Kwa mujibu wa repoti kutoka katika Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hadhrat Ayatollah Haj Hafidh Najafi alikutana na wageni hao katika Markaz yake, Kituo hicho cha elimu kina jukumu muhimu katika kulea na kuwafundisha watoto kwa misingi ya Qur’ani, kikiwa na lengo la kueneza utamaduni wa kiislamu kupitia elimu ya Qur’ani.
Katika kuonana nao, Ayatollah Bashir Najafi aliwasisitizia watoto umuhimu wa kuwaheshimu wazazi wao na kuwa na mafungamano ya karibu na Qur’ani, aliwaambia: "Tengenezeni urafiki na Qur’ani, ipokeeni Qur'an kwa moyo na roho zenu, na muishi katika mazingira ya Qur’ani."
Aidha, aliwakumbusha umuhimu wa kuzingatia matamshi sahihi ya herufi wanaposoma Qur’ani, huku akiwaonya kuwa kusoma Qur'an bila uangalifu kunaweza kusababisha makosa katika usomaji wa aya za Qur’ani.
Kwa upande wa walimu, aliwataka wazingatie wajibu wao wa kuwafundisha wanafunzi wao kusoma Qur’ani kwa usahihi, na kuhakikisha wanawaelekeza watoto katika njia inayofaa.
Ayatollah Bashir Najafi pia aliwahimiza watoto kuwaheshimu wazazi wao kwa kusema: "Mnapowatendea wema wazazi wenu, hadhi na daraja lenu mbele ya Mwenyezi Mungu huongezeka, hususan jitahidini mjipatie nafasi katika nyoyo za mama zenu na mnufaike na dua zao njema, kwani dua ya mama kwa mwanawe huwa na baraka na hukubaliwa na Mwenyezi Mungu."
Maoni yako