Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, waandaaji wa maandamano hayo walikadiria idadi ya washiriki kufikia watu 600,000, huku takwimu za polisi na halmashauri ya jiji zikionesha zaidi ya watu 500,000 walishiriki katika mjumuiko huo mkubwa wa kuiunga mkono Palestina.
Ben Jamal, mkurugenzi wa kampeni ya mshikamano na Palestina, alisema: “Mpango uliotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump, si suluhisho la kudumu wala halisi kwa amani, bali ni mpango wa muda mfupi usioangalia mizizi halisi ya jinai hizi.”
Akaendelea kueleza kuwa maandamano na upinzani vitaendelea hadi pale mauaji ya kimbari na vita Ghaza vitakapositishwa kabisa na usitishaji wa kudumu wa mapigano utakapowekwa. Wakati wa maandamano hayo, waandamanaji walibeba bendera za Palestina na mabango yaliyokuwa yakitoa wito wa kusitishwa kwa uuzwaji wa silaha kwa Israel.
Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa usitishaji wa mapigano, jeshi la Israel katika saa 24 zilizopita limewaua watu 17 na kuwajeruhi zaidi ya 72, huku majeshi yake yakiendelea kuwepo katika maeneo ya Ghaza.
Aidha, Tume Huru ya Umoja wa Mataifa ilitangaza wazi mwezi Septemba kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari huko Ghaza.
Usitishaji wa mapigano uliotangazwa ulianza alfajiri ya siku ya Ijumaa, mara baada ya utawala wa Kizayuni kuupokea rasmi, na kwa sasa unahusisha maeneo ya Ghaza City na Khan Younis, hasa katika usitishaji wa mashambulizi ya mizinga.
Mara baada ya tangazo hilo, UNICEF ilitoa wito wa kufunguliwa mara moja kwa njia zote za mipaka kuelekea Ghaza, ikisisitiza kuwa watoto wa Kipalestina wanateseka sana kutokana na ukosefu wa maji safi na chakula bora kwa muda mrefu wa vita hivi.
Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa zaidi ya watu 700,000 wamekimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi makali ya mabomu na uvamizi wa jeshi la Israel katika jiji la Ghaza na maeneo ya kaskazini.
Chanzo: Middle East Eye
Maoni yako