimu kwa wanafunzi na mafaqihi wengi waliokuja baada yake. Marehemu Allamah Na’ini alikuwa na kumbukumbu yenye nguvu, akili kali, na kipawa cha kipekee. Alikuwa na usemi fasaha, kalamu thabiti, uhodari wa Kifarsi na Kiarabu, na uwezo mkubwa wa kufundisha na kulea wanafunzi.
Akizungumzia nafasi ya wanafunzi wa shule ya Na’ini, alisema: Kutoka katika shule yake ya fiqhi na usul walitoka wanafunzi na waandishi mashuhuri waliotumikia kwa baraka za Mwenyezi Mungu katika kueneza fikra zake katika vyuo vya Najaf, Qum, na vituo vingine vya kielimu. Wanafunzi hawa walifafanua na kukuza mawazo yake, na wakaunda harakati ya kielimu na kifikra katika ulimwengu wa Kishia.
Mirza Na’ini — Mwanazuoni wa Kisiasa na Mjenzi wa Fikra za Kiustaarabu
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi (Majlis Khobregān) aliongeza: Pamoja na sifa zote za kielimu, ukamilifu, wepesi wa fikra na ufasaha wa Na’ini — kama alivyonukuliwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu — yeye ni mwenye shule ya fikra ya kisiasa na msomi wa fikra za ustaarabu katika zama za kisasa. Aliishi katika kipindi kigumu sana, lakini kwa ujasiri wa kielimu na umakini wa kidini. Ni kipindi ambacho ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa ukikabiliana na changamoto kubwa za ukoloni, udikteta, na mgogoro wa utambulisho.
Kushikamana na Sunnah na Harakati ya Ubunifu
Ayatullah A‘rafi alihitimisha kwa kusema: Marehemu Mirza Na’ini, kwa akili yake ya ijtihadi, alitufundisha kwamba; mtu anaweza kuwa mwaminifu kwa sunnah za dini na wakati huohuo kuwa mbunifu na mwenye kujibu mahitaji ya zama. Kwa kulinda misingi ya dini na kuelewa kwa kina mahitaji ya wakati, alionesha njia ya uwiano wa kweli kati ya uaminifu kwa jadi na majibu ya kimujitahidi kwenye changamoto za kisasa.
Yeye ni mfano wa mwanazuoni kamili, mwenye fikra za mageuzi, na faqihi aliyeunda zama — kielelezo ambacho hawza zinapaswa kurejelea zaidi, na kufufua fikra zake katika safari ya maendeleo ya kifikra na kistaarabu ya umma wa Kiislamu.
Ayatullah A‘rafi, akiyachambua mazingira ya kihistoria na kijamii ya zama za marehemu Mirza Muhammad Husayn Na’ini, alisema: Marehemu Na’ini aliishi katika nusu ya pili ya karne ya kumi na tisa na nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. Kipindi hicho kilikuwa ni zama ambazo dunia ilikabiliwa na mageuzi makubwa ya kifikra, kifalsafa, kijamii na kisiasa. Ingawa baadhi ya mageuzi hayo yalikuwa mbali na ulimwengu wa Kiislamu, athari zake zilifika pia katika nchi za Waislamu. Vita vya Kwanza vya Dunia vilibadilisha kwa kiasi kikubwa mizani ya nguvu duniani, na ulimwengu wa Kiislamu haukuachwa bila kuguswa na matokeo yake.
Mirza Na’ini — Shujaa wa Zama Zake
Ayatullah A‘rafi akiashiria mazingira ya kiakili ya kipindi hicho, alisema: Katika zama hizo, kwa upande mmoja, kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kielimu na kifikra, na kwa upande mwingine, ukoloni na uvamizi wa madola ya Magharibi katika ardhi za Kiislamu. Mvumo wa fikra na mafundisho ya kigeni ulienea katika ulimwengu wa Kiislamu. Katika mazingira haya, marehemu Na’ini, akiwa katika pembe za Samarra na Najaf, hakubakia amejitenga na dunia; bali aliifahamu kwa mapana upeo wa ulimwengu na akajishughulisha na uchambuzi wa masuala mapya. Alikuwa na mizizi imara katika misingi ya ijtihadi, lakini wakati huo huo alikuwa mtu wa zama zake, mwenye uelewa wa kina wa mwenendo wa kifikra na kijamii wa wakati wake.
Akaongeza: Marehemu Na’ini alikuwa kinara wa elimu, mbeba bendera wa mageuzi na mtengenezaji wa mwelekeo wa kielimu. Katika fikra ya kisiasa ya Kiislamu pia alianzisha shule ya fikra. Kama alivyonukuliwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mirza Na’ini ni mfano bora wa ubunifu na tafakuri katika masuala mapya ya siasa na uongozi. Alishiriki mashindano ya kielimu na kifikra na wasomi wakubwa wa zama zake, kama vile Isfahani na wanazuoni wengine wa Hawza ya Najaf, akidhihirisha ubunifu na upeo mpana wa kielimu.
Ubunifu wa Kielimu wa Mirza Na’ini
Ayatullah A‘rafi aliongeza kuwa: Ubunifu wa marehemu Na’ini katika nyanja mbalimbali — kuanzia usul na fiqhi hadi katika masuala ya kijamii, istilahi, hoja na hukumu — ulileta mageuzi makubwa ambayo ni nadra katika historia ya elimu ya usul. Fikra za Na’ini, baada ya fikra za marehemu Akhund Khurasani, zilisambaa katika vyuo vya kidini na kupata wafuasi na wakosoaji wengi. Imam Khomeini (r.a), licha ya kumheshimu sana Na’ini, mara nyingi alichambua na kukosoa baadhi ya maoni yake — jambo linaloonesha ukubwa wa nafasi yake ya kielimu.
Akaendelea: Hata leo, katika Hawza ya Najaf na vituo vingine vya kielimu, “dars-e kharij” (masomo ya juu ya fiqhi na usul) ya Na’ini hufundishwa kila wiki, na ni nadra kikao cha kielimu kupita bila kutajwa au kuchambuliwa kwa mitazamo na hoja za Na’ini. Hili linatia moyo wanafunzi na walimu vijana hapa Qum, Najaf, na vyuo vingine vya Kiislamu, na linadhihirisha umuhimu wa kumtambua upya mtu huyu na upeo wa fikra zake. Mirza Na’ini ni kama jua linalong’aa katika anga la fikra za Kiislamu, na kunufaika na fikra zake ni jambo muhimu kwa sasa na siku zijazo.
Maisha na Mtazamo wa Na’ini — Ya Kiuchambuzi na Yenye Uelekeo wa Kutatua Masuala
Ayatullah A‘rafi aliendelea kusema: Marehemu Na’ini aliishi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia — kipindi ambacho ulimwengu wa Kiislamu ulitawanyika na athari za ukoloni wa Magharibi zilikuwa dhahiri. Alizifahamu na kuzichambua fikra na siasa za Magharibi katika karne ya kumi na tisa na ishirini. Wakati huo huo, alitambua hatari za ukoloni na uvamizi wa fikra za kigeni, na akaelewa nafasi ya ulimwengu wa Kiislamu katika kipindi hicho. Na’ini alikabiliana na migongano na changamoto hizo akiwa mchambuzi, mwenye mwongozo na muelimishaji. Aliweza kuweka wazi misingi ya kifiqhi na kisiasa ya Uislamu kwa namna iliyoelezea majibu ya changamoto mpya.
Na’ini — Kiongozi wa Kielimu, Kijamii na Kisiasa
Akionyesha heshima kwa nafasi ya juu ya Mirza Na’ini katika uwanja wa siasa na jamii, alisema: Mwanazuoni huyu mkubwa na marja‘ mtukufu, awe alipokuwa pamoja na Mirza Shirazi, au alipokuwa karibu na Akhund Khurasani, au alipokuwa mwenyewe katika nafasi ya marja‘, daima alikuwa na uchungu kwa ulimwengu wa Kiislamu na kwa mataifa ya Iran na Iraq. Alitambua kwa undani masuala ya zama zake na hakuwahi kukwepa changamoto au hatari. Katika hatua zote za maisha yake, alishiriki kikamilifu katika medani za uongozi wa fikra na ushawishi, akitoa mfano wa fikra za kisiasa na kisheria zilizojengeka juu ya ufahamu wa wakati na uaminifu kwa misingi ya Kiislamu.
Mshauri wa Fikra wa Mirza Shirazi na Nguzo ya Akhund Khurasani
Ayatullah A‘rafi aliongeza: Na’ini alikuwa mshiriki hai na mwenye ushawishi mkubwa katika harakati na mapambano makubwa ya Iran na Iraq. Iwe akiwa karibu na Mirza Shirazi, au akiwa pamoja na Akhund Khurasani, au katika kipindi cha uongozi wake wa marja‘iyya, alibaki kuwa mtu wa mstari wa mbele katika harakati za kielimu na kijamii. Nusu karne ya uwepo wake katika Iran na Iraq, na juhudi zake katika nchi hizo mbili, ni jambo lenye thamani kubwa — na hadi leo, maisha yake ni kielelezo bora kwa wanafunzi na watafiti wa kielimu.
Ayatullah A‘rafi aliendelea kusema: Katika ujana na ubarobaro wake, Na’ini aliaminiwa sana na Mirza Shirazi. Alishiriki katika maamuzi na hatua za kisiasa za Mirza Shirazi, na maoni yake yalikuwa na ushawishi mkubwa. Uaminifu na ushawishi huu, kabla ya Na’ini kufikia nafasi za kijamii au marja‘iyya, ulionesha nafasi yake ya kielimu na kifikra miongoni mwa wafuasi wakuu wa wakati huo.
Na’ini ndani ya Najaf na Karibu na Akhund Khurasani
Ayatullah A‘rafi alisema: Baada ya kuhamia Najaf, marehemu Na’ini aliungana na Akhund Khurasani. Ingawa uhusiano wa kawaida wa mwanafunzi na mwalimu haukuwa wa kawaida kabisa, uaminifu wa Akhund Khurasani kwake ulikuwa dhahiri. Taarifa nyingi za kisiasa, matamko muhimu na maamuzi ya kijamii ya Najaf wakati huo yalitokana na ushauri wa Na’ini na mtazamo wake.
Kazi Muhimu ya Na’ini katika Mapambano Dhidi ya Ukoloni
Akaendelea: Na’ini alikuwa kiongozi na kielekezo muhimu katika mapambano ya Iraq dhidi ya utawala wa Kiingereza. Alikuwa na ushawishi mkubwa katika kuongoza harakati za wananchi na kisiasa, hadi pale walipopinduliwa kwenda Qum kama matokeo ya moja kwa moja ya shughuli zake. Mtindo huu wa Mirza Na’ini unaunganisha elimu, ufahamu wa kisiasa, ujasiri na uwajibikaji wa kijamii, na unaonesha dhana yake ya kina kuhusu maslahi ya Uislamu na mataifa ya eneo.
Ayatullah A‘rafi alisema: Imam Khomeini (r.a) katika historia ya karne ya ishirini alileta mapinduzi makubwa, ambapo uelewa wa mashujaa wa taifa la Iran na harakati za mageuzi za Hawza vilitokea kwa mfano wa kipekee katika miaka elfu moja iliyopita. Hali za kisaikolojia kutoka Baghdad na enzi za Mongol hadi harakati za Mashurutiyya zilikuwa na mteremko na kupanda, lakini wakati wa Imam, mabadiliko makuu yalitokea katika Uislamu na taifa la Iran.
Umuhimu wa Historia ya Hawza
Ayatullah A‘rafi alibainisha: Leo, Hawza zinapaswa kuwa chachu ya motisha kwa wanafunzi na walimu, kwa kuchunguza historia ya kina ya shughuli za kielimu na kijamii na kuitumia kujibu changamoto za sasa. Watu wakubwa kama Mirza Na’ini na Akhund Khurasani, tofauti na baadhi ya waliotangulia, waliweza kuingia kikamilifu katika siasa za Najaf na kutoa ushauri wa kuongoza.
Kujifunza kutoka Mafanikio na Makosa ya Zamani
Aliongeza kusema: Ni lazima tuchambue mafanikio na pia kushindwa. Harakati za Mashurutiyya zilitoa funzo kubwa; kuanzia mapambano ya aina fulani hadi juhudi za kuondoa ukoloni na utawala wa kifahari. Wanazuoni wa dini daima wamekuwa mstari wa mbele pamoja na taifa la Iran. Imam mkubwa alitumia uchambuzi wa kina wa harakati za zamani — kuanzia harakati za tumbaku na Mashurutiyya hadi harakati za mafuta — kuunda mfumo mpya ambapo marja‘iyya na wilaya ni kiini.
Na’ini — Kiongozi wa Kielimu, Kijamii na Kisiasa
Ayatullah A‘rafi alisema: Mbali na sifa zake za kielimu, Mirza Na’ini alikuwa ni shujaa wa kijamii na kisiasa. Heshima yake ya kiroho, nafsi na maadili bado haijatambuliwa kikamilifu na jamii. Leo zaidi ya wakati mwingine wowote, tunahitaji viongozi wa maadili na kiroho, ambapo Na’ini yuko mstari wa mbele kati yao.
Maoni yako