Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatullah Khamenei katika kikao hicho alimwelezea Allāmah Na’ini kuwa ni nguzo miongoni mwa nguzo tukufu za kielimu na kimaanawi za hawza kongwe ya Najaf, na katika kubainisha vipengele vya utu wake alisema:
“Kwa upande wa taaluma, sifa mashuhuri ya marehemu Na’ini ni kuunda mfumo wa kielimu wa ‘ilm al-usul (misingi ya fiqhi) kwa msingi wa nidhamu ya fikra na elimu, sambamba na ubunifu wake wenye nguvu katika fani hiyo.”
Kiongozi wa Mapinduzi alisema kuwalea wanafunzi mashuhuri nayo ni sifa nyingine muhimu ya Allāmah Na’ini, na akaongeza kusema:
“Sifa nyingine mashuhuri inayomtofautisha yeye na wanazuoni wengine wakubwa ni kuwa na fikra ya kisiasa, jambo lililodhihirika katika kitabu chake cha thamani kilichosahauliwa kwa muda, Tanbīh al-Ummah.”
Mtukufu Ayatullah Khamenei alibainisha kuwa; imani ya kuunda serikali ya Kiislamu kwa msingi wa Wilāyah dhidi ya udikteta ni moja ya nguzo kuu za fikra ya kisiasa ya Allāmah Na’ini, na akaongeza:
“Kulingana na fikra ya kisiasa ya marehemu Na’ini, serikali na wote walio madarakani wanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa kitaifa na wawajibike kwa wananchi. Sharti la jambo hilo ni kuundwa kwa bunge la wawakilishi kupitia uchaguzi, ili liwe na jukumu la kusimamia na kutunga sheria, na uhalali wa sheria za bunge hilo unategemea idhini ya mafaqihi na wanazuoni wakubwa wa dini.”
Yeye alifafanua kuwa mfumo uliokusudiwa na Allāmah Na’ini – yaani serikali ya Kiislamu yenye tabia ya kimaendeleo na ya watu – kwa lugha ya kisasa ndio Jamhuri ya Kiislamu, na kuhusu sababu ya kuandika kitabu Tanbīh al-Ummah na Mirza Na’ini mwenyewe, alisema:
“Harakati ya kikatiba (mashrūṭiyyah) ambayo marehemu Na’ini na wanazuoni wa Najaf waliiunga mkono, kimsingi ilikuwa ni harakati ya kuhimiza kuanzishwa kwa serikali ya haki na kuondoa udikteta. Hivyo basi, ilikuwa tofauti kabisa na ile harakati iliyopandikizwa na Waingereza nchini Iran kwa jina la katiba, ambayo ilisababisha migongano na matukio kama vile kunyongwa kwa kamba marehemu Shaykh Fazlullāh Nūrī.”
Katika kikao hiki, Ayatullah A‘rāfī, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, alitoa ripoti kuhusu mipango na shughuli za Mkutano wa Kimataifa wa kumbukumbu ya Allāmah Na’ini.
Kwa mujibu wa ripoti hii, maandiko kamili ya hotuba ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرّحمن الرّحیم
الحمد لله ربّ العالمین و الصّلاة و السّلام علی سیّدنا محمّد و آله الطّاهرین سیّما بقیّة الله فی الارضین.
Moja ya kazi nzuri sana za Hawza ya Qom ni maadhimisho haya, ambayo kwa hakika nafasi yake ilikuwa wazi. Marehemu Na’ini, wakati mmoja, alikuwa ameijaza anga ya Najaf kwa fikra na maneno yake. Lakini baadaye, kabisa alisahaulika katika uga wa kielimu na kiutafiti, na umuhimu mkubwa kwake haukuonekana.
Naam, huko Qom tuliona kuwa wanazuoni wakubwa walimheshimu, na wanafunzi wake huko Najaf walikuwa miongoni mwa marāji‘ (viongozi wa kidini). Lakini kwa mtu mwenyewe – Allāmah Na’ini (ra) – pamoja na sifa zake maalumu, hakuzingatiwa ipasavyo. Sasa ninyi mnafanya hivyo; InshaAllah vipengele vya kielimu, kimatendo, na kisiasa vyake viwekwe wazi.
Marehemu Allāmah Na’ini bila shaka ni moja ya nguzo tukufu za Hawza kongwe ya Najaf. Hawza ya Najaf, ambayo sasa ina zaidi ya miaka elfu moja tangia ianzishwe, imepitia nyakati za kupanda na kushuka: wakati mwingine ilikuwa na wanazuoni wakubwa, na wakati mwingine ilikuwa tulivu bila kuwa na watu mashuhuri, ukilinganisha na maeneo kama Hillah na sehemu nyingine.
Lakini takriban kuanzia miaka mia mbili iliyopita hadi leo – yaani tangu zama za wanafunzi wa marehemu Āghā Bāqir Bahbahānī, kama marehemu Baḥrul-‘Ulūm na marehemu Kāshif al-Ghitā’ (ambao waliishi Najaf, ingawa mwalimu wao Bahbahānī alikuwa Karbalā) – Hawza ya Najaf ilipata uhai mpya na nguvu za kielimu. Ililea baadhi ya watu mashuhuri wasio na mfano katika historia ya fiqhi na usūl, kama vile Shaykh Anṣārī, mwandishi wa Jawāhir, na marehemu Ākhūnd (ra), na wengine wakubwa wa aina hiyo.
Mtu huyu mkubwa, marehemu Allāmah Na’ini, alikuwa miongoni mwao — mmoja wa watu wenye cheo cha kipekee na mashuhuri kstika zama hizo.
Sifa muhimu zaidi ya marehemu Na’ini katika fani yake maalumu — ambayo ni fiqhi na hasa ‘ilm al-usul — ni “uundaji wa mfumo.” Yeye aliweka misingi ya usul katika mpangilio mpya, kwa fikra mpya, na kwa utangulizi mahsusi katika kila mada. Hili halikuonekana sana katika vitabu vya wanazuoni waliomtangulia.
Sikumbuki mtu yeyote aliyeandika kwa mpangilio na nidhamu kama yake: kila anapoingia katika mada, huanza kwa utangulizi unaofaa, kisha hutiririsha hoja kwa mpangilio na hufikia hitimisho safi kabisa. Labda sababu ya wingi wa wanafunzi na wanazuoni kuhudhuria darasa lake — ambalo lilikuwa darasa la juu zaidi la Najaf baada ya marehemu Ākhūnd — ni kutokana na nidhamu yake ya fikra, nidhamu ya kielimu, na ufasaha wa hotuba yake.
Na pamoja na kwamba yeye (Allāmah Na’īnī) huko Najaf alikuwa akifundisha ‘Ilmu al-Usūl kwa lugha ya Kifarsi — katika mazingira ya Najaf ambako masomo yote hufundishwa kwa Kiarabu — lakini wanafunzi wengi Waarabu walihudhuria darasa lake.
Mimi binafsi sikupata fursa ya kumuona, lakini nimesikia kwamba marehemu Shaykh Ḥusayn Ḥillī (ra), ambaye alikuwa Mwarabu halisi, alikuwa akifundisha Usūl kwa lugha ya Kifarsi, kwa sababu alikuwa amejifunza kutoka kwa mwalimu wake kwa lugha hiyo hiyo ya Kifarsi!
Hii inamaanisha kuwa yeye (Na’īnī) alikuwa na uwezo wa kipekee wa kufafanua mambo kwa uwazi na mantiki ya hali ya juu.
Kwa hakika, ubunifu wake katika misingi ya kielimu ya Usūl ulikuwa wa kipekee mno na mwingi sana. Mambo mapya aliyoyaleta katika masuala mbalimbali ya Usūl ni mengi kwa idadi. Ama yale aliyoelezea na kufafanua kutoka katika maneno ya marehemu Shaykh Anṣārī, au yale aliyoyazusha yeye mwenyewe katika mada tofauti za Usūl, yote hayo ni masuala yenye thamani kubwa ya kielimu. Hilo ni jambo la kwanza.
Kwa mtazamo wangu, moja ya sifa muhimu za marehemu Allāmah Na’īnī ni ulezi wa wanafunzi. Sijawahi kuona mfano wake katika hilo.
Naam, miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa karne za hivi karibuni, marehemu Ākhūnd Khurāsānī alikuwa na wanafunzi wengi sana, na pia waliokuwa mahiri sana — si kwa wingi wa idadi tu, bali kwa ubora wa wanafunzi wake mashuhuri. Vivyo hivyo, marehemu Allāmah Na’īnī naye alikuwa hivyo: alikuwa na wanafunzi mashuhuri wengi mno.
Kulea wanafunzi wenye umahiri wa hali ya juu ni jambo muhimu sana. Katika miaka ninayoyakumbuka — takriban miaka ya ۱۳۷۷ Hijri Qamari (sawa na takriban 1957 Miladia) — karibia Mara'ji wote waliokuwa wakati huo huko Najaf walikuwa wanafunzi wake.
Kama vile Ayatullah al-Khū’ī, marehemu Ayatullah al-Ḥakīm, marehemu Sayyid ‘Abdulhādī (Shīrāzī), na wengine waliokuwepo wakati huo kama marehemu Mīrzā Bāqir Zanjānī, Shaykh Ḥusayn Ḥillī, Mīrzā Ḥasan Bujnūrdī, na wengineo — hawa wote walikuwa wanafunzi wa Bwana Na’īnī.
Naam, baadhi yao, bila shaka, walihusishwa kielimu na wanazuoni wengine pia, kama marehemu al-Ḥakīm ambaye pia alikuwa miongoni mwa wanafunzi mashuhuri wa Āghā Ḍhiyā’, lakini kimsingi, wengi wa hawa wanazuoni wakubwa na marāji‘ wa wakati huo walikuwa wanafunzi wa marehemu Allāmah Na’īnī.
Ulezi huu wa wanafunzi na wingi wa wanafunzi wenye umahiri mkubwa ni miongoni mwa sifa kuu za pekee za Bwana Na’īnī. Hilo linahusu upande wa kielimu wake, ambao nimeugusia kwa ufupi.
Ama kuhusu upande wa pili — yeye alikuwa na kipengele cha kipekee ambacho hakuna miongoni mwa marāji‘ wa karibuni aliyekuwa nacho, — nacho ni masuala ya kisiasa, yaani fikra ya kisiasa.
Fikra ya kisiasa ni kitu tofauti na mwelekeo wa kisiasa. Baadhi ya watu walikuwa na mwelekeo wa kisiasa; kwa mfano marehemu Ākhūnd, marehemu Shaykh ‘Abdullāh Māzandarānī, na wengine waliokuwa wakati huo, walikuwa na mwelekeo wa kisiasa.
Wakati huo hata miongoni mwa wanafunzi wa kidini kulikuwa na mwelekeo wa kisiasa. Sababu yake ni kwamba magazeti ya Misri na Shām (Syria) na mfano wake yalikuwa yakifika Najaf katika maktaba, na magazeti hayo yalikuwa yameathiriwa na Sayyid Jamāluddīn (al-Afghānī) na Muḥammad ‘Abduh na watu wa aina hiyo, ambao walikuwa wakitoa mawazo mapya.
Marehemu Āghā Najafī Quchānī anasimulia katika kumbukumbu zake kwamba; kulikuwa na wanafunzi wengi wa Najaf waliokuwa na mwelekeo wa kisiasa. Vivyo hivyo miongoni mwa wanazuoni kulikuwa pia na waliokuwa na mwelekeo huo.
Lakini mwelekeo wa kisiasa, au kupenda siasa, au hata kuzungumza masuala ya siasa, ni jambo moja; fikra ya kisiasa ni jambo jingine kabisa.
Allāmah Na’īnī alikuwa na fikra ya kisiasa — alikuwa na mtazamo wa kina wa kisiasa.
Kitabu Tanbīh al-Ummah kwa hakika kimeonewa sana (hakijapewa haki yake). Mwenyezi Mungu amrehemu marehemu Ayatullah Ṭalaghānī, ambaye alikichapisha upya kitabu hiki; la sivyo, nakala za awali za kitabu hicho — kama tulivyosikia — zilikuwa zimetolewa kwa mtindo duni na uliopitwa kimaendeleo.
Yeye (Ṭalaghānī) alikichapisha upya, akakiwekea maelezo chini (footnotes) na kukifanyia marekebisho. Hata hivyo, mpaka sasa, kitabu hiki bado kimesahauliwa, ilhali ni miongoni mwa vitabu muhimu sana.
Sasa, nitatoa maelezo mafupi kuhusu masuala yaliyomo katika kitabu hicho.
Kwanza, yeye (Na’īnī) alikuwa na imani kamili juu ya haja ya kuundwa kwa serikali ya Kiislamu. Hili lenyewe ni wazo muhimu — kwamba lazima iundwe serikali ya Kiislamu. Naam, hakubainisha muundo kamili wa serikali hiyo, lakini katika maneno yake ndani ya Tanbīh al-Ummah, ameeleza wazi kwamba ni lazima iundwe serikali ya Kiislamu. Hilo ni jambo la kwanza, na ni jambo muhimu sana.
Jambo la pili ni kwamba kiini cha serikali hiyo ya Kiislamu ni Wilāyah. Yeye anatumia istilahi ya “al-ḥukūmah al-wilā’iyyah”, kinyume na “al-mālikiyyah al-istibdādiyyah” (umiliki wa kidikteta).
Inaonekana kuwa anaeleza kwamba badala ya serikali ya kidikteta au umiliki wa kimabavu, panapaswa kuwa na serikali ya kiwilāyah, yaani serikali ya Kiislamu ya uongozi wa kisheria.
Yaani, muundo, maudhui, na kiini cha serikali hiyo ni Wilāyah — jambo ambalo ni muhimu sana na lenye nafasi kubwa ya kujadiliwa. Yeye ameliweka wazi kabisa jambo hilo. Hichk ndicho kipengele kinachofuata.
Hoja muhimu nyingine sana ni suala la “usimamizi wa kitaifa.” Yeye (Ayatullah Naeini) anaamini kwamba serikali lazima iwe chini ya usimamizi; yaani, viongozi wote wana wajibu na wanapaswa kusimamiwa. Sasa swali ni: nani anapaswa kuwazibiti au kuwachunguza hawa viongozi? Kwa mujibu wa maneno yake, chombo hicho ni “Baraza la Wajumbe Waliotumwa (Majles-e Mab‘uthān)” — yaani, chombo cha kutunga sheria. Kimsingi, baraza hili linakaribiana kimaana na bunge la wawakilishi au kitu kama hicho.
Sasa, ni nani anayelianzisha baraza hilo? Ni watu wenyewe; wananchi wanashiriki katika uchaguzi, na kwa njia hiyo baraza linaundwa. Kisha baraza hilo linafaa kutunga sheria, lakini kutungwa huko kwa sheria hakuna uhalali wowote, hadi zitakapothibitishwa na wanazuoni wakubwa wa kidini — yaani, na Baraza la Wataalamu wa Dini (kama vile Shūrā-ye Negahbān. Yeye mwenyewe anasisitiza waziwazi kuwa sheria ya Bunge la Wajumbe haina uhalali mpaka itakapopata idhini ya wanazuoni wa Kiislamu na mafaqihi wa dini.
Baraza hili la Wajumbe, kwa kuwa linaanzishwa na wananchi, basi uchaguzi unakuwa ni wajibu. Anasema uchaguzi ni wa lazima kifiqhi, kwa kuwa ni “sehemu ya sharti la wajibu” — anatumia neno hilo lenyewe “muqaddimat al-wājib,” akimaanisha kwamba kwa kuwa matokeo yake ni wajibu, basi uchaguzi wenyewe pia unakuwa wajibu. Hivyo anajenga hoja zake juu ya dhana za kidini kama amr bi’l-ma‘rūf wa nahy ‘an al-munkar (kuamrisha mema na kukataza maovu), uwajibikaji kamili, na uwajibikaji wa viongozi.
Yaani, kwa kuangalia hoja zake, yeye anapendekeza mfumo wa kiserikali ambao unajengwa juu ya misingi ifuatayo:
1. Ni serikali yenye nguvu, yenye mamlaka.
2. Chanzo chake ni wananchi – watu wenyewe ndio wanaochagua.
3. Ni inayolingana na mafundisho ya kidini na sheria za Mwenyezi Mungu – bila hayo haina maana.
Kwa hivyo, ni serikali ya Kiislamu na ya wananchi. Tukitumia maneno ya leo, mfumo huu unalingana na dhana ya “Jamhuriyya ya Kiislamu ” — “Jamhuriyya” ikimaanisha kuwa ni ya wananchi, na “islamu” ikimaanisha kuwa ni ya kidini. Ingawa yeye mwenyewe hakutumia istilahi hizi kwa namna ya kisasa, maana ya kauli yake ni hiyo hiyo: serikali inayoundwa na watu wacha Mungu, wenye imani, waliochaguliwa na wananchi, chini ya usimamizi mkali wa wananchi, ambapo viongozi wa kila sekta wana uwajibikaji kamili na wanapaswa kutoa majibu kwa maswali yote; na baraza la wawakilishi linatunga sheria, lakini sheria hizo hazina uhalali bila idhini ya wanazuoni wa dini. Hizo ndizo fikra zake — na kweli ni jambo muhimu sana.
Sasa, sisi tunasoma mafundisho ya Ayatullah Naeini mkubwa huyu, tunanufaika nayo, tunafundisha kutokana nayo, lakini hatuleti misingi yake ya kifiqhi katika uangalizi wa kina. La kuvutia ni kwamba yeye hakuzungumza kwa maneno ya kisiasa tu, bali alijenga hoja zake kwa misingi ya fiqhi safi — kwa usahihi wa hoja, umakini na uchambuzi wa kielimu wa kina, kama ambavyo mwanazuoni mkubwa wa fiqhi anavyofanya. Alizingatia dalili za vyanzo vya dini pamoja na muktadha wa kijamii (ʿurf), kama inavyofanyika katika fiqhi ya kawaida.
Kwa mtazamo wangu, huyu ni miongoni mwa wanazuoni wa kipekee kabisa, kwani ni nadra mno kumpata miongoni mwa wanazuoni waliomtangulia mtu mwenye uwiano huu wa kielimu na kifalsafa.
Na hata Marehemu Akhund Khorasani, ambaye aliandika tanbihi ya kitabu hiki, alikikubali kikamilifu. Akhund hakuwa mtu wa daraja ya chini, bali alikuwa ni mwanazuoni mkubwa mno, na kwa maoni yangu alikisoma kwa undani na akanufaika nacho. Kwa mtazamo wetu, kitabu “Tanbīh al-Ummah wa Tanzīh al-Millah” ni kati ya vitabu muhimu sana vilivyowahi kuandikwa.
Kisha anahitimisha kwa kusema: sasa jukumu linawaangukia wale waliohusika kukusanya nakala za kitabu hiki na kuziondoa. Kwa dhahiri, jambo hili lilitokea; kwani, kwa mujibu wa simulizi tulizosikia kutoka kwa waliokuwa Najaf na marafiki wa marehemu baba yetu waliokuwa huko, walisema kwamba Naeini mwenyewe alijaribu kwa juhudi kukusanya nakala za kitabu hicho — akinunua kutoka kwa yeyote aliyekuwa nacho ili kisiendelee kusambaa.
Sababu yake ni ipi? Ni kudhani kwamba mwanazuoni wa kiwango cha juu, mwenye nguvu kubwa za hoja, anaandika kitabu, kisha anageuka kiasi cha kukataa mwenyewe kazi yake! Hilo halina maana kabisa. Mafaqihi wanaweza kubadilisha mitazamo yao ya kifiqhi, lakini hawafuti wala hawakusanyi vitabu vyao.
Sababu halisi ni kwamba ile harakati ya Kikatiba (Mashrūṭiyyah) iliyokuwa imeenea Najaf haikuwa ile halisi iliyotokea baadaye. Wale kama Akhund Khorasani, Sheikh Abdullah Mazandarani, na wengine walikuwa wakipigania kitu tofauti — walitaka serikali ya uadilifu, kuondoa dhulma na istibdād (udikteta).
Lakini neno “mashrūṭeh” (katiba) na mfumo wake kwa sura tuliyoiona vililetwa na Waingereza — wao ndio waliopendekeza jina hilo na wakauchora mwenendo wake.
Naam, jambo lililofanywa na Waingereza lilikuwa wazi kabisa kuwa ni wapi litafikia: lilizua migawanyiko, mizozo na fitina mbalimbali, hadi ikafikia mahali ambapo mtukufu Shaykh Fadlullah Nūrī alinyongwa, Sayyid ‘Abdullah Behbahānī akauwawa kwa mauaji ya kisiasa, na Sattār Khān pamoja na Bāqir Khān wakateketezwa kila mmoja kwa namna yake.
Wakati habari hizi zilipofika Najaf, wanazuoni waliokuwa wamelitegemeza jambo hili walijuta kwa kuunga mkono harakati hiyo. Kwa mtazamo wangu, Ayatullah Naeini alikuwa katika hatua hii: alitambua kuwa kwa kitabu chake cha kielimu, kifiqhi na chenye hoja thabiti, alikuwa amesaidia jambo ambalo hakulikubali — jambo ambalo alipaswa kulipinga.
Na jambo hilo halikuwa jingine ila “Mashrūṭiyyah” (katiba) ile iliyopangwa na Waingereza nchini Iran, bunge walilolianzisha wao, na matukio mabaya yaliyofuata, kama kuuawa kishahidi kwa Shaykh Fadlullah Nūrī na mengineyo.
Kwa maoni yangu, yeye alikuwa mwanachuoni wa kipekee mno, katika nyanja zote, Kielimu, alikuwa katika ngazi ya juu sana; kiutendaji, alijulikana kwa uchaji Mungu, zuhdi, na maarifa ya kina ya kiroho. Imenukuliwa kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na Akhund Mullā Husayn-Qulī Hamadānī; yaani, wakati alipokuwa akitoka Sāmarrā kuelekea Najaf, alikuwa akimzuru marehemu huyo.
Pia alikuwa na uhusiano na Mullā Fath‘Alī Samarrā’ī, ambaye naye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kiroho. Hivyo basi, alikuwa katika mawasiliano na viongozi wa juu wa elimu na ma‘rifa.
Kadhalika alipokuwa Isfahan, alikuwa karibu na Jahangīr Khān Qashqā’ī na wengineo. Inasemekana hata alisoma falsafa chini ya Jahangīr Khān, jambo linaloonesha kwamba alikuwa na ufahamu wa elimu za falsafa na alikuwa mtu wa maana na uchaji mkubwa.
Siku chache zilizopita, nilisikia kutoka kwa baadhi ya wanazuoni wakubwa simulizi kuhusiana na namna ya sala ya usiku ya Ayatullah Naeini — ikisimuliwa na Agha Najafī, mkwe wake aliyekuwa Hamadān, ambaye alikuwa amemuona mwenyewe.
Alisimulia kuwa Ayatullah Naeini alikuwa akisali kwa hali ya unyenyekevu wa ajabu, kwa du‘ā na munājāt zenye uchungu na unyenyekevu wa kina; hali ambayo inadhihirisha roho yake ya kipeke.
Ni wazi kwamba hali kama hizi za kiroho ndizo humsaidia mtu kupata mwanga wa haki, kumuonesha njia sahihi, na kumfikisha kwenye matokeo ya kweli.
Tunatarajia, in shā’ Allāh, kwamba mkusanyiko huu wenu wa kielimu na kihistoria, iwe ni Qom, Najaf, au Mashhad, utafanikiwa vyema.
Na hukk Mashhad, mmefanya vizuri mno. Kwa hakika, marehemu Ayatullah al-Mīlānī ndiye aliyefufua jina na fikra za Ayatullah Naeini huko Mashhad.
Kwa sababu, huko Mashhad, kwa muda mrefu, kutokana na uwepo wa mwana wa Akhund Khorasānī, fikra za Akhund ndizo zilikuwa zimetawala. Lakini baadaye, Mīrzā Mahdī Isfahānī, mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Mīrzā Naeini, alipofika Mashhad, aliuvunja ule utawala wa fikra za Akhund, na akaeneza fikra mpya za kielimu, zenye hoja za kina na mantiki mpya.
Marehemu baba yetu — ambaye alihudhuria masomo ya wote wawili, Aqāzādeh na Mīrzā Mahdī — alikuwa akisema: “Wakati Mīrzā Mahdī alipofika Mashhad, mazingira yote ya kielimu ya usul, yaliyokuwa yakifuata mtazamo wa Akhund, yalibadilika kabisa.”
Lakini baada ya kufariki Mīrzā Mahdī, jina la Naeini lilianza kusahaulika. Ni Ayatullah Mīlānī aliyefufua upya fikra na hoja za marehemu Naeini; alikuwa akizinukuu, kuzijadili, wakati mwingine kuzikosoa, na mara nyingi kuzikubali.
Kwa hivyo, mmefanya vyema sana kwamba mliweka tawi la kumbukumbu yake huko Mashhad, na Najaf bila shaka inafahamika nafasi yake. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie nyinyi wote taufiki na ulinzi Wake.
Wassalāmu ‘alaykum wa rahmatullāhi wa barakātuh.
Maoni yako