Jumanne 14 Oktoba 2025 - 20:55
Irani yaicharaza Tanzania Bakora 2 - 0 Bila ya Huruma

Hawza/ Mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya taifa ya irani na tanzania umechezwa leo katika uwanja wa Rashid Stadium uliopo Mjini Dubai, falme za kiarabu (UAE), ambapo wenyeji Irani wameibuka na ushindi wa goli mbili kwa bila dhidi ya Taifa stars ya Tanzania.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza Katika mtanange huo uliokuwa na ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha kwanza, irani ilianza mchezo kwa kasi na kujihakikishia ushindi mapema kupitia magoli mawili ya kipindi hicho.

Goli la kwanza la Irani lilifungwa dakika ya 17 kwa njia ya penalti, baada ya mchezaji wa safu ya ulinzi wa Tanzania kufanya kosa ndani ya eneo la hatari. Mshambuliaji Amir Huseinzadeh alisimama nyuma ya mpira na kutupia wavuni kwa ustadi mkubwa, akiipa Irani uongozi wa bao moja kwa sifuri.

Dakika tisa baadaye, yaani dakika ya 26, Irani iliongeza bao la pili kupitia kwa Mohamad Mohebi, ambaye alipokea pasi murua na kumalizia kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Tanzania bila majibu.

Magoli yote mawili yalipatikana ndani ya kipindi cha kwanza, na kipindi cha pili kilishuhudia timu zote zikicheza kwa tahadhari zaidi. Tanzania ilionekana kubadilika kidogo baada ya mapumziko, ikijaribu kushambulia kwa kupitia pembeni, lakini haikuweza kuvunja ukuta wa ulinzi wa Irani uliokuwa imara muda wote wa mchezo.

Kwa ujumla, Irani ilitawala mchezo kwa asilimia kubwa ya umiliki wa mpira na nidhamu ya kiuchezaji, huku Tanzania ikionyesha dalili nzuri za kupambana lakini ikikosa ufanisi katika eneo la mwisho la ushambuliaji.

Matokeo haya yanaiweka Irani katika nafasi nzuri ya kujiandaa kwa mashindano yajayo ya kimataifa, huku kwa upande wa Tanzania, mchezo huu unatoa nafasi muhimu kwa benchi la ufundi kutathmini kikosi na kuboresha mbinu kuelekea mechi zijazo za ushindani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha