Jumatano 15 Oktoba 2025 - 14:08
Mwanasiasa Nguli Nchini Kenya Afariki Dunia Akiwa Nchini India

Hawza/ Mwanasiasa mashuhuri wa Kenya na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, Raila Amolo Odinga, amefariki dunia leo hii tareh 15 Oktoba 2025 akiwa nchini India ambako alikuwa akipokea matibabu. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Hospitali ya Devamatha, iliyoko jimbo la Kerala, marehemu alipoteza maisha baada ya kupata mshtuko wa moyo (cardiac arrest).

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Raila Odinga alifariki majira ya asubuhi baada ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake kushindikana. Taarifa hizo ziliidhinishwa pia na familia yake kupitia msemaji wake, Bi. Winnie Odinga, aliyesema marehemu alikuwa akipata tiba ya kiafya ya jadi (Ayurvedic treatment) kwa siku kadhaa kabla ya tukio hilo.

Historia ya kisiasa

Raila Odinga, ambaye alizaliwa tarehe 7 Januari 1945, alikuwa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya Kenya.
Alihudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya kati ya mwaka 2008 na 2013 chini ya serikali ya muungano wa kitaifa iliyoundwa baada ya machafuko ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Katika safari yake ndefu ya kisiasa, Raila aligombea urais mara tano lakini hakuwahi kufanikiwa kushinda kiti hicho licha ya kuungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi. Wengi wamekuwa wakimtambua kama sauti ya demokrasia, mageuzi na haki za wananchi nchini humo.

Mchango na misimamo ya kimataifa

Mbali na siasa za ndani, Raila Odinga alijitokeza mara nyingi kama mtetezi wa haki za binadamu duniani, hususan kwa watu wa Palestina.

Katika matamko yake kadhaa hadharani, aliwahi kulaani ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina, akisisitiza kwamba “Afrika haiwezi kunyamaza mbele ya mateso ya watu wanaonyimwa uhuru wao.”

Mnamo mwaka 2021, Raila aliongoza maandamano ya amani jijini Nairobi kushinikiza jumuiya ya kimataifa kulinda raia wa Ghaza, huku akisisitiza kuwa ukombozi wa Palestina ni suala la haki na utu wa binadamu, si la dini wala siasa.
Msimamo huo ulimfanya aheshimiwe si tu katika ukanda wa Afrika Mashariki, bali pia na wanaharakati wa kimataifa wanaotetea amani na usawa.

Mchango wake kwa taifa

Marehemu Raila Odinga alitambulika kwa juhudi zake katika kupigania katiba mpya ya Kenya iliyopitishwa mwaka 2010, pamoja na kupigania utawala bora, uwajibikaji wa viongozi, na usawa wa kijamii.
Aidha, alikuwa kiungo muhimu katika juhudi za kuleta maridhiano ya kisiasa kupitia mazungumzo na serikali zilizopita, ikiwemo makubaliano ya kisiasa (handshake) na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2018, na baadaye ushirikiano wa kisiasa na Rais William Ruto mwaka 2025.

Hisia za majonzi na rambirambi

Taarifa za kifo chake zimeutikisa ulimwengu wa kisiasa nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla.
Viongozi mbalimbali wa Afrika Mashariki, akiwemo Rais William Ruto, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, wametoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na wananchi wa Kenya.

Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) aliandika:

“Kenya imepoteza mwanasiasa mkomavu na mzalendo wa kweli. Raila Odinga alikuwa nguzo muhimu katika historia ya taifa letu. Tutaendelea kumkumbuka kwa ujasiri, uvumilivu na mapambano yake kwa haki.”

Urithi wake

Raila Odinga ataendelea kukumbukwa kama nguzo ya mageuzi ya kisiasa nchini Kenya, mpiganiaji wa demokrasia na mwanasiasa aliyekuwa tayari kushirikiana na wapinzani wake kwa maslahi ya taifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka familia yake, mipango ya mazishi inafanyika, na ratiba kamili ya shughuli hizo itatangazwa baada ya ushauri na serikali ya Kenya.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha