Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Katika ziara hiyo, Sheikh Jalala alipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma, Ndugu Hassan Rugwa, ambapo walifanya mazungumzo yenye lengo la kuimarisha uhusiano na kuelezea malengo ya ziara yake. Pia alitoa historia fupi ya namna Ushi’a ulivyoingia nchini Tanzania na shughuli kuu za Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC).
Historia Fupi ya Ushi’a Nchini Tanzania
Sheikh Jalala katika ziara hiyo alieleza kuwa: Ushi’a ulianza kuingia nchini karne ya 17 kupitia Washirazi, hili linadhihirishwa na mchango wa Afro-Shirazi Party, chama kilichosaidia kupigania uhuru.
Kundi la pili lilikuwa ni la Makhoja, waliowasili nchini karne ya 19, Kuanzia mwaka 1955, mafundisho ya Ushi’a yalianza kuenea nje ya jumuiya hizo, na Waafrika wazawa walianza kujifunza itikadi ya Kishia.
Mwaka 1968, kundi la kwanza la Mashia wazawa lilipelekwa nje ya nchi kwa ajili ya masomo ya dini. Waliporejea, waliunda Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) kama mwamvuli wa kuunganisha Mashia wote nchini.
Jumuiya hiyo ilisajiliwa rasmi mwaka 1992, ikiendelea kufanya kazi zake hadi leo.
Shughuli Kuu za Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC)
Sheikh Jalala katika kikao hicho alibainisha pia baadhi ya shughuli mbali mbali ambazo husimamiwa na Jumuiya hiyo ya Mashia zikiwemo:
1. Kujenga na kudumisha mahusiano mazuri miongoni mwa Mashia nchini, kama mwamvuli wa Mashia wote mbele ya Serikali.
2. Kukuza uhusiano mwema na ndugu wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.
3. Kuimarisha mahusiano na Wakristo kwa misingi ya kuheshimiana na kuishi kwa amani.
4. Kuimarisha ushirikiano na Serikali katika masuala mbalimbali ya kijamii na kidini.
5. Kuhubiri amani, umoja na mahusiano mema kati ya Watanzania wote bila kujali tofauti za dini au kabila.
Ziara ya Sheikh Jalala mkoani Kigoma ni sehemu ya juhudi endelevu za Jumuiya ya Shia Tanzania katika kuimarisha umoja wa kitaifa, kujenga mashirikiano ya kidini na kijamii, na kueneza ujumbe wa amani kwa Watanzania wote.
Maoni yako