Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, mauaji ya kimbari yanayofanywa Ghaza na Israel, pamoja na ukatili usio na mipaka wa utawala huo dhalimu, vimewasukuma watu huru na wanaotetea utu wa kibinadamu kote duniani kuinuka na kupaza sauti za upinzani. Miongoni mwa vielelezo vya wazi vya hali hii ni maandamano makubwa ya hivi karibuni yaliyofanyika nchini Hispania na Italia.
Vyombo vya habari navyo vimekuwa vikiunga mkono harakati hizi kwa kuonesha picha na matukio yanayoakisi hasira na ukali wa wapinzani wa jinai hizo. Nchini Marekani, licha ya ukandamizaji mkali, kukamatwa na kufungwa kwa wanaharakati, vuguvugu la wapigania haki za Wapalestina limeendelea kukua, na idadi ya waandamanaji imezidi kuongezeka siku baada ya siku.
Hata katika miezi ya mwanzo ya mauaji haya ya kimbari, maelfu ya Wayahudi kote ulimwenguni walishiriki kwenye maandamano haya, wakilaani mauaji na uhalifu wa utawala wa Kizayuni, huku wakijitenga wazi na matendo hayo kwa niaba ya dini ya Uyahudi. Walisema wazi kwamba wanapinga kwa ukali uhalifu huu na kwamba mauaji hayo hayana uhusiano wowote na mafundisho ya dini yao.
Mwezi wa Machi mwaka 2024, wanafunzi wanaopinga sera za Israel na watetezi wa haki za binadamu kwwnye chuo kikuu cha Columbia (Marekani) waliweka kambi ya muda katika uwanja wa chuo hicho na kuifanya kuwa kituo cha shughuli zao za kupinga uhalifu wa Israel. Kambi hiyo ilipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vingine pia. Kwa masikitiko, serikali ya Trump iliizikandamiza harakati hizo kwa nguvu, ikiwatuhumu wanafunzi hao kuwa “wapinga Uyahudi.”
Nchini Uingereza, polisi wa miji mikuu tayari wamewakamata zaidi ya watu 1,900 waliokuwa wakishiriki maandamano ya kuunga mkono haki za Wapalestina na kupinga uhalifu wa Israel.
Hali kama hiyo — na hata mbaya zaidi ya hiyo — imeshuhudiwa kwenye mataifa mengine pia. Wafuasi wa Palestina nchini Ujerumani, Italia, Hispania, Norway, Sweden, na nchi kadhaa za Afrika wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo makubwa ya kimataifa.
Chanzo: The Guardian
Maoni yako