Ijumaa 24 Oktoba 2025 - 12:47
Ni Vipi Tutafahamu Kwamba Mungu  Peke Anatosha

Hawza/ Wakati miangaiko ya kidunia inapomtoa mwanadamu katika njia ya uja na utumishi wa Mwenyezi Mungu, Imam Sajjad (a.s) anatupa ufunguo wa dhahabu wa ukombozi: kuomba kutoshelezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Shirika la Habari la Hawza - Imam Zaynul-‘Ābidīn (a.s) katika Sahifat Sajjadiyyah anamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutumia maneno haya:

«وَاکْفِنِی مَا یَشْغَلُنِی الاِهْتَمامُ بِهِ.»

“Na unitosheleze mimi katika mambo ambayo kuyashughulikia hunifanya nijishughulishe (na dunia).” (1)

Sherehe:
Mara nyingi hutokea kwamba mwanadamu anaazimia kutenda jambo jema, lakini kuna mambo yanayozuia kutendeka kwa jema hilo au kucheleweshwa. Wakati mwingine mtu hulazimika kujihusisha mno na baadhi ya mambo ya kidunia — ambayo mara nyingi hayana thamani — kiasi cha kwamba huachwa nyuma katika malengo na masuala ya kiroho na yenye thamani ya kweli.

Imam Sajjad (a.s) anatufundisha kwamba tumuombe Mwenyezi Mungu Mtukufu atutosheleze katika mambo yetu, ili katika njia ya  kumcha yeye na kufikia malengo ya kimungu, kisipatikane chochote kitakachotuchelewesha au kutuzuia.

Mwenyezi Mungu katika Qur’ani anasema:

«أَلَیْسَ اللَّهُ بِکَافٍ عَبْدَهُ.»

“Je, Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza kwa mja Wake?!” (2)

Kwa hakika, kupitia maneno mazuri ya Imam Sajjad (a.s) tunaweza kuitikia wito huu wa Mwenyezi Mungu katika Qur’ani kwa kusema:

Ndiyo, Ewe Mola wangu! Hakika Wewe ni mwenye kunitosheleza.

Ewe Mungu wangu! Wewe watosha kabisa katika kunisimamia na kushughulikia mambo yangu.

«وَکَفَیٰ بِاللَّهِ وَلِیًّا.»

“Na Mwenyezi Mungu yatosha kuwa ni Msimamizi (Mlinzi).” (3)

Ewe Mungu wangu! Wakati wa matatizo, msaada na nusra Yako yanitosheleza.

«وَکَفَیٰ بِاللَّهِ نَصِیرًا.»

“Na Mwenyezi Mungu yatosha kuwa Msaidizi.” (4)

Ewe Mungu wangu! Wakati wa vishawishi vya nafsi na shetani, uongofu Wako wanitosheleza.

«وَکَفَیٰ بِرَبِّکَ هَادِیًا.»

“Na Mola wako yatosha kuwa ni Mwongozaji.” (5)

Na Ewe Mungu wangu! Nategemea na kutawakali kwako peke Yako; kwani Wewe watosha kunilinda na kunitetea.

«وَکَفَیٰ بِاللَّهِ وَکِیلًا.» 

“Na Mwenyezi Mungu yatosha kuwa ni Mwakilishi (Mlinzi wa mambo yote).” (6)

Rejea:
1. Sahifa Sajjadiyyah, Dua ya Ishirini (Dua ya Makarimul-Akhlāq).
2. Sūratu Zumar, aya ya 36.
3. Sūratu Nisaa, aya ya 45.
4. Aya hiyo hiyo (Sūratu Nisaa).
5. Sūratu Furqān, aya ya 31.
6. Sūratu Ahzāb, aya ya 3.

Imeandaliwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha