Kwa mujibu wa ripoti kotoka katika idara ya tarjama Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Sajid Ali Naqvi Raisi wa Shura ya Ulamaa Pakistani katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Eid al-Fitr, ameeleza kuwa siku hii siyo tu alama ya furaha na shangwe, bali pia ni fursa ya kudhihirisha umoja na mshikamano kwa umma wa kiislamu.
Aliwapongeza Waislamu wote Duniani kutokana na mnasaba wa Eid hii tukufu na kusisitiza kuwa, siku hii inatufundisha kutekeleza wajibu wa kiislamu wa umoja na mshikamano kama ulivyoelekezwa katika Qur’ani na mafundisho ya Mtume mtukufu (saw).
Raisi wa Shura ya Ulamaa Pakistani alisisitiza kuwa: Eid inapaswa kuwa mwanzo wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kijamii, na kwamba waislamu wanapaswa kudumisha umoja huu kwa ari na ikhlasi hadi Eid inayo fuata.
Mwanazuoni huyu aliashiria kuhusiana na hali ya wasiwasi inayo ukumba ulimwengu wa kiislamu hususan Palestina na Kashmir, na kubainisha kuwa: Eid siyo siku ya kusherehekea tu, bali ni fursa ya kuifanya upya ahadi katika harakati za kudai haki na kutetea wanyonge. Alisisitiza kuwa ukombozi wa Msikiti wa Al-Aqsa, kuondoshwa vizuizi kwa Gaza, na kukomesha mateso ya watu wa Kashmir ni masuala yanayopaswa kuendelea kuwa kipaumbele katika umma wa kiislamu wenye dhamira hai.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Sayyid Sajid Ali Naqvi aliwataka Waislamu wote kutumia siku hii takatifu siyo tu kwa kusambaza upendo na huruma katika jamii, bali pia kwa kujitahidi kuondoa matatizo yanayoukabili ulimwengu wa kiislamu na kuunga mkono harakati za ukombozi na mapambano ya wanyonge.
Maoni yako