Jumatano 5 Februari 2025 - 09:40
Risala ya Imam Sajjad kuhusu Sheria ni dhihirisho la uadilifu

Ayatollah Nouri Hamedani amesema: Kwa mujibu wa ushahidi wa historia, moja ya nukta angavu katika maisha ya Hadhrat Sajjad (amani iwe juu yake) ni kwamba alikuwa hakubaliani na watawala madhalimu, na khutba zake huko al-Kufa na Sham ziko wazi kabisa na ni ushahidi ulio bayana wa dai hili. Lakini walimuarifisha kuwa alikuwa mbali na masuala ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawzat, Ayatollah Hossein Nouri Hamedani alisema katika ujumbe wake kwa Kongamano la Kimataifa la Imam Sajjad (amani iwe juu yake):

Ingawa uso angavu na mashuhuri wa Imamu Sajjad (amani iwe juu yake) umepotoshwa na baadhi ya marafiki wasio na ufahamu na maadui wenye ufahamu wa kutosha na wamemdhihirisha (Imamu huyo) kuwa ni mtu ambaye alikuwa ni mgonjwa daima na aliye mbali na masuala ya kisiasa, lakini kwa mujibu wa historia, moja ya nukta angavu katika maisha yake alikuwa hana makubaliano (hana muafaka, wala kukubaliana kabisa) na watawala madhalimu, na mahubiri yake huko al-Kufa na Sham ni uthibitisho wa wazi wa dai hili.

Maandiko ya ujumbe huu ni kama ifuatavyo: Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na rehema na amani ziwe juu ya Bwana wetu na Mtume wetu, Abu Al-Qasim Al-Mustafa Muhammad, na pia ziwe juu ya Aali zake wema na Watoharifu, hasa kwa Baqiyyatullah ardhini.

Salamu na pongezi za Mnasaba wa Eid / Sikukuu za Shabaniyah (Mwezi wa Sha'ban) ziwafikie kwenye Mkutano adhimu unaoendelea kufanyika.

Moja ya vipindi muhimu vya kihistoria ni matukio ya maisha ya Hadhrat Ali bin Al-Hussein (amani iwe juu yake). Ingawa uso unaong'aa na mashuhuri wa Imam Sajjad (amani iwe juu yake) umepotoshwa na wale baadhi ya marafiki wasiokuwa na ufahamu na maadui wenye ufahamu wa kutosha, na wakamdhihirisha Imamu huyo kama mtu aliyekuwa mgonjwa daima na kwamba alikuwa mbali na masuala ya kisiasa, lakini kiuhalisia na kwa mujibu wa ushahidi wa historia, moja ya maeneo angavu katika maisha yake, hakuwa akikubaliana kamwe na watawala madhalimu, na mahubiri yake huko al-Kufa na Sham ni uthibitisho wa wazi wa dai hili.

Kufichuliwa kwa dhulma na ukatili na jinai za Serikali ya Bani Umaiyyah na la muhimu zaidi, kuwaarifisha familia ya Mtume (s.a.w.w) kama viongozi wa kweli, kulisababisha mwamko wa watu wa al_Kufa na Sham.

Ingawa aliishi katika hali mbaya zaidi ya wakati ule na alikuwa chini ya shinikizo kubwa zaidi kutoka kwa watawala (hao waovu), lakini tunaona kuwa alikuwa wa kipekee katika kueneza imani na kuhuisha Uislamu safi wa Muhammad na njia ya Babu yake Mtukufu, ingawa watawala waovu na madhalimu wa wakati huo walikuwa wakifuatilia kwa umakini harakati za Imamu ambazo zilikuwa ni harakati za kiungwana na hawakuruhusu kumpa nafasi ya matengenezo (masahihisho) ya kijamii.

Wanasayansi na watafiti wengi wa Kiislamu wanaona zama za Imamu Sajjad (amani iwe juu yake) kuwa zilikuwa zama za giza zaidi kisiasa na kiutamaduni, na wanazitaja kuwa ni zama za kuanguka kwa utamaduni wa Kiislamu. Katika zama hizo, pamoja na mateso, kuua na kunyonga, maadili ya Kiislamu pia yalikuwa yamefikia kiwango chake cha chini kabisa na ni jina tu la Uislamu lililobakia, na ambalo pia lilikitajwa ili kupata nguvu (za Utawala) na kupata mkate, na hakuna mtu alikuwa na hamu ya kujua maagizo / maelekezo / na mafundisho ya Uislamu.

Imam Sajjad (amani iwe juu yake) anasema kuhusu hali yake:

Wakati wetu miongoni mwa watu wetu ni kama wakati wa Waisraeli baina ya Mafarao walioua Vijana wa kiume (wavulana) na kuwazika wasichana wakiwa hai.

Leo, hali ni ngumu kwetu kiasi kwamba watu wanatafuta ukaribu kwa maadui zetu kwenye mimbari kwa sababu ya kumtukana Kiongozi wetu.

Imamu Sajjad (amani iwe juu yake) alijaribu kuutenganisha Uislamu na ukengeufu, na akatumia swala ambayo hadi wakati huo ilikuwa ikijulikana kuwa ndiyo njia pekee ya kuwasiliana na Mwenyezi Mungu, kuwa ndiyo njia bora ya kupambana na upotovu na upotofu wa mfumo wa Bani Umaiyyah, na mengine mengi zaidi.

Alifundisha elimu safi katika muundo huu kwa jamii ya Kiislamu na kwa wapenda ukweli (na Haki), kiasi kwamba Kitabu cha Sahifat al_Sajjadiyyah ni moja kumbukumbu ya zama hizo.

Ingawa uadilifu na usawa ni moja ya nguzo muhimu za Uislamu, lakini wakati wa Uimamu, ubaguzi na dhulma kali ziliwekewa jamii ya Kiislamu na watawala wa Bani Umaiyyah, Risala ya Imam Sajjad (Amani iwe juu yake) kuhusu Haki ni moja ya mifano muhimu katika uamsho (na uhuishaji) wa maadili ya Kiislamu na udhihirisho wa Haki na kuzingatia usawa, na kuonya watu dhidi ya kukiuka Haki za Binadamu wenzao.

Katika Risala hii, anaichukulia Serikali kuwa ina wajibu wa kutenda Haki, kuwa Baba mwema na Mkarimu, ili kuendeleza manufaa ya watu wote kwa watu wote. Katika dhana hii, mfumo wa utawala unapaswa kuwa na wema, sio tu kwa marafiki zake, bali pia kutenda wema kwa kila mtu, na usiishie kuwa mlezi tu, bali uwe na huruma na uwe Baba katika utumishi wa watu na kuzuia dhuluma, ubaguzi, na kupoteza Haki za wanyonge.

Mwisho, ninahisi ni muhimu kuwashukuru wale wote waliohusika katika mkutano huu adhimu, hasa Mwakilishi Mheshimiwa wa Waliyul_Faqih katika Mkoa wa Hormozgan, ambaye alifuatilia suala hili kwa juhudi kubwa katika miaka ya hii yote, na ninamuomba Mwenyezi Mungu Taufiq na Mafanikio kwa ajili ya kila mtu.

Amani iwe juu yenu pamoja na Rehema za Mwenyezi Mungu na Baraka Zake.

Hossein Nouri Hamedani

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha