Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika hotuba yake ya kwanza, Ayatollah Khamenei aliwapongeza wananchi wa Iran na waislamu wote kwa mnasaba wa Eid al-Fitr, pamoja na sikukuu ya Nowruz na kumbukumbu ya tarehe 12 Farvardin, siku ambayo mfumo wa Jamhuri ya kiislamu ulipitishwa rasmi na wananchi, alieleza kuwa: Ramadhani ya mwaka huu imekuwa mwezi wa ustawi wa kiroho na kisiasa, ambapo wananchi wameonyesha msukumo mkubwa wa imani.
Akitaja fadhila za mwezi wa Ramadhani, alieleza kuwa ni moja ya neema kubwa za Mwenyezi Mungu, fursa adhimu kwa waja wake kujikurubisha naye, kujisafisha kiroho na kuimarisha maisha ya kiimani. Alisisitiza kuwa ibada za kufunga, usomaji wa Qur’ani, usiku wa Laylatul Qadr, na maombi ya unyenyekevu ni nyenzo muhimu za kujenga imani za waumini.
Kiongozi wa Mapinduzi alitaja kuongezeka kwa mahusiano na Qur’ani, kuenea kwa utoaji wa sadaka, na maandalizi ya futari katika misikiti, vituo vya kidini, na maeneo ya umma, pamoja na ushiriki mkubwa, hasa vijana katika ibada na dua, kuwa ni miongoni mwa sifa za mwezi wa Ramadhani uliojaa utajiri wa kiroho kwa taifa la Iran. Alisisitiza kwamba kila mtu anapaswa kujitahidi kutumia na kuhifadhi manufaa ya kiroho yaliyopatikana katika mwezi huu hadi Ramadhani ijayo.
Alitaja matembezi ya siku ya kimataifa ya Quds kuwa ni ujumbe mzito kwa wale wanaotaka kuielewa Iran na msimamo wake thabiti.
Katika hotuba yake ya pili, Ayatollah Khamenei alilaani kuendelea kwa mauaji ya halaiki na ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watoto wa Gaza na Lebanon, akisisitiza kuwa jinai hizi zinaungwa mkono na Marekani.
Alieleza kuwa utawala wa Kizayuni ni chombo cha uwakilishi wa mabeberu katika eneo hilo na akaongeza kuwa: Mataifa ya Magharibi yanawatuhumu wapiganaji huru kama mawakala wa nje, lakini ukweli ulio dhahiri ni kwamba wakala halisi wa mabeberu ni utawala huu fisadi, ambao kwa uchochezi wa vita, mauaji ya halaiki, na uvamizi wa mataifa mengine, unaendeleza na kutimiza njama za mataifa yaliyojipa mamlaka juu ya eneo hili baada ya vita kuu ya pili ya Dunia.
Kiongozi wa Mapinduzi alielezea madai ya upingaji ugaidi yanayotolewa na mabeberu wanaotawala dunia kwa kutumia fedha na vyombo vya habari, akisema: Wale wanaotaja juhudi za mataifa katika kutetea haki zao na ardhi yao kuwa ni ugaidi na uhalifu, ndio hao hao wanaofumbia macho mauaji ya kimbari na vitendo vya wazi vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni, au hata kusaidia vitendo hivyo moja kwa moja.
Akitaja mauaji ya viongozi kama Abu Jihad, Fathi Shaqaqi, Ahmad Yassin, na Imad Mughniyeh katika nchi mbalimbali mikononi mwa utawala wa kizayuni, pamoja na mauaji ya mara kwa mara ya wasomi wa Iraq yanayofanywa na utawala huo, alisema: Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi yanaunga mkono vitendo hivi vya kigaidi, huku ulimwengu mzima ukishuhudia tu.
Hadhrat Ayatollah Khamenei aliikosoa vikali jamii ya kimataifa kwa kutofanya lolote kuhusu kuuawa kwa zaidi ya watoto 20,000 wa Kipalestina katika kipindi cha chini ya miaka miwili, akisisitiza kuwa kama ulimwengu ungepewa taarifa sahihi, maandamano dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni yangeenea zaidi.
Alisisitiza kwamba: Kundi hili la wahalifu, waovu na wauaji lazima liangamizwe kabisa kutoka Palestina na maeneo yote, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, jambo hili litafanyika, aidha alisisitiza kuwa juhudi za kufanikisha hili ni jukumu la kidini, kimaadili na kibinadamu kwa watu wote duniani.
Kiongozi wa Mapinduzi aliashiria uthabiti wa msimamo wa Jamhuri ya kiislamu katika sekta hii na kusema: "Msimamo wetu ni thabiti na uadui wa Marekani na utawala wa Kiyahudi bado ni kama ilivyokuwa zamani."
Hadhrat Ayatollah Khamenei katika hitimisho la hotuba yake ya pili, alitoa tahadhari mbili kwa Marekani: Kwanza, ikiwa Marekani au utawala wa Kizayuni utafanya kitendo cha kichokozi, watakabiliana na jibu kali na madhubuti. Pili, ikiwa watajaribu kuanzisha fitina ndani ya Iran, wananchi wa Iran watawapa jibu kali kama walivyofanya huko nyuma.
Maoni yako