Jumapili 23 Machi 2025 - 05:57
Ayatullah Khamenei: Ikiwa Marekani itafanya ukhabithi dhidi ya taifa la Iran, itazabwa kofi kali

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameionya Marekani dhidi ya kutumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran.

Shirika la Habari la Hawza - Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya wa Hijria Shamsia mapema Ijumaa jijini Tehran katika mkutano na wananchi wa matabaka mbali mbali, Ayatullah Khamenei amesema kuwa maadui watazabwa kofi kali la usoni iwapo watafanya kitendo chochote kiovu dhidi ya Iran.

"Marekani inapaswa kujua kwamba katika kukabiliana na Iran, kamwe haiwezi kufika popote kwa kutumia vitisho", amesema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu.

Aameongeza kuwa, "Marekani na wengine wanapaswa kujua kwamba ikiwa watachukua hatua yoyote mbaya dhidi ya taifa la Iran, watazabwa kofi kali la uso."

Ayatullah Khamenei aidha ameashiria chuki ya mataifa mbalimbali dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala dhalimu wa Israel na kuitaja lugha ya vitisho dhidi ya taifa kubwa la Iran kuwa haina tija. Amesema: Mataifa na vituo vya kambi ya muqawama na mapambano wakiwemo watu wa Palestina, Lebanon na Yemen, vinakabiliana na utawala mbovu na fasiki wa Kizayuni kutokana na misukumo ya ndani na ya kidini.

Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran linasimama kidete kukabiliana na ukatili na uonevu wa maadui wa nchi yao na limetangaza wazi msimamo wake wa kuwaunga mkono wapiganaji wa Palestina na Lebanon ambao wanazilinda nchi zao.

Nini maana ya wapiganaji wa niaba? 

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameponda matamshi yanayotolewa na wanasiasa wa Marekani an Ulaya wakivitaja vituo vya muqawama kuwa ni vikosi vinavyopigana kwa niaba ya Iran akiyataja kuwa ni kosa kubwa na ni matusi kwa makundi hayo. Amehoji: "Nini maana ya wapiganaji wa niaba? Wananchi wa Yemen na vituo vya muqawama katika eneo hili vina msukumo wa ndani wa kusimama dhidi ya Wazayuni, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haihitaji wakala, na maoni yetu na yao yako wazi."

Akisisitiza upinzani wa mataifa dhidi ya maovu yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, na muqawama wao dhidi ya utawala huo kwa njia zote zinazowezekana, ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imesimama kidete kukabiliana na maovu hayo na imetangaza waziwazi misimamo na mbinu zake za daima kwamba itawaunga mkono wapiganaji wa Palestina na Lebanon wanaoilinda nchi zao.

Iran haijawahi kuanzisha vita

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amesisitiza katika kujibu vitisho vya maadui wa Iran kwamba: "Hatujawahi kuanzisha vita na mapigano, lakini iwapo mtu yeyote ataanzisha mapigano kwa chuki, ajue kwamba atazabwa makofi makali."

Akizungumzia kushamiri maandamano ya kupinga jinai za utawala dhalimu wa Israel  katika mataifa yasiyo ya Kiislamu na maandamano wananchi na wanafunzi wa vyuo vikuu huko Marekani na katika nchi za Ulaya, Ayatullah Khamenei amesema: "Viongozi wa nchi za Magharibi hawataki kuona ukweli huo wala kuelewa misimamo ya mataifa yao; Kwa hiyo, wanakimbilia kwenye vitendo kama vile kukata bajeti ya chuo kikuu ambacho wanafunzi wake wamefanya maandamano kuitetea Palestina, jambo ambalo, bila shaka, ni dhihirisho la madai yao kuhusu mtiririko huru wa habari, uliberali, na haki za binadamu.

Umuhimu wa Nahjul Balagha kwa Umma wa Kiislamu

Ayatullah Khamenei ameelezea kipindi cha sasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni maalumu kwa ajili ya kwa Imam Ali (AS) na amesisitiza kuwa watu wa Iran na mataifa ya Kiislamu wanapaswa kugeukia Nahj al-Balaghah ili kujifunza kutoka kwa Imam Ali (AS), ambaye anachukuliwa kuwa mwanadamu bora zaidi baada ya Mtume Muhammad (SAW). Pia amewashauri watu walioko katika uwanja wa kitamaduni "kutilia mkazo maalum katika kusoma na kufundisha kitabu hiki bora." Imam Khamenei pia ameelezea Usiku wa Qadr kama fursa ya thamani kwa ajili ya Swala na dua kwa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa ibada katika kipindi hiki , hasa miongoni mwa vijana, inaweza kubadilisha hatima ya mtu binafsi na taifa zima.  

Chanzo: IQNA 

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha